Na Haji Nassor, PEMBA
WATU nane wakiwemo mabaharia wanne, wamenusurika kifo baada ya jahazi
walilokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Wete Pemba, kukumbwa na upepo mkali
na kulazimika kumwaga mzigo waliokua wamepakia.
Kadhia hiyo iliwakumba jana majira ya saa 8:50 jioni, wakati jahazi
hiyo ikiwa imebeba bidhaa za aina mbali mbali za wafanyabiashara wa miji ya
Pemba.
Baadhi ya mabaharia waliokuwemo kwenye chombo hicho, walisema
waliondoka bandari ya Tanga wakiwa salama na kwamba mzigo waliobeba ulikuwa wa
kawaida, lakini hali ilibadilika kadiri safari ilivyoendelea.
Walisema walibeba matenga ya tungule 300, viazi mbatata gunia 30,
vituguu maji gunia 40, magodoro 30 pamoja na vitu vyengine vidogo vidogo kama
mafuta ya kupikia, madumu, misumari na mapipa matupu.
Mmoja kati ya mabaharia hao aliejitambulisha kwa jina moja la Mohamed
(Mudi) alisema, wakati wako nusu ya safari yao, ulitokezea upepo usio wa
kawaida na kuliyumbisha jahazi lao.
Alisema baada ya kuona jahazi linayumba mara tatu mfululizo, nahodha
alitoa agizo kali la kuwataka mabaharia wamwage mzigo kupunguza uzito.
Nae abiria aliekuwemo kwenye chombo hicho, Nd. Ali Khamis Juma,
akizungumza kwa njia ya simu alisema, zaidi ya matenga 25 ya tungule, madumu ya
mafuta, baadhi ya viroba vya misumari vilitupwa baharini.
“Taharuki haikuwa ndogo, lakini kutokana na tuliokuwemo kwenye jahazi
ni watu wa bahari, tulijua nini tufanye, na tukaanza kumwaga mzigo taratibu
hadi utulivu ulipopatikana,’’ alisema.
Baadhi ya mashuda wengine waliokuwemo kwenye jahazi hilo walidai kuwa,
mzigo ulikuwa umezidi uwezo wa jahazi hilo na ndio maana, baada ya kubakia
mzigo wake wa kawaida safari iliendelea.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba,Sheikhan Mohamed Sheikhan,
alisema taarifa za tukio hilo bado hazijafika ofisini kwake.
Hivi karibuni watu watano walihofiwa kufa, baada ya boti ya Mv.
Kilimanjaro II waliokuwa wakisafiria, kukumbwa na dhoruba ilioambatana na upepo
mkali, katika eneo la mkondo wa bahari ya Nungwi, wakati ilipokuwa ikitokea
bandari ya Mkoani kwenda Unguja.
Mamlaka ya hali ya hewa
Tanzania (TMA) na Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar ZMA, katika kipindi cha
miezi miwili mfululizo sasa, imekua kikitoa taarifa za tahadhari kila siku
kupitia vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa upepo mkali katika bahari ya Hindi.
Ama watu wengine Wana Bezo kweli kweli.. Hivo matangazo yote yaliotolewa kuhusu kuchafuka kwa hali ya Hewa katika siku hizi 3.. Hawa jamaa haweajayaona hayooo?... Au Wamekula pesa za watu halafu wakajitia kwamba wameitupa mizigo bahaarini... KLwanini wasingoje Upepo na dharuba kutulia ndipo wakasafiri..
ReplyDeleteMimi nasema Wapemba wana Bezo kweli kweli... (Sorry Muuum) ..Lakini jamaaa zangu wa Kipemba saanyengine Mauti Huyatafuta wenyewe...
Kusudi haiyanmbiwi Pole...