Habari za Punde

DK SHEIN AIPONGEZA WIZARA YA BIASHARA KWA KUIFANYA MABADILIKO YA KUJIIMARISHA KIUTENDAJI

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                                16 April , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema mafanikio ya mabadiliko makubwa katika wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko katika miaka mitatu iliyopita yanadhihirisha sio tu uwezo walionao watumishi wa Serikali bali dhamira waliyonayo katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.
“Katika miaka mitatu iliyopita tumeshudhudia mabadiliko makubwa katika Wizara hii na Taasisi zake na hii inadhihirisha uwezo tulionao kama tukidhamiria kujituma katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku” Dk. Shein amesema.
Mhe Rais ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akifunga mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 katika kikao kilichofanyika Ikulu.
Amebainisha kuwa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imefanya jitihada kubwa na hatimae kuweka mwelekeo wake katika njia sahihi kufikia malengo ya kukuza biashara, masoko na viwanda kwa manufaa ya taifa.
“Nimeridhishwa na mikakati ya wizara pamoja na taasisi zake zikiwemo Shirika la Biashara la taifa- ZSTC na Shirika la Viwango Zanzibar-ZBS pamoja na upya wake” Dk Shein alisema.
Alifafanua kuwa jitihada za kutafuta masoko ya bidhaa za Zanzibar ikiwemo karafuu zinazofanywa na ZSTC hazina budi kupongezwa kwa sababu zimeliweka shirika hilo katika mwelekeo mzuri wa kibiashara unaosaidia taifa.
Dk. Shein pamoja na kupongeza mafanikio makubwa katika kuimarisha wajasiriamali nchini lakini alihimiza jitihada zaidi katika kuwapa wajasiriamali hao taarifa zaidi juu ya fursa zilizopo.

Aliongeza kuwa hiyo ni pamoja na kuwasaidia wale ambao wamebahatika kupata fursa za kuunganishwa na masoko wazidi kuwezeshwa ili waweze kukidhi viwango vya ubora vya masoko hayo ili kufikia matarajio ya masoko hayo.
Aidha katika mkutano huo, Mhe Rais ameiagiza Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara nyingine husika kuhakikisha kuwa suala la kushughulikia uingizaji wa bidhaa zilizotumika hasa za eletroniki linafanyiwa kazi haraka bila ya kuchelewa.
“suala hilo tumekuwa tukilizungumza kwa muda mrefu na mwelekeo wa biashara ya bidhaa za aina hiyo hivi sasa unaonesha kuwa Zanzibar imekuwa kama jaa kwa kuwa baadhi ya bidhaa hizo zikishafika nchini kuishia kutupwa bila kuuzwa au kutumika” alieleza Dk. Shein.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ametahadharisha kuhusu tabia inayojengeka hivi sasa katika Wizara na Taasisi za serikali kutumia huduma za washauri binafsi hata kwa mambo ambayo wao wenywe ni wataalamu na wanaweza kuyafanya.
Amesema watendaji waliopewa dhamana wakiwemo wakurungezi wamepewa kutokana na sifa zao na uzoefu walionao hivyo hakuna ulazima kila wakati kutumia fedha nyingi kugharimia huduma za ushauri wakati wao wenyewe wana ujuzi huo pengine kuliko hata hao wanaowapa kazi hizo.
“Wakurugenzi ni wataalamu hivyo ni lazima waoneshe utaalamu wao katika maeneo wanayoyafanyia kazi na ni jambo muhimu kujiuliza kwanza kama kweli tunahitaji washauri katika kila kazi”alisisitiza Katibu Mkuu Kiongozi.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia pamoja na kupongeza jitihada za wizara za kuimarisha ujasiriamali alishauri pia mafanikio katika sekta hiyo yatangazwe zaidi ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na shughuli za ujasiriamali.
“Tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha ujasiriamali nchini. Tukiangalia tulikotoka hadi sasa tunaona wajasiriamali wetu hasa kinamama wako katika hatua nyingine kabisa kwa kulinganisha bidhaa walizokuwa wakizalisha huko nyuma na hizi za sasa” Balozi Ramia alisema.
Awali akitoa taarifa ya Wizara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Julian Raphael alieleza kuwa kwa mwaka 2013/2014 Wizara hiyo ilipanga kutekeleza malengo 16 ambayo hadi sasa yametekelezwa kwa viwango tofauti.
Miongoni mwa malengo hayo ni kukusanya mapato ya shilingi milioni 90, kukuza ushindani wa kibiashara, kufanya utafiti wa bidhaa, kufanya mapitio ya sera na sheria, kukuza biashara na masoko, kukuza maendeleo ya viwanda na ujasiriamali, kusimamia viwango na ubora wa bidhaa.
Malengo mengine ni kutekeleza mkakati wa maendeleo ya karafuu, mageuzi ya shirika, kununua karafuu wastani tani 4000-4200, kuimarisha rasilimali watu, kukuza ushiriki wa Zanzibar katika majadilinao ya kikanda na kimataifa pamoja na majadiliano baina ya sekta binafsi na Serikali.         
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.