Na
Mwandishi wetu
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametembelea kiwanda
kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote duniani cha Dangote Cement
Obajana Plant kinachomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Aliko Dangote,
ambaye pia anajenga kiwanda kikubwa cha saruji mjini Mtwara.
Akiandamana
na Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda, kwa siku nzima, Rais Kikwete
alitembelea kiwanda hicho kilichoko katika eneo la Obajana, jimbo la Kogi,
kilomita 400 kaskazini mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Nigeria,
Lagos.
Rais
Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria kongamano ya uchumi
Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu, aliamua kutumia siku yake ya mwisho ya ziara
yake ya siku tatu nchini humo, kwa kutembelea uwekezaji mkubwa wa mwekezaji
ambaye ameanza ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Mtwara ambacho kitakuwa kiwanda
kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote katika Tanzania, kikiwa na
uwezo wa kuzalisha tani za kimetriki milioni tatu kwa mwaka.
Rais Kikwete ambaye alipokewa kwenye uwanja wa
ndege wa kiwanda hicho na Dangote mwenyewe, na kuanza ziara yake kwa kutembelea
machimbo ya kiwanda hicho ambayo yako kilomita tisa kutoka kiwandani ambako
malighafi ya kiwanda hicho husafirishwa kwa madaraja na mikada maalum hadi
kiwandani.
Alimwambia
Rais Kikwete kuwa kwa sasa kiwanda cha Obajana kinazalisha tani za kimetriki
milioni 10.25 kwa sasa kwa mwaka na hivyo kukifanya kiwanda hicho kuwa kiwanda
kikubwa zaidi cha saruji duniani kilichoko katika eneo moja na kuwa baada ya
upanuzi unaoendelea kufanywa kwenye kiwanda hicho, uwezo wake wa uzalishaji
utaongezeka na kufikia tani za kimetriki 13.0 kwa mwaka ifikapo mwakani 2015.
Dangote alimwambia
Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilicho kwenye eneo la kilomita za mraba saba
kitakuwa kimegharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5 wakati upanuzi wake
utakapokamilika.
Kwa sasa
kiwanda hicho kina biashara ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka.
Bilionea
huyo alimwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2003
na kukamilishwa 2006 na hatimaye kuzinduliwa na Rais Olusegun Obasanjo Mei 12,
mwaka 2007, wiki mbili kabla ya kustaafu urais wa Nigeria, kinaajiri watu 800
kwa wakati mmoja na hivyo kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa zaidi katika
Nigeria.
“Mheshimiwa
Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na kijamii za kiwanda hiki na
viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya Nigeria, unahitaji kukumbuka
kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria nzima ilikuwa na uwezo za
kuzalisha tani za kimetriki za saruji milioni 1.5 tu, wakati huo chini ya miaka
10 iliyopita,” alisema.
"Tunataka
kufikia hatua ya kuhakikisha kuwa eneo la Afrika Magharibi na hata bara letu la
Afrika linaacha kabisa kuagiza saruji nje ya bara letu na tutafikia huko,” alisema.
Mbali na kiwanda
cha Obajana, kampuni ya saruji ya Dangote inazalisha saruji katika maeneo
mengine mawili ya Nigeria
ambalo uzalishaji wa jumla wa maeneo hayo matatu ni tani za metriki 20.25 kwa
mwaka.
Alipoulizwa
na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna yoyote umeme wa taifa, Dangote
alijibu kwa furaha,
“hatujaunganishwa kwenye gridi ya taifa na tunadhani hili
ni jambo zuri kwa sababu hatua tulizochukua zinatuhakikishia umeme wakati wote
na kwa kiwango ambacho tunakihitaji. Tunatumia gesi ama diseli yetu wenyewe. Na
wala siyo umeme tu, hata miundombinu ya eneo hilo kiliwemo daraja hili kubwa
linalounganisha eneo la machimbo na kiwanda, tumejenga sisi,” alisema.
Alisema
mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lake lenyewe
kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma
ya maji ya serikali.
Aidha,
bwawa hilo
linatoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Mbali na
shughuli za kiwanda, kampuni ya Dangote inashiriki kwa karibu shughuli za jamii
inayozunguka kiwanda ambacho kwa sasa imeanzishwa miji midogo saba katika eneo lililokuwa
pori lenye
nyumba 50 za wenyeji tu kabla ya shughuli za kiwanda hicho kuanzishwa.
Alimwambia
Rais Kikwete kuwa kampuni yake inatoa misaada katika sekta za elimu, maji na
umeme kwa wananchi ambao wanazunguka kiwanda ambacho tokea kuanzishwa kwake kimevutia
mabenki 13 ambayo yameanzishwa matawi yake katika eneo la kiwanda.
Alisema mbali
na kutoa huduma nyingine za kijamii, kampuni ya saruji ya Dangote inajenga
taasisi kubwa ya elimu ya Dangote
Academy ambayo itatoa
elimu na mafunzo ya kiufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho
na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Alisema
kampuni yake inafanya jitihada kubwa kuhakikisha Rais Kikwete anakifungua
kiwanda cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao.
Mbali na
Nigeria na Tanzania, Dangote ana viwanda ama anajenga viwanda vya saruji na
shughuli za saruji katika nchi 14 za Afrika ikiwamo Ethiopia, Zambia, Msumbiji,
Kenya, Senegal na Sierra Leone, Afrika Kusini, Congo (Brazzaville), Cameroun,
Ghana, Liberia na Ivory Coast.
Aidha
Dangote ambaye anakubaliwa kuwa tajiri mkubwa zaidi katika Afrika kwa thamani
ya dola za Marekani bilioni 25 yeye na kampuni yake ya Dangote Group pia ina
shughuli za uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa chumvi, utengenezaji wa
magunia, uzalishaji maji, uzalishaji wa vyakula vya aina mbali mbali,
uzalishaji wa mafuta ya kupikia na utengenezaji wa nyanya.
Kwa sasa
anaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea na kile cha kuzalisha bidhaa za
petrol na kemikali.
No comments:
Post a Comment