Habari za Punde

Spika Amelazimika kuahirisha Kikao kwa Dakika 15

Na Himid Choko.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho  leo  jioni amelazimika kuahirisha kikao cha baraza la wawakilishi kwa muda wa dakika  15 kutokana na wajumbe wengi kucherewa kufika katika kikao hicho.
Akizungumza baada ya kurejea tena katika kikao hicho Mhe Kificho amewataka wajumbe hao kuacha mara moja tabia mbaya ya utoro na ucherewaji katika vikao vya baraza .

Amesema chombo cha baraza la wawakilishi ni chombo kikubwa  katika nchi hivyo kinapaswa kuwa kioo, hivyo si nyema kwa wajumbe wa baraza hilo kucherewa au kutoroka katika vikao hivyo ambayo vinaonyeshwa  na kutangazwa moja kwa moja  kupitia vyombo vya habari.

Amesema amewaomba wawakilishi hao kutoendelea kujipa sura mbaya kwa wananchi  na badala yake watekeleze ipasavyo majukumu waliyokabidhiwa na wananchi  kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
Aidha spika kificho amewaomba radhi wananchi kutokana na kitendo kilichofanywa na wawakilishi wao .
Wakati huo huo katibu wa BLW  Yahya khamis Hamadi amesema  Baraza la Wawakilishi limelazimika kuitisha Kikao cha Dharura cha Kamati ya Uongozi  ya Baraza ili kujadili kitendo hicho cha leo.

Amesongeza kusema kwamba kitendo kilichoonyeshwa na  waheshimiwa wawakilishi hao hii leo si nidhamu wala si cha haki  hivyo Kamati ya uongozi ya baraza itakutana jumatau ijayo kuangalia uwezekano wa kubadilisha Kanuni  ili kudhibiti nidhamu ya Baraza.

Amesema cha kusikitisha zaidi hii leo wakati mhesimiwa Spika anaakhirisha kikao hicho kwa muda hata wanadhimu wa vyama  na serikali nao hawakuwemo wakati huo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.