Habari za Punde

TBC iache mchezo huu mchafu

Na Salim Said Salim
 
KWA miaka mingi iliyopita palisikika kilio cha kutaka vyombo vya habari vya serikali vibadilike na kuacha kuwa vya propaganda za serikali, chama tawala au taasisi yoyote nyingine.
 
Watu wengi waliipongeza hatua ya serikali ya kuifanya Radio Tanzania na kituo cha serikali cha televisheni kuwa shirika na kuwa vya umma.
 
Hapo mwanzoni vituo vya redio na televisheni vya TBC, vilitoa mwanga wa kuwa kweli vya umma.
Lakini pole pole tokea TBC kupata uongozi mpya tunaona ukereketwa wa CCM na kujikita zaidi katika siasa kuliko kuheshimu maadili ya taaluma ya habari, ikiwa pamoja na ya watu kupata habari za kila upande.
 
Hii sasa Watanzania wengi unawasikia wakisema masikini TBC imepotea njia na hakuna wa kuiongoza njia sahihi.
 
TBC ya leo imejitokeza wazi kuonyesha ukereketwa wa CCM na kuegemea kupita kiasi upande wa serikali na kujisahau kuwa ni mali ya walipa kodi wote wa Tanzania.
 
Kwa kweli na hii sio siri TBC ya jana sio ya leo, na kama inataka kuendelea hivyo ni vizuri ikabadili jina na kujiita CCM Radio au CCM TV badala ya kutumia jina la Tanzania. Lakini ikifanya hivyo isitumie pesa za walipa kodi.

Mara nyingi nimesikia kwa uthibitisho juu ya namna ambavyo uongozi wa TBC ulivyowahi kulalamikia baadhi ya vipindi vilivyopita ambapo zilisikika sauti za kuikosoa serikali, kama vile ni haramu kufanya hivyo.
 
Hapo mwanzo nilitaka kuamini ule ulikuwa ni utashi wa baadhi ya viongozi wa shirika hili, lakini matokeo ya hivi karibuni yameonyesha kuwa hii ndiyo sera mpya ya TBC.
 
Watanzania wengi walisikitishwa kuona matangazo ya Bunge la Katiba yaliyokuwa yakiendelea Dodoma yamekatishwa ghafla kwa vile palisikika kauli za kuilaumu serikali na CCM juu ya muundo wa Muungano.
 
Maelezo tuliyopewa ni kuwa ati matangazo yalikatika kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo yamekuwa yakitokea kila pale wapinzani walipokuwa wanajieleza na kuikosoa serikali na CCM.
 
Lakini matatizo haya huwa hayatokei pale viongozi wa serekali na wa CCM wanapowakandia wapinzani. Haya ni maajabu makubwa.
 
Kwa wale waliokuwa hawataki kuamini kwamba TBC ya jana sio ya leo, ilibidi wasubiri na kupata ushahidi zaidi, yaani ule unaoitwa ushahidi usiokuwa na shaka (evidence beyond reasonable doubt).
Ushahidi huu ulipatikana karibuni pale TBC ilipokuwa inarusha moja kwa moja matangazo ya kongamano la kuadhimisha miaka 50 ya Muungano lililofanyika Zanzibar.
 
Matangazo ya TBC yalisikika vizuri kwa muda wote ule hadi pale aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, aliposema ni Serikali ya Zanzibar ndiyo iliyoanza kutaka serikali tatu mwaka 1984 na kuwashangaa wanaolibeza jina la Tanganyika kutumika.
 
Prof. Kabudi aliweka wazi kuwa wakati ule madai ya serikali tatu yaliyotolewa na Zanzibar yalisimamiwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.
 
Katika maelezo yake, Prof. Kabudi alieleza kuwa hoja ya kutaka serikali tatu ilipelekwa pia kwenye Baraza la Wawakilishi ambapo Brigedia mstaafu Ramadhan Haji Faki (aliyekuwa Waziri Kiongozi), aliongea kwa sauti nzito na kusema “Zanzibar siyo koloni la Tanganyika”. Hapo tena matangazo yakakatika ghafla.
 
Jamani hivi TBC wanataka kutueleza kuwa kila panapozungumziwa hoja ya kwanini pawepo serikali tatu ndiyo mitambo yao huharibika na kukatika matangazo?
 
Hivyo, TBC wanamdanganya nani? Ukweli ni kwamba wanajidanganya wenyewe, kwani Watanzania sio mbumbumbu na wanaelewa kuwa haiwezekani kila panapotokea hoja za kuikosoa serikali na CCM ndiyo mitambo iwe inaharibika.
 
Kwa kweli kwa mwenendo huu TBC haiwatendei haki walipa kodi wa Tanzania na baya zaidi inakwenda kinyume na maadli ya taluma ya habari. Kinachofanywa na TBC ni uhuni na dhambi.
 
Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuheshimu maadili ya taaluma na hata kuwa na ujabari wa kuvifungia vinavyodaiwa kuwa vimekiuka maadili.
 
Lakini kama kipo chombo ambacho kinaonekana kuwa ni kinara wa kuvunja maadili na kinafaa kufungiwa (kwa mtazamo wa serikali) basi TBC ni nambari wani.
 
Lakini viongozi wa TBC pia waelewe sio wanajitia aibu wao tu bali wanawafedhehesha wanataaluma wote wa habari kwa mwenendo huu wa ukereketwa wa kupendelea CCM uliokithiri.
 
Umma unataka kujua kila upande una hoja gani juu ya huu mchakato wa kutafuta katiba mpya, na zaidi juu ya mtafaruku uliopo sasa wa kuwa na mfumo gani wa Muungano. Kama hawawezi kuvumilia fikra za watu wengine, waache taaluma ya habari na wakauze nyanya.
 
Kuwapa watu habari za upande mmoja ni mbaya na hatari na kwa kweli ni kinyume na mwenendo wa kidemokrasia na hakusaidii nchi kusonga mbele.
 
Umma unafaidika unaposikia sauti za kila pembe, na pale raia anapopewa nafasi ya kusikia maoni tofauti ndiyo huchambua na kufanya uamuzi sahihi.
 
TBC lazima ielewe hizi sio zama za kuficha mambo. Umma wa Tanzania haudanganyiki, na kama wao wanafikiri wanaweza kuwanyima Watanzania haki ya kusikia fikra tofauti, waelewe vipo
vyombo vingine vitatoa yale wanayoyaficha na wao kubaki kufedheheka kama inavyotokea hivi sasa.
 
Viongozi wa TBC wanapaswa kuachana na mchezo huu mchafu, na kama wanafikiri mwenendo huu utasaidia kuwadumaza Watanzania kifikra, basi wamechelewa, tena sana.
 
Kwa taarifa ya viongozi wa sasa wa TBC, ambao upeo wao wa taaluma ya habari unatia shaka, vituo vyao vya redio na televisheni vimeanza kwa kasi kubwa kupoteza imani ya watu wengi wa Visiwani.
Siku hizi vyombo hivi havionekani tena kuwa ni vya umma kama ilivyokuwa mwanzo, bali vinahukumiwa kuwa ni vya kitengo cha chama tawala cha CCM na kwamba haviwatumikii Watanzania ambao wanavuja jasho kuvichangia kwa kulipa kodi.
 
Kwa mwenendo huu wa sasa wa kuminya habari, viongozi wa TBC wanaitia aibu serikali na kuichonganisha na wananchi.
 
Njia nzuri ya kujipendekeza kwa serikali na umma ni kutenda haki na sio kuvigeuza vituo vya redio na televisheni vya TBC kuwa vituo vya propaganda za kisiasa.
 
Umma wa leo wa Watanzania haudanganyiki. Unajua zuri na baya, na unapowanyima habari kupitia kituo kimoja cha redio, utatafuta ukweli kupitia kituo kingine na hivyo hivyo kwa televisheni na gazeti.
 
Hawakukosea Wazanzibari wanaolilia uongozi uliopita wa TBC ambao ulikuwa una sura ya kweli ya Kitanzania na sio ya CCM, CUF wala CHADEMA au NCCR-Mageuzi.
 
Kama vongozi wa TBC sasa wanataka kujigeuza wanasiasa, ni vyema wakaachana na taaluma ya habari na kuingia katika siasa kama baadhi ya wafanyakazi wenzao waliogombea ubunge na wengine kuwa mawaziri.
 
Siku hizi miongoni mwa kipimo cha kukomaa demokrasia katika nchi ni namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi, na unapokuwa na vyombo vya habari vya umma vinashabikia chama kimoja cha kisiasa au kuegemea serikalini tu na wengine kutopewa haki ya kusikika, basi hapo huwa hapana demokrasia.
 
Ninawaomba viongozi wa TBC wasiifikishe nchi yetu huko. Rais Jakaya Kikwete amekuwa mvumilivu wa fikra tofauti, na wao wanafaa kuiga mfano wake.
 
Chombo cha habari hakistahiki kuongozwa kwa utashi wowote ule, hadaa au nongwa. Ni vizuri TBC ikaachana na mwendo huu mara moja kwani vyombo hivi si mali ya familia za viongozi waliopewa dhamana ya kuviendesha, bali ni ya Watanzania wote
 
Chanzo - Tanzania Daima

2 comments:

  1. Ustaadh Salim kuna kitu unakisahau. Bora nikukumbushie. Zanzibar ni nchi ya kimapinduzi,na panasemwa "mapinduzi daima" .Yanini kuumisha kichwa chako.Pigania kama utaweza kuufuta msemo huo kwanza.

    ReplyDelete
  2. usijali ndugu salim , sisi tunajua kuwa TBC na vyombo vingi vya habari ni vya serikali tawala na chama chake, njia ya mwongo ni fupi , wenye akili wameona haya na bado mengine yatafuata , lakini msimamo wetu ule ule aluta continua mpaka tupate uhuru znz , na wakilazimisha wahakikishe kuwa yanayotokea siria , krimea na kwengineko hayako mbali kufika na hapa, kama damu kumwagika ndicho wanachotaka itamwagika kwa wote sio upande mmoja , watumie hekima watuachie nchi yetu kwa amani tuendelee ushirikiano wa kijirani

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.