Habari za Punde

Dk Shein : Zanzibar inajivunia uhusiano wake na Misri

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                               28 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemshukuru Balozi mdogo wa Misri aliyemaliza muda wake Mhe Walid Mohamed Ismail kwa kutimiza wajibu wake vyema wa kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Misri wakati wote akiwa nchini.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi Walid ambaye alifika Ikulu kumuaga kuwa, katika kipindi cha miaka minne ambayo Balozi Walid ameitumikia nchi yake humu nchini, Zanzibar na Misri zimeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yao.
 
Aliongeza kuwa Zanzibar inajivunia sana uhusiano wake na Misri kwa kuwa umekuwa wa karne nyingi na kutolea mfano kuwa Misri ni moja ya nchi za mwanzo ambazo Zanzibar ilianzisha ubalozi wake mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
 
Alibainisha kuwa chini ya uhusiano huo mzuri na thabiti Zanzibar na Misri zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbali mbali kama vile elimu, afya na kilimo ambapo ushirikiano huo umekuwa ukijumuisha msaada wa kiufundi kwa kubadilishana wataalamu katika sekta hizo.
 
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Misri kwa misaada yake mbalimbali kwa Zanzibar na kutolea mfano msaada wa hivi karibuni ambapo Serikali hiyo imeipatia Zanzibar vifaa kwa ajili wagonjwa wenye matatizo ya figo.
 
Dk. Shein alieleza kuwa vifaa hivyo vitakuwa mwanzo wa safari ndefu ya dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma za tiba kwa wagonjwa wanaougua maradhi ya figo nchini.   
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza matumaini yake kuwa kasi ya kuimarisha mashirikiano kati ya Zanzibar na Misri itaendelezwa na Balozi mdogo anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Balozi Walid.
 
Kwa hiyo alieleza haja ya kutilia mkazo ushirikiano katika maeneo mengine yakiwemo utalii na utamaduni ambapo Misri imepiga hatua nzuri na ina uzoefu kubwa.
 
Kwa upande wake Balozi Walid alimueleza Mhe Rais kuwa amefurahi kuona kuwa katika kipindi cha miaka minne aliyoitumikia nchi yake, Zanzibar imeweza kufanikisha masuala mengi yaliyomo katika ushirikiano kati ya nchi yake na Zanzibar.
 
Alibainisha kuwa pamoja na nchi yake kuweza kuendelea kutoa fursa za masomo kwa vijana wa Zanzibar lakini pia mpango wa kuwaleta madaktari wa Misri ambao ulisimama kwa kipindi kirefu sasa umo mbioni kurejeshwa tena.
 
Balozi Walid alisifu ukarimu wa wananchi wa Zanzibar na kuahidi  kuwa balozi mzuri kuitangaza Zanzibar.   
 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.