SERIKALI
imetangaza bajeti ya shilingi bilioni 705.1 kwa mwaka wa fedha 2014/2015, ambapo
shilingi bilioni 399.8 zinatokana na mapato ya ndani na shilingi bilioni 305.3
ni mapato ya nje na misaada.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee,
alisema serikali inatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 374.7 kwa
shughuli za kawaida zikiwemo bilioni 184.5 fedha za mishahara ya wafanyakazi wa
umma.
Alisema
viwango vya mishahara hiyo vinakwenda sambamba na mabadiliko ya mishahara
kulingana na viwango vya elimu na uzoefu kwa watumishi wa umma.
“Kila
mfanyakazi atapata mshahara uliofanyiwa marekebisho kwa mujibu wa elimu na
uzoefu wake,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka huu imeangalia vipaumbele vikuu vinne, ambavyo ni afya, miundombinu, maji safi na elimu ambapo jumla ya shilingi bilioni 159.6 zikiwa sawa na asilimia 48.4 ya bajeti ya maendeleo, zinatarajiwa kutumika kwa miundo mbinu ya uwanja wa ndege ukiwemo ujenzi wa bara bara za kurukiwa ndege, kukamilishwa kwa maegesho pamoja na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba.
Alisema
shilingi bilioni 30.6 ambazo ni sawa na asilimia 9.3 ya bajeti ya maendeleo ya
zinatarajiwa kutumika katika sekta ya afya, ambapo elimu itatumia bilioni 28.4
sawa na asilimia 8.6 ya fedha za maendeleo.
Alisema
serikali pia imezipa kipaumbele huduma za maji safi na salama ambapo inatarajia
kutumia shilingi bilioni 26.8 sawa na asilimia 8.1 ya bajeti na kuongeza kuwa,
sekta hizo zinachangia maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kuhusu
mchango wa serikali kwa mwaka huu wa fedha, alisema serikali ilichangia
shilingi bilioni 65.6 ambapo washirika wa Mmaendeleo walichangia milioni 264.
Akizungumzia
suala la mfumko wa bei, alisema umeshuka kwa asilimia 9.4 hadi mwaka 2012
ambapo kwa mwaka 2013 ulikuwa asilimia 5, hali iliyotokana na mpango wa
serikali kupunguza kodi katika bidhaa za vyakula vikiwemo mchele, sukari na
ngano hasa kwa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Aidha
alisema uzalishaji wa mpunga ulichangia ukuaji wa uchumi ambapo serikali
inaendelea kudhibiti bei za vyakula zisipande.
Katika
kupunguza ajira kwa vijana nchini, alisema sekta ya uwekezaji ilizidi kwa mwaka
2013 ambapo ZIPA ilisajili miradi 35
iliyozalisha ajira 1365 wakati mwaka 2012 miradi 25 ilisajiliwa na kuzalisha
ajira 1,123 jambo ambalo lilikuza ajira kwa vijana hasa katika sekta binafsi.
Akizungumzia
kukua kwa pato la taifa alisema hadi mwaka 2013 lilikuwa shilingi bilioni
1442.8 wakati mwaka 2012 lilikuwa 1342.6 bilioni.
Hata
hivyo alisema bajeti ya mwaka huu imezidi kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na ya
mwaka jana ambapo ilikuwa bilioni 658.5 kati ya fedha hizo bilioni 380.6
zilikuwa fedha za nje na bilioni 277.9 zilitokana na mapato ya ndani.
No comments:
Post a Comment