Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi akijumuika na baadhi ya Wananchi kuangalia athari iliyojichomoza
kwenye nyumba ya Bwana Salim Ahmed Salim baada ya ukuta na dari yake
kuanguka saa sita usiku juzi mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja
Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Sehemu ya mbele ya Nyumba ya Bwana Salim
Ahmed Salim iliyoporomoka Mtaa wa Vuga mkabala na Skuli ya Sekondari ya
Tumekuja.Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana
na athari hiyo.
Athari ya nyumba iliyobomoka hapo Mtaa wa
Vuga ilisababisha usumbufu wa watumiaji wa Bara bara itokayo Vuga kuelekea
Shangani au Serena na kulazimika kufungwa kwa bara bara hiyo.
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar , Jeshi la Polisi
pamoja na Mamlaka ya Usafiri zimekumbushwa kuendelea kuzuia uingiaji wa
gari kubwa zenye uzito wa zaidi ya Tani Mbili katika eneo la Mji Mkongwe ili
kunusuru majengo yaliyono ndani ya mamlaka hiyo.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi kukagua athari ya nyumba iliyoporomoka ukuta na Dari yake juzi usiku iliyopo Mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ukaidi wa baadhi ya madereva wa gari kubwa kupitisha Gari gari zao katika eneo hilo umesababisha uchafuzi wa mandhari na haiba ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao hivi sasa uko katika urithi wa Kimataifa.
“ Jeshi la Polisi wakati huu litahitajika kuwa na kazi ya ziada katika kuhakikisha agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimpa pole
Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim Ahmed Salim kwa hasara
aliyoipata alimtaka kuwasiliana na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe
wa Zanzibar katika juhudi zaujenzi wa nyumba hiyo utakaozingatia
mpango halisi wa uhifadhi wa Mji huo.
Akitoa ufafanuzi wa athari nyingi
zilizojitokeza ndani ya nyumba za Mji Mkongwe, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano
na Utafiti cha Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Bibi Madina Haji
Khamis alisema ujenzi usiozingatia utaalamu wa Mamlaka husika pamoja na
upitishwaji wa gari kubwa ndio sababu kubwa za msingi za athari hizo.
Bibi Madina alifahamisha kwamba baadhi ya
wamiliki wa nyumba hizo walikuwa wakipandishia kuta wakati wa
ujenzi au matengenezo zaidi ya uwezo wa msingi wa nyumba hizo hali
inayoleta athari ya mipasuko ya nyumba hizo sambamba na mitetemeko ya
gari kubwa zinazopitishwa pembezoni mwa nyumba hizo.
Mapema Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim
Ahmed Salim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwamba dalili za kuanguka kwa jengo hilo zilijionyesha mapema kutokana na
kuvimba na baadaye kupasukwa kwa eneo la mbele la ukuta wa nyumba hiyo.
Bwana Salim alifahamisha kwamba kutokana na
hali hiyo alilazimika kuuarifu Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliolazimia
baadaye kwa kushirikiana na jeshi la Polisi kuchukuwa hatua za kuifunga bara
bara hiyo.
“ Nilijaribu kuufuata Uongozi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Mji Mkongwe uniruhusu kuifanyia matengenezo makubwa nyumba yangu
ili baadaye niitumie kwa makazi na familia nyangu lakini bado sijapata
jibu na huku inaporomoka “. Alieleza Bwana Salim Ahmed Salim.
Nyumba hiyo ya ghorofa moja mpaka
inaporomoka ukuta na dari yake majira ya saa sita juzi usiku lakini hamna watu
waliokuwa wakiishi ndani yake.
Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa
kushirikiana na Taasisi nyengine zimelazimika kuzuia Gari zote
zinazotumia Bara bara hiyo kutoka Vuga kuingia Shangani au kupitia
Serena ili kujaribu kuepuka hatari katika kipindi hichi cha Mvua za
Masika.
Kwa mujibu wa hali halisi ilivyo hivi
sasa gari zote zinazokusudia kuingia ndani ya eneo la Mamlaka ya Mji Mkongwe
zinalazimika kutumia Bara bara itokayo Malindi na zisizidi uzito wa zaidi ya
Tani mbili.
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar
kwa miaka kadhaa sasa imo ndani ya Ramani ya Dunia ya urithi wa hifadhi ya
Kimataifa chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na
Utamaduni { UNESCO }.
Sasa kipi ni sahihi kati ya kuporomoka kwa jengo hilo kati ya kupita magari makubwa,mvua,uchakavu wa umri wa jengo au majengo au ingredients zilizotumika katika kujenga jengo hilo.Wacheni kudanganyana jamani na mkazibwa macho na Unesco kwa uhifadhi wa mji mkongwe.Ikumbukwe kwamba majengo hayo yote ya mji mkongwe yalijengwa miaka 200 iliyopita kwa kuchanganywa dongo,chokaa na mawe.Sasa hayana uhimili tena maana yamechoka.Yakirowa maji yanajiachia,vishindo kidogo ndio safari.Ikumbukwe pia Unesco wanaziba macho suala la uhifadhi maana huko makwao Unesco majengo yaliyojengwa kwa saruji,na zege wakiyaona na athari kidogo tu basi ni kuvunjwa ku-demolish na kujengwa jipya lenye kila aina ya proof-kama ni fire proof,water proof au hata tetemeko - earthquake proof . Kwetu sisi wanatuziba macho kwa vijipesa wanavyochangia.Tusipokuwa macho naamini majengo ya mji mkongwe yataleta maafa makubwa kwa kupoteza roho za watu.
ReplyDelete