Habari za Punde

Wizara ya afya yapokea msaada wa madawa kutoka Serikali ya Ras Al Khaimah

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiongozana na Mfamasia Mkuu wa Serikali Bwana Habib Ali Sahrifu akiitembelea Bohari Kuu ya Dawa iliyopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji akipokea msaada wa dawa mbali mbali kwa ajili ya hospitali za Zanzibar kutoka kwa Makamuwa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi zilizotolewa msaada ya Serikali ya Ras Al – Khaimah kupitia Jumuiya  ya misaada inayoendesha kiwanda cha Dawa ya Gulf.

Balozi Seif na Waziri wa Afya Mh. Juma Duni wakibadilishana mawazo mara baada ya hafla ya kukabidhi dawa mbali mbali  zilizopo pembeni yao kwenye Jengo la Bohari Kuu liliopo Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Na Othman KHamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameikabidhi Wizara ya Afya Zanzibar dawa mbali mbali za matumizi ya Wanaadamu zilizotolewa msaada na Serikali ya Ras  Al – Khaimah kupitia Jumuiya inayoendesha kiwanda cha Dawa ya Gulf { Gulf Pharmacetical Industries }.

Makabidhiano ya msaada huo wa dawa mbali mbali yamefanyika kwenye Jengo la Bohari Kuu ya Dawa la Wizara ya Afya Zanzibar liliopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Akimkabidhi dawa hizo Waziri wa Afya  Mh. Juma Duni Haji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  alisema msaada huo ni awamu ya pili kuwahi kutolewa na Serikali ya Ras Al – Khaimah kwa ajili ya Wananchi wa Zanzibar.


Alisema awamu ya kwanza ya misaada iliyopokelewa na Zanzibar ilihusisha vyakula, nguo pamoja na baadhi ya vifaa kama  baskeli za watu wenye ulemavu   ambavyo vingi kati yao vilipelekwa nyumba za kulelea watoto yatima Mazizini, nyumba za wazee  sebleni na welezo kwa unguja na Dimbani Kisiwani Pemba.

Alifahamisha kwamba awamu hiyo pia ilifaidisha watoto pamoja na wazee wanaoishi katika mazingira magumu hasa katika vijiji vya Mgonjoni Wilaya ya Kaskazini B na Kiuyu Mbuyuni Micheweni Pemba.

Akipokea msaada huo Waziri wa Afya  Mh. Juma Duni Haji aliipongeza Serikali ya Ras Al – Khaimah kupitia Taasisi zake zinazojitolea kutoa misaada mbali kwa ajili ya kusaidia ustawi wa Wanaadamu sehemu mbali mbali Duniani ikilenga zaidi Zanzibar .

Waziri Juma Duni alisema msaada huo wa Dawa zinazotibu maradhi ya Gesi, vidonda vya tumbo pamoja na maradhi ya kisukari zitaongeza nguvu ya akiba ya dawa zilizopo kwenye Bohari hiyo ya Wizara ya Afya  kwa ajili ya kuhudumia Wananchi.

Akizungumzia suala la ujenzi wa Vituo vya Afya katika Maeneo mbali mbali hapa Nchini Mh. Juma Duni alimfahamisha Balozi Seif kwamba mkakati wa Wizara ya Afya uliopo hivi sasa umelenga  kuwaomba wafadhili pamoja na wananchi kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa nyumba za Madaktari ambazo zimekuwa na upungufu mkubwa badala ya Vituo vya Afya.

Alisema Zanzibar tayari imefanikiwa kuvuka lengo la azimio la Shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } la kuwa na Kituo cha huduma za afya kila baada ya kilomita tano.

“ Hivi sasa tayari tumeshakuwa na vituo vya kutosha vya Afya katika maeneo yetu mbali mbali Mjini na Vijijini ambavyo baadhi ya maeneo mengine havifiki hata kilomita tatu baina ya kituo kimoja na chengine  hali ambayo inatudhihirisha kwamba tumevuka lengo la Shirika la Afya Duniani la kuwa na Kituo cha Afya kila baada ya Kilomita Tano “. Alifafanua Waziri wa Afya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata wasaa pia wa kulikaguwa  Bohari Kuu la Dawa  na kujionea hali halisi ya kiwango cha kuridhisha cha Dawa  zilizomo kwenye Bohari hiyo.

Mfamasia Mkuu wa Serikali Bwana Habib Ali Sharifu alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara ya Afya inaendelea kujiandaa na mpango maalum wa matumizi na ugawaji wa Dawa katika vituo mbali mbali vya Afya Nchini kwa kutumia mfumo mpya wa Mtandao wa Mawasiliano ya Kompyuta.

Bwana Habib alisema mpango huo hivi sasa uko katika majaribio katika  Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambapo ukikamilika mfumo huo utakuwa na uwezo wa kujua upungufu au kiwango cha Dawa kinavyoendelea kutumika katika kila kituo.

Msaada huo wa Dawa zinazotibu maradhi mbali mbali kutoka Nchini Ras Al – Khaimah Kupitia jumuiya inayoendesha Kampuni ya Dawa ya Gulf zimegharimu  jumla ya Shilingi za Kitanzania Milioni  171,212.000/-.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.