Na Salim Said Salim
UPO usemi maarufu wa kiswahili tokea dahari na enzi unaotumika sana Zanzibar usemao; “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”.
Usemi huu ulitokana na hali iliyokuwapo hapo zamani ya watu wengi wa Visiwani kuwaangalia kwa ubaya na kutowaamini mabaniani (watu wa jamii ya Hindu kutoka India). Hawa mabaniani walikuwa maarufu kwa kushona viatu, hasa vya kiume.
Lakini pamoja na kumuoa baniani kuwa ni mbaya, bado watu wengi walikuwa hawaridhiki ilipofika mwezi mtukufu wa Ramadhani kama hawajaenda kwa baniani ili kumshonea mtoto wake au hata mwenyewe viatu kwa ajili ya Sikukuu ya Idd el Fitr.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa baadhi ya baniani, licha kuonekana na jamii kuwa ni watu wabaya, walikuwa wakiwashonea watu viatu kwa mkopo, tena bila ya kuwatoza riba.
Baniani mmoja aliyekuwa akiitwa Surti katika Mji Mkongwe alikuwa na msemo maarufu alipokuwa akitoa mkopo kwa kusema; “Vaa buti leo, lipa pesa kesho”.
Hali hii ndio iliyozaa msemo huu wa “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”. Ndiyo hali inayojitokeza waziwazi Zanzibar katika siasa zilizopitwa na wakati za wahafidhina na baadhi ya wastaafu wa vikosi vya ulinzi na usalama ambao wanaona fahari kupalilia mbegu za siasa za chuki, uhasama, ubaguzi na ufashisti.
Ukiutafakari mwenendo wa hawa wahafidhina na wastaafu ambao wanaonekana kuogopwa na serikali na ndiyo maana hawawajibishwi kisheria kwa kauli zao za uchochezi na ubaguzi, utaona waliowashikia bango zaidi ni watu wa Kisiwa cha Pemba.
Ukiangalia kwa undani utaona hapana lolote lile lililosababisha kujengeka kwa hizo chuki, isipokuwa wivu na uhasidi unaotokana na Wapemba kupata mafanikio makubwa ya kimaisha. Hii inatokana na ukweli kwamba Wapemba ni watu wa kujituma zaidi kuliko wenzao wa Kisiwa cha Unguja kadiri ya muono wangu.
Wakati kijana mwenye asili ya Kisiwa cha Pemba anaweza kufanya kazi ya sulubu kabla ya jua kuchomoza hadi linapozama huku akipumzika kwa muda mchache, na kuendelea tena na kazi nyingine kwa saa mbili ama tatu wakati wa usiku, vijana wengi wa Unguja huona wamefanya kazi sana kama wakitumia saa tatu au nne!
Hali hii inatokana na umwinyi, kupenda makubwa na maisha ya fahari, kunakoonekana zaidi miongoni mwa vijana wa Kisiwa cha Unguja kuliko wenzao wa Kisiwa cha Pemba.
Lakini wakati wahafidhina na wastaafu wakiimba nyimbo zao chafu za kuwataka Wapemba waliopo Unguja warudi kwao (ati Unguja na Pemba hazina historia ya watu wake kuwa wamoja), siwasikii kusema na hizi karafuu ambazo kila baaada ya siku chache huletwa kwa wingi kutoka Pemba kuja Unguja zibakie huko huko Pemba.
Kwa maana hiyo, hawa wanafiki wa kisiasa hawawataki Wapemba kwa sababu ya msimamo wao wa kisiasa wa kuwa wapinzani, lakini wanazipenda karafuu zinazotoka Pemba.
Taarifa ya serikali ya hivi karibuni imeeleza kuwa Shirika la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZSTC) hadi wiki iliyopita limeshanunua tani 1,500 za karafuu kisiwani Pemba kwa msimu huu, na zoezi hilo linaendelea kwa kasi nzuri.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Biashara wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kazi ya uchumaji wa karafuu inaendelea vizuri Pemba na lengo ni kwa ZSTC kununua zaidi ya tani 4,500 msimu huu.
Wakati Pemba imeshachuma na kuuza serikalini zaidi ya tani 1,500, Kisiwa cha Unguja ndiyo kwanza kinajikongoja kukaribia kuuza tani 300 na kikifikia tani 1,000 mwishoni mwa msimu itakuwa maajabu.
Kwa kawaida Pemba huzalisha zaidi ya robo tatu ya zao lote la karafuu la Zanzibar ambalo kwa miaka mingi limechangia zaidi ya asilimia 90 ya pato lake la fedha za kigeni. Mchango huo sasa umeshuka na kuwa kati ya asilimia 35 hadi 40.
Fedha za karafuu nje ya nchi ndizo zinaipa serikali kwa kiasi kikubwa ubavu wa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo Unguja na Pemba. Vile vile, fedha hizi ndizo zinazowalipa mishahara hao wastaafu na wahafidhina, pamoja na kiinua mgongo na posho wanayoipata kila mwezi.
Kinachonishangaza na ninawauliza wahafidhina na wastaafu, wakiwemo wale wanaosalisha Ijumaa waumini wa dini ya Kiislamu, mbona siwasikii kuitaka serikali iziache hizi karafuu Pemba badala ya kuzileta Unguja? Ama hawakukosea waswahili waliposema “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”?
Kwa hakika watu wa Pemba wanapaswa kupongezwa kwa kuonyesha uzalendo wa kuitikia wito wa serikali wa kuuza karafuu zao kwa ZSTC na kuacha kuzisafirisha nje kwa magendo ambayo yangeweza kuwapatia bei kubwa zaidi.
ZSTC imebahatika kununua tani 1,500 za karafuu kwa msimu mzima kutoka Pemba. Hii ilitokana na karafuu nyingi, zaidi ya nusu, kusafirishwa kwa magendo nje ya Zanzibar.
Lakini serikali nayo inafaa kupongezwa kwa kusikiliza kilio cha Wapemba cha kuomba unyonyaji waliokuwa wakitendewa kama haukuweza kuondoshwa basi angalu upunguzwe ili na wao wapumue.
Kwa muda mrefu Mpemba alipata sio zaidi ya asilimia 50 (upo wakati alilipwa asilimia 2.25) ya bei ya soko la dunia. Hivi sasa mkulima wa karafuu analipwa kati ya asilimia 78 na 82 ya bei ya soko la dunia ambayo hupanda na kushuka baada ya kila kipindi kifupi.
Kwa vyovyote vile, hatua ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Ali Mohamed Shein, inafaa kupongezwa kwa kuonyesha kuwajali wakulima wa Pemba kwa kuongeza bei ya kuuza karafuu. Hali hii imewafurahisha Wapemba ambao kwa miaka mingi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar, lakini hawatendewi haki kwa malipo ya karafuu.
Ni matarajio yangu uzalendo ulioonyeshwa na Wapemba kwa nchi yao unafaa uwe somo kwa wahafidhina ambao wamejenga chuki zisizokuwa na msingi, isipokuwa husuda tu kwa Wapemba.
Ni vyema wahafidhina sio tu wakaachana na kumkataa baniani na kupenda kiatu chake, lakini wakabadilika na kuanza kampeni ya kuwataka watu wa Unguja nao wachangie pakubwa zaidi uchumi wa nchi yao kama wanavyofanya ndugu zao wa Pemba.
Umoja na sio fitna za kibaguzi ndio utakaojenga Zanzibar na hili wajue sio wahafidhina tu, bali hata wale wenye ndoto ya kuwagawa hata watu wa Kisiwa cha Unguja kwa makabila au maeneo wanayotoka ya mjini na mashamba, kaskazini na kusini.
Wakati Wazanzibari wakisherehekea miaka 50 ya mapinduzi na kumalizika sherehe hizi zilizogharimu mabilioni ya shilingi na kuanza safari mpya ya kujitafutia maendeleo, ni vizuri kwa watu wote Visiwani, Unguja na Pemba, kuachana na siasa za chuki, uhasama na ubaguzi.
Ni umoja tu na maelewano, licha ya tofauti zao za kisiasa ndio utakaoweza kuwapatia maendeleo wao na vizazi vijavyo.
Chanzo : Tanzania Daima
Ndugu muandishi maneno uliyoandika yana ukweli ndani yake lakini ulichosahau kuwafatilia hao wahafidhina ujue background zao, muunguja asili hawezi kumbagua mpemba kwa maangliano yalokuwepo miongoni mwao toka zama za mababu.
ReplyDelete
ReplyDeleteMuandishi huyu ni mkongwe lakini inaonesha anazeeka vibaya ao anao waita wapemba wengi wao iyo mikarafuu wameipata 1967 serekali ya mapinduzi ilipogawa eka tatu tatu, wengi walikuwa mabawabu
mimi ni mpemba lakini ardhi pemba haikuathirika yaani kuchukuliwa kama utatembea ni sehemu ndogo tu ya ardhi iltaifishwa na eka tatu tatu wengi waliacha au kuzirejesha kwa kumuogopa muumba na RAIS MWINYI aliwataka wenye mali zao warejeshewe na eka zimebakia kwenye mikono ya askari na maafisa kutuka UNGUJA kwa ajili ya kulima kwa kipindi wanapokuwepo PEMBA kikazi
DeleteAliona macho haambiwi tizama sasa kazi kwako miandishi wa kwanza
Deletehapo mtakubaliiana na maoni ya watu kuwa kama muungano wa tanzania utakufa basi Muungano kati ya unguja na pemba haufiki mbali.wengi wao wapemba wamekuwa wanaupinga muungano wa Tanzania kwakuona wa Unguja wamekuwa wakiwatumia wa Tanzania Bara kuwatawala Wapemba.mambo yalibadilika tu pale CCM ilipompitisha Mpemba kwa pinde awe mgombea Urais Zanzibar.na kuwazima viongozi wakuu wastaafu wa Unguja na waziri kiongozi wakati huo walipojaribu kuzuia Mpemba asiwe rais Zanzibar.kwasasa wapemba wamepunguza upinzani kwenye muungano.kuhusu uchapakaza na kuzitafuta pesa hapo hakuna ubishi.muunguja na mzaramo wote wanafanana kwa hilo la baniani mbaya ila kiatu chake dawa.hayo yapo pia DSM kati ya mzawa na mubara.mubara DSM hatakiwi ila mchele/sukari/viazi/mahindi/vyakula vyake kwa jumla ni vizuri.
ReplyDeleteHaya tutaona mwisho wake
ReplyDeletehayo mabo huyajui nenda Pemba ukaulize asilimia kubwa ya watu wamerejesha eka ikiwemo familia yangu na kijiji ambacho ninatoka tangia miaka ya 80 kutokana na nafsi zetu zilivyo kuogopa mungu zaidi
ReplyDeleteKama wapemba walikua ni mabawabu ni lini ulisikia waarabu kulalamikia kupokonywa mashamba kama vile wanavyolalamika kupokonywa majumba unguja. Waarabu wenye asili Pemba wanamiliki mashamba yao hadi kesho. Mimi kwetu nimeshuhudia Baba alikata pori na kupanda mikarafuu isiyopungua Mia tano. Wacha ujinga.
ReplyDeleteHao wanao chukia Wapemba sio Waunguja nilazima twende deep na asili, Muunguja katu hamchukii mpeba bali ni mapandikizi ya machipukizi ya Watwana wa kibara walokimbia viboko vya mjerumani enzi hiio.
ReplyDeleteSasa wamekuja zanzibar na kuzaa na Wazanzibar kwahio ndio hujifanya wao ni Wazanzibar na wafrica ukenda deep hawajifishi asili zao.
Jamani sikilizeni! Tusiwe na jazba kubwa, hawa jamaa watajaribu kutugawa lakini hatugawiki! Hii ni shaani M/Mungu, mfano kama mimi vipi nitamtenga muunguja au mpemba na kumbagua? Baba ni muunguja na mama ni mpemba, kaka zangu wengine wameoa unguja na wengine wameoa pemba, na dada vile2 wameolewa huku na huku, huo ni mfano wangu mimi, na hivyo ndivyo ilivyo kwa wazanzibari wengi! Bwana muandishi huwezi kutubaguwa kwasababu ya maneno ya kipuuzi walioyasema na wanayosema wanaojiita muhafidhiina na wastaafu, mpemba asili hawezi kumbagua muunguja, na muunguja asili hawezi kumbagua mpemba, hata hizo karafuu ulizozitaja haziwezi kutubagua, huu ndio ukweli, sisi ni ndugu toka enzi za (bemba moshi na uungu umejaa) enzi za mababu.
ReplyDeletemsiwe na wasiwasi hakuna muunguja kumbagua mpemba au mpemba kumbagua muunguja , hizo ni propaganda za watanganyika wenye kuogopa muungano kuvunjika ndio hukamatia hapo kama kisingizio cha kuendeleza ukoloni mamboleo kwa visiwa vya znz. Tuvunje muungano kwanza halafu muone jinsi visiwa hivi vitavyokamatana na kupata maendeleo kwa muda mfupi.
ReplyDeleteMwandishi acha uchonganishi!! Mambo hayo ilikua wakati wa komandoo sio sasa
ReplyDelete