Na
Francis Rikanga, ARUSHA
WATU
14 wa kijiji cha Engalaoni kata ya Mwandet mkoani Arusha, wamepigwa na
kujeruhiwa vibaya na kikundi cha watu wanaosadikiwa wanatoka wilaya ya Monduli,
waliovamia na kujenga makazi katika maeneo ya malisho yaliyotengwa na wafugaji
wa wilaya ya Arumeru kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Watu
hao walishambuliwa kwa sime, mikuki fimbo na marungu na wamelazwa hospitali ya
Selian mkoani Arusha na baadhi yao
kuruhusiwa huku mmoja wao akiwa katika hali mbaya.
Akizungumza
na waandishi wa habari kijijijini hapo, Diwani wa kata ya Mwandet, Bonifas
Mollel, alisema watu hao walijeruhiwa na kikundi cha watu kutoka wilaya ya
Monduli.
Aliwataja
watu hao kuwa ni Melau Taiko, Muyae Kuresoi, Lengai Kivuyo, Mepalaari Kuresoi,
Lomnyak Meijo, Akui Lomeji na Isack
Lesikar.
Wengine
ni Loitore Lomeji, Balozi Kapurwa, Moiyo Kapurwa, Shiiki Korduni, Losieku
Kimani, Taiko Kuresoi na Kooki Sane, ambaye hadi sasa amelazwa hospitali baada
ya kujeruhiwa vibaya kichwani na kukatwa vidole vinne vya mkono wa kulia.
“Kwa
kweli serikali haina budi kukidhibiti kikundi hiki, watu wanapigwa kama wanyama. Huyu mzee Kooki Sane amepigwa vibaya, kichwa
hakifai, tumboni hadi kifuani amechomwa na mkuki na amekatwa vidole vinne vya
mkono wake wa kulia, watu hawa ni lazima serikali sasa iwadhibiti,” alisema.
Aidha,
alisema pamoja na watu hao kupigwa na kujeruhiwa, maboma yao yamechomwa moto na mifugo kuteketezwa na
kusababisha hasara kubwa huku mifugo mingine ikiibiwa.
Alisema
katika maboma 35 yaliyochomwa, ndama 12, mbuzi 30, dawa za mifugo, nguo na
vyombo mbalimbali vya wafugaji navyo viliteketezwa.
Aidha,
alisema tokea watu hao wavamie maeneo hayo, mifugo 103 na punda 26 wameibiwa.
Uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini kuwa vurugu hizo zimekuwa
zikitokea mara kwa mara na chanzo ni watu wa Monduli kuzuia mifugo ya wilaya ya
Arumeru kuingia katika maeneo ya malisho pamoja na kuwa maeneo hayo ya malisho
yapo ndani ya wilaya ya Arumeru.
Katibu
wa Umoja wa Wafugaji wa wilaya ya Arumeru, Yohanes Emanuel Lomanyaa, alisema
mipaka ya wilaya ya Aumeru iko wazi na tayari wamemtembeza mkuu wa wilaya ya
Arumeru kukagua mipaka hiyo.
No comments:
Post a Comment