Khamisuu Abdallah na Salum Simba, MUM
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi
Zanzibar, Nd. Vuai Ali Vuai, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya
Jamuuhuri ya Muungano wa Tanzania zinategemeana katika kulinda na kudumisha
muungano.
Alisema
Zanzibar na Tanzania Bara zimekuwa zikitegemeana katika masuala mbalimbali
yakiwemo biashara, ulinzi,elimu na mambo mbalimbali ya kijamii hivyo si vyema
kwa baadhi ya watu kusema muungano huo upo kwa ajili ya sehemu moja tu.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) baada ya kupokea maandamano ya vijana
yaliyoanzia Amani hadi Mwembekisonge.
Alisema Muungano wa Tanzania ni kupigiwa mfano
kwani umeleta maelewano na kukuza udugu uliopo.
Akizungumzia rasimu ya pili ya katiba,alisema
chama cha Mapinduzi bado kinaamini kuwepo serikali mbili kwani ndizo
zinazowasaidia Watanzania.
Hata hivyo, alimpongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufanikisha
sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo kujenga mnara wa
kumbukumbu katika maeneo ya Muembekisonge.
"Nampongeza sana Rais Shein kuibua wazo la
kujenga mnara wa kumbukumbu hapa Kisonge pamoja na kutoa kitabu rasmi
kinachoelezea historia ya Zanzibar japo kuwa kuna watu wanaosema mnara huu
unaitia hasara serikali,” alisema.
Hivyo aliwasihi wananchi hasa vijana kutoona
tabu kuendelea kudumisha muungano na
kuyalinda Mapinduzi kwani ndio yaliyowafikisha katika hatua mbalimbali za
maendeleo .
Sambamba na hayo aliwataka vijana kujitokeza kwa
wingi kwenda kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze
kupata haki yao ya msingi.
Nae Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Nd. Sadifa Juma
Khamis, alisema wameamua kufanya matembezi hayo kwa ajili ya kumpongeza
Rais kwa hutuba yake aliyoitoa katika sherehe za kuadhimisha miaka
50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment