Na
A K Khiari
Moja
katika utaratibu mzuri aliojiwekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, ni utaratibu wa kukutana na watendaji katika
wizara zake kila baada ya miezi mitatu ili kuweza kupata kujua yanayojiri katika
wizara hizo yakiwemo mafanikio, matatizo na changamoto zinazowakabili.
Utaratibu
huu pia humpa picha nzuri Mheshimiwa Rais kuweza kwanza kuwasikiliza watendaji
wake na kisha kutoa maagizo na maelekezo ya nini kipewe kipaumbele na yepi ya
kuzingatiwa katika kutekeleza maagizo ya Rais katika programu ya mpango kazi.
Kwa
utaratibu huu, lazima tumpongeze Rais wetu kwa kuweza kuwa karibu na watendaji bila ya kupitia Mawaziri au Makatibu wake na
kupata maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa wahusika wa ngazi za chini kama
wakurugenzi na kadhalika.
Ni
katika utaratibu huu tumeweza kuona jitihada za watendaji wanavyokuwa makini
katika kuziandaa ripoti za kuweza kumweleza Mheshimiwa Rais juu ya yaliyojiri
katika vitengo vyao.
Naamini
kuna mengi mazuri yamejitokeza katika utaratibu huu na ndio maana Mheshimiwa
Rais amekuwa akiuendeleza kila baada ya miezi mitatu na hivyo kuwapa watendaji
majukumu ya ziada ya kujipanga wakati wanapokwenda kuonana na Rais.
Katika
mrejesho ambao kwa mtu aliye mbali na jikoni (Ikulu) ambaye hupewa kila
kinachokubalika kutolewa na Ikulu kwa waandishi wa habari ni kwamba kumeonekana
kwamba Ikulu sasa si mahala tena ambapo kulipokuwa mbali na watendaji ambapo
kufika sehemu muhimu kama ile huwa ni nadra sana. Sasa kila baada ya miezi
mitatu hufika pale.
Ni
mwanzo na hatua nzuri ya kupongezwa kwa Rais wetu.
Hata hivyo kuna jambo ambalo
bado linanipa uzito katika kuamini kwamba utaratibu huu hauna changamoto ambazo zinaweza kukwamisha na kuleta tija
inayokusudiwa kwa sababu zifuatazo.
Kwanza
Ninaweza
kujiaminisha kwamba washauri wa Rais huwa wanafanya tathmini kila baada ya
miezi mitatu kuangalia utaratibu huu na kufanya mrejesho ( feedback) jinsi
wanavyouona ila siioni sehemu yoyote inayoonesha kuwepo kwa kuhakikiwa Ripoti hizi
ili kuona maendeleo yale (Progressive) isije kuwa na umahiri tu wa kuandikwa
ripoti hizi ila panapokuja utekelezaji ni kwamba kama hubakia kwenye ripoti tu.
Je
Mhe Rais ameweza kujipangia utaratibu mwengine wa kuchagua japo baadhi ya ripoti hizi (randomly) na kufanya
ziara hasa za ghafla (field) kuweza kujionea hali halisi ili akapata picha ya
kinachoendelea (reality on the ground) ili alinganishe na anacholetewa? Au
ameridhishwa na maelezo ya watendaji wake na hivyo hakuna haja ya kufuatilia
zaidi? Ninafahamu kutingwa kwa majukumu mengi kwa Mhe Rais lakini akipata muda
japo mdogo basi ni vyema tungelimuomba angeliutumia katika kuhakikisha anapata
kuona upande mwengine wa shilingi.
Khalifa
Umar ibnul Khattaab, alipokuwa Kiongozi wa Waislamu (Amiirul Muuminiin),
alikuwa akitoka usiku kwenda kukagua na kujionea mwenye hali halisi ya wananchi
wake. Alifika Marikiti kuhakikisha kwamba maagizo aliyokuwa akiyatoa yanatekelezwa
na hakuridhishwa tu na kutoa, maagizo na kisha kusubiri ripoti, alijiwekea
utaratibu maalum wa kukagua yeye mwenyewe.
Pili
Sijui
kama iliwahi kuripotiwa ila sijapata kusikia au kwa waandishi wa Rais kutoa
maelezo kwamba Ripoti fulani imekataliwa na Rais kwa sababu A, B C. Wakati
mwengine ripoti ukisomewa tu kwa mtu mwenye akili yenye upeo wa kuona mbali
inakupa picha halisi kwamba hapa kuna kitu kina walakini. Niliwahi kumuona Rais
wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, akiikataa rasmi ripoti ya mafuriko yaliyotokea
Morogoro mwaka jana papo hapo tena mbele ya hadhara ilipotolewa na kumuamuru
Mkuu wa Mkoa kwenda kuiandika upya ili ikidhi vigezo vya kuwa ripoti.
Ushahidi
uliomsukuma Rais Kikwete kuikataa ripoti ile ni kwamba kila ilipokuwa ikisomwa
wananchi waliguna na kuzomea na hapo mheshimiwa Rais kuhisi kuna namna.
Watendaji
wako wanapokuja Ikulu, mhe Rais hawana wa kuwazomea wala wa kuguna ili
kukushtua kwamba kilichomo kwenye ripoti hizi kina walakini. Lakini upeo wako
wa kufahamu mambo na kuyapima yanaweza kukupa taswira kwamba sasa tumepata
mabingwa wa kuandika ripoti zilizokosa dira ya utendaji uliotukuka.
Utendaji
wa aina hii hauwatii tumbo joto wahusika na kujenga mazingira
kinachotakiwa si ripoti bora bali bora
ripoti.
Tatu
Miongoni
mwa dhana za utawala bora ni dhana ya uwazi (transparency) na dhana ya
uwajibikaji (accountability). Dhana hizi mbili ni muhimu sana katika kujenga
taifa litakalokuwa imara na kuwa na maadili ya kusimamia mikakati na maazimio
ya Serikali husika na kujenga umuhimu wa kujua wajibu na majukumu ya kila mmoja
na kuhakikisha anayetekeleza ipasavyo.
Azma
ya Rais wetu katika kuhakikisha haya yanakuwepo ni kuanzishwa Wizara maalum
inayosimamia utawala bora.
Sijaona
bado dhana ya uwazi au uwajibikaji katika uwasilishaji wa ripoti hizi na feedback zake endapo yale
yaliyopangwa kutekelezwa na Wizara fulani yameshindwa kutekelezeka na kuundiwa
sababu za kushindwa na sababu hizi kuonekana si za msingi. Je mara zote watapewa
fursa nyengine wakajirekebishe? Au wataweza
kuwajibishwa?
Dk.
Shein alipokutana na watumishi wa Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwataka kuifahamu vyema dhana ya
utawala bora ili wawe mfano wa kuigwa katika kuitekeleza dhana hiyo kwa vitendo.
Kama
ni dhana ya utawala bora, basi inahitaji kuonekana kwa vitendo si kwa watumishi
tu bali tokea kwa mheshimiwa Rais mwenyewe akionesha vipi anaisimamia dhana hii
si kinadharia tu bali katika uhalisia wake.
Ikiwa
Mhe Rais keshaonesha njia, anatakiwa kuwa mstari wa mbele na kutokuwa na
kumsalia Mtume wala kuwa na muhali kwa wote wanaokwenda kinyume na dhana hii na
hapo atajenga kigezo bora na nguzo muhimu kwa walio chini yake kuitekeleza
dhana kikamilifu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Mhe
Rais, ni kweli kama ulivyowazindua watendaji kwamba wasifike wakati watumishi wakajiona kuwa wao ni watu wasioguswa na
wasiohojiwa, mbona tayari wapo!!!.Ndiyo maana tunakuzindua jaribu kufanya ziara
za ghafla ukajionee hali halisi!.
Vyenginevyo
mhe Rais, hii itabakia kuwa ni dhana tu iliokosa meno na iliokosa mwega wa
kuisimamia ikaweza kuisaidia serikali ili isimame katika kutekeleza misingi hii
miwili muhimu ya uwazi na uwajibikaji na kupatikana kwa utawala bora.
No comments:
Post a Comment