Habari za Punde

Miundombinu na Mawasiliano yapinga kutolewa mashindanoni


Na Mwajuma Juma

TIMU ya Soka ya Miundombinu na Mawasiliano imetuma barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Rais Dkt Khalid Salum Mohammed ya kutaka asimamishe michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa timu za Mawizara na taasisi za Serikali hadi pale utakapopatikana ufumbuzi wa tatizo lao la kupokonywa pointi sita na kamati  inayosimamia michuano hiyo.

Barua hiyo ya Novemba 25 mwaka huu, iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Rajab Uweje Yakoub imesema kuwa wizara imepokea kwa masikitiko makubwa kunyang’anywa kwa pointi sita ambazo zimewafanya waondolewe moja kwa moja katika michuano hiyo wakati tayari walikuwa wameshaingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Hivyo barua hiyo imeeleza kuwa kupitia barua hiyo inamuomba Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuyasimamisha mashindano hayo na kulipatia ufumbuzi suala hilo.


“Kwa barua hii wizara yetu inakuomba Katibu Mkuu kuyasimamia mashindano haya na kulipatia ufumbuzi suala hili kwanza kabla ya mashindano haya kuendelea”, ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Akizungumzia suala hilo Katibu Khalid alisema kuwa bado ofisi yake haijapokea barua hiyo, hivyo hawezi kuzungumza chochote hadi pale atakapopokea barua.

“Jana (juzi) nilizungumza na uongozi wa timu hiyo ya wizara lakini walisema wataleta barua lakini mapaka tunaongea mimi na wewe sijapokea barua yao hivyo sitoweza kuzungumza chochote”, alisema.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa na Kamati inayosimamia michuano hiyo yenye kumbukumbu namba OMPR/S.40/C.4/VOL.III/03 ya Novemba 22 mwaka huu, imesema kuwa imeipokonya pointi timu hiyo baada ya kumchezsha mchezaji Othman Haidar ambae si mfanyakazi halali wa wizara hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mohammed Azan alisema kuwa maamuzi ya kamati hiyo yaliyokana na maamuzi ya kikao cha kamati ya michuano hiyo kilichokaa Novemba 21 mwaka huu, ambacho kilishirikisha viongozi kutoka timu zote 14 zinazoshiriki michuano hiyo.

Hata hivyo alisema kuwa mpaka sasa hawajapokea barua ya kusimamishwa kwa mashindano hayo na yanaendelea kama kawaida.

Hata hivyo Katibu wa timu hiyo Salum Mohammed amesema kuwa kuondolewa kwa timu hiyo kumetokana na njama za makusudi zilizofanywa na kamati hiyo ya kutaka kuingiza timu yao ya Ofisi ya Makamu wa Pili ambayo ilifungwa katika mechi mbili na kutoka sare mechi moja.

Alisema kuwa haiwezekani wawaandikie barua ya kuwanyang’anya pointi huku timu ikiwa tayari imeshamaliza kucheza mechi zote na kuingia katika hatua ya nusu fainali.

“Huu ni mchezo wa makusudi umechezwa kwa kutaka kuwaondowa katika michuano hiyo hii na kuingiza timu wanazotaka wenyewe”, alisema.

Nae Kocha wa timu hiyo Nassor Mwinyi Bwanga amesema maamuzi hayo yamewathiri kw akiasi kikubwa hasa kutokana na kuwa barua ya kuondolewa kwake wameipata kwa muda ambao tayari alishakwisha kuwaandaa wachezaji wake.

“Maamuzi kwa kiasi yameniathiri kisaikolojia na hatua hii kwa kweli hairidhishi na wamefanya hivi kwa kuwa wanamipango yao ya kutaka kuingiza timu yao ambayo haina uwezo wowote”, alisema.

Hivyo alishauri katika michuano inayofuata waingizwe viongozi wa ZFA ili waweze kusimamia sheria za mchezo huo kuliko ilivyo sasa ambayo yameendeshwa kwa kutaka wenyewe.

Wakati maamuzi hayo yanatolewa timu hiyo tayari ilikuwa imejusanyia pointi tisa baada ya kushinda katika mechi zake zote tatu huku pointi tatu za mwisho walinyang’anywa baada ya wapinzani wao kuondolewa kwenye mashindano hayo kufatia kufanya vurugu na matokeo yake kufutwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.