Habari za Punde

Michango ya Wajumbe wa Bunge la Katiba Dodoma

Na Mwandishi Wetu.
BAADHI ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, wameupiga marufuku Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutokwenda kufanya mikutano katika majimbo yao,ili kuiepusha nchi kuingia kwenye ghasia.

Wajumbe hao, waliyasema hayo jana wakati wakichangia sehemu ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba mjini Dodoma.

Mwakilishi kutoka makundi ya dini, Nouman Juma Jongo, akitoa maoni yake, alisema analishangaa kundi la UKAWA kuamua kuitumia Zanzibar kuendesha maandamano na kuiingiza nchi kwenye vurugu.

Alisema lazima kundi hilo litambue kuwa Zanzibar imechoka na vurugu za aina yoyote na haikubaliki kuona viongozi kwa UKAWA kutangaza kuiutumia Zanzibar kama ndio nchi ya kuendesha harakati zao.

Alisema wananchi wa Zanzibar hivi sasa wapo katika kuendeleza umoja wa kitaifa baada ya kuchoshwa na vurugu zilizosababisha vifo vya watu.

“Zanzibar tumechoka na vurugu tuangalie yaliotokea miaka ya nyuma, watu walikufa na sasa Zanzibar iko vizuri, kwa nini kambi ije ifungwe huku wakati hapa watu wameridhiana, hatutaki kwani wanaoathirika ni Wazanzibari,” alisema.


Kwa upande wake, Dk. Maua Abeid Daftari alilitaka kundi hilo lifanye mikutano yake Tabora au Singida ili nao wao waone raha, lakini Mwenyekiti wa bunge hilo, Samuel Sitta, alisema hata watu wa Tabora hawawataki UKAWA kwa sababu hawapendi vurugu.

Alisema ni vyema viongozi hao wakaona umuhimu wa kukaa pamoja, kwani ajenda waliyopanga kuitumia kwenye maandamano yao ikiwemo udini, ukabila na siasa chafu, vitachangia kuvuruga amani.

“Mimi naona hapa kuna jambo kwanini vurugu hizi ziletwe Zanzibar na viongozi wake kama Lipumba, alipaswa kupeleka UKAWA mji wa Tabora, Lisu nae aende nao huko Singida, tumechoka na vurugu Zanzibar,” alisema.

Nae Tawhida Galos Nyimbo, alisema vijana wa Zanzibar hawatakuwa tayari kuona kundi la UKAWA linaruhusiwa kufanya mikutano yake kwani wamechoka kuifanya Zanzibar chambo cha vurugu.

“Vijanaa wamenituma wanasema hawautaki UKAWA, sasa watafute pa kwenda kwani wana uwezo wa kwenda mikoa mingine na sio Zanzibar pekee,” alisema.

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe,akitoa mchango wake aliwaripua wanasheria wa UKAWA, akiwaita ni wanasheria wanaostahili kunyanganywa vyeti vyao kwa vile wamekuwa wakisema uongo.

Alisema viongozi hao wameamua kutumia taaluma yao kinyume na malengo ili kuipotosha jamii na kutimiza matakwa yao.

Alisema inashangaza kuona wanaojiita wasomi wa sheria, kudai Zanzibar inaweza kuwa Hongkong, wakati kuna visiwa vingi duniani havijafanana na nchi hiyo.

Mapema akitoa maelezo yake, Mwenyekiti wa Bunge hilo,Samuel Sitta, alisema kikao kinachoendelea hakihitaji akidi kwani kwa njia moja ama nyengine katiba mpya itapatikana

2 comments:

  1. ndugu jongo wewe huwezi kuwa msemaji wa wazanzibari, tumechagua mwl sefu kuwa msemaji na mtetezi wetu , na yeye akitereza kukubaliana na watanganyika tutamtimua tutafute mwengine mwenye kuweza kutukombolea visiwa vyetu

    ReplyDelete
  2. Ukweli huyu jongoo anatoka Zanzibar au, mbona kiherehere hivi na akapime akili yake kwanza

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.