Habari za Punde

RC Arusha aapa kumshughulikia Mkurugenzi wa jiji

Na Joseph Ngilisho, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Nd. Magesa Mulongo ameapa kumchukulia hatua kali Mkurugenzi wa jiji la Arusha,Sipora Liana na amempa siku sita amwombe radhi,yeye pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nd. John Mongela kupitia Kamati ya Fedha na Utawala kutokana na tabia yake ya umbea na maneno ya uchonganishi.
Aidha amewasihi Wakuu wa Idara na wafanyakazi wa jiji hilo kutimiza majukumu yao na kutokubali kudanganywa kwani kunyamaza kwake si kwamba hawezi kuchukua maamuzi.
Mulongo alitoa onyo hilo katika kikao cha kazi cha jiji la Arusha alichokiitisha kwa ajili ya kujadili mpango wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya elimu, ukusanyaji mapato na mifugo ambacho kiliwashirikisha Madiwani, Wakuu wa Idara,Wenyeviti wa tarafa,  na Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.
Alisema amemvumilia kwa muda mrefu Mkurugenzi huyo lakini sasa ameshindwa na ifikapo Disemba 28 kama atakuwa hajamuomba radhi, atamng’oa iwe fundisho kwa watendaji wengine wenye tabia kama hiyo.
Alisema si mara ya kwanza kwa Liana kumsingizia uongo kuwa yeye (Mulongo) ameamrisha wamachinga kurudi kwenye mitaa mbalimbal ya jiji la Arusha.
Alisema Mkurugenzi huyo aliwahi kuandika barua kwa Waziri Mkuu,MizengoPinda kudai yeye ameagiza Mkurugenzi wa kampuni ya  Skytel,Allbless Shoo,  aliyepewa zabuni ya kuweka matangazo maeneo yenye taa jijini humo na kukusanya ushuru kuwa, apewe zabuni bila kufuata taratibu kwa sababu amemuahidi ‘kitu fulani.’

Alisema waliitwa na Waziri Mkuu kuzungumzia suala hilo ikiwemo suala la kumtuhumu Meya wa jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kuwa aliandika ‘invoice’ ya shilingi milioni 20 ili aweze kuwahudumia wageni waliofika jijini humo kwa ajili ya chakula lakini Liana alipofuatilia aligundua ni shilingi milioni 5 .
Aidha alisema Mkurugenzi huyo alimtuhumu Mkuu wa Wilaya  kuwa amekuwa mpenda posho kwenye vikao vya kamati katika halmashauri hiyo huku akisema maafisa usalama,Mkuu wa Mkoa,Mkuu wa Wilaya na Meya ni wezi wakubwa wa fedha za umma.
“Hivi unawezaje kufanya kazi na watu ambao wana matatizo, tumezushiwa uongo ambao nimeona bora ninyamaze yapite lakini kumbe unaponyamaza yanakuja mengine tena,” alisema.
Aidha alisema Mkurugenzi huyo alitaka kuanzisha mahakama ya kuwafunga machinga wanaokaidia kuhama na tayari alishaanza mchakato wa kuomba mahakimu wa kuendesha kesi na askari wa kuwakamata bila kujalidiana na mkoa.
Ametoa siku 6 kuanza jana  akimtaka Mkurugenzi huyo kuitisha kikao cha kumwomba radi yeye,Mkuu wa Wilaya, Meya, Katibu Tawala na maafisa usalama aliowaita wezi na wala rushwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.