Habari za Punde

Wananchi wa Jumuiya Zisizo za Kiserekali Kuazisha Miradi

Na Khamis Haji. OMKR
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amewahimiza wananchi na jumuiya zisizokuwa za Kiserikali kuendeleza juhudi za kuanzisha miradi ya nishati mbadala ambayo ni rahisi wananchi kuweza kumudu gharama zake za kuiendesha.
Waziri Ferej ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua mradi wa umeme wa Jua katika skuli ya Mto wa Pwani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema skuli nyingi pamoja na wana jamii hapa Zanzibar hulazimika kutumia fedha nyingi kulipia huduma ya umeme, gharama ambazo zinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa, iwapo watajikita zaidi katika kuanzisha miradi ya nishati mbadala, ikiwemo ya umeme wa Jua.
“Hivi sasa huduma ya umeme imeshapanda bei na isitoshe skuli zote zinalipa umeme kwa bei za biashara, wakati skuli zetu zipo kwa lengo la kutoa huduma na sio kwa lengo la biashara”, alisema Waziri Ferej.
Waziri Ferej alitoa pongezi kwa jamii ya Wazanzibari kwa kuonesha mwamko mkubwa wa kukuza elimu na kueleza kuwa kutokana na mwamko fuo pamoja na juhudi za serikali, hivi sasa kiwango cha uandikishaji wanafunzi kimefikia zaidi ya asilimia 124 kwa elimu ya msingi.
Nao walimu na wanafunzi wa skuli hiyo katika risala yao wamesema mradi huo utakuwa ni chachu ya maendeleo sio tu kwa walimu na wanafunzi, bali wana kijiji wote wa Mto wa Pwani.
Walisema wanawapongeza taasisi zote zilizosaidia kufanikisha mradi huo, kutokana na umuhimu wake katika wakati huu ambao teknolojia inapewa umuhimu wa kipekee ambapo pia shughuli nyingi haiwezi kufanyika bia, ya huduma ya umeme.
Mradi huo umeanzishwa na jumuiya ya Labayka kwa ushirikiano na taasisi ya Zanzibar Enteprise and Employability Training (ZEET) na umegharimu jumla ya shilingi milioni 3.4.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.