Habari za Punde

Tindwa awaasa wananchi kuwa wamoja

Shemsia Khamis na Habiba Zaral, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, amewataka wananchi kisiwani humo, kuwa wamoja katika kuudumisha muumgano wa Tanganyika na Zanzibar kwa maslahi ya sasa na baadae.

Alisema maazimio ya Muungano ni kuwakusanya Waafrika katika kupata haki zao, ikiwemo kuwawekea makaazi mazuri na kuondoa ubaguzi, kwa lengo la kuleta maendeleo.

Aliyasema hayo  Chake Chake, alipokuwa akizungumza na wananchi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema usharikiano na maelewano yaliyoanzishwa na waasisi wa Muungano, yakiendelea kudumishwa nchi inaweza kuwa salama, sambamba na kukuza umoja uliopo.

Alisema kazi ya serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu kwa njia yoyote, ili wananchi waweze kuishi kwa salama, ambapo Muungano umeweza kusaidia katika hilo.


Akizungumzia mchakato wa katiba unaoendelea, alisema muundo wa serikai uliopo unakidhi mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake, Ofisa tawala mkoa wa kusini Pemba, Hanuna Ibrahim Massoud, alisema  Muungano umewafanya wananchi wote kuwa wamoja, hivyo ni vyema kuuenziwa ili uweze kudumu.

Nae Ofisa Mipango mkoa wa kusini Pemba, Matar Zahor Massoud, akisoma risala kwa niaba ya mkoa alisema, ni vyema wananchi kuunga mkono Muungano uliopo kwa faida ya wote.


Maadhimisho siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huadhimishwa ifikapo Aprili 26 kila mwaka, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema, utanzania wetu ni muungano wetu, tuulinde, tuimarishe na kuudumisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.