Habari za Punde

Lawama haitoshi kwa ndoa za utotoni

Na Salim Said Salim
 
KWA miaka nenda miaka rudi sasa imekuwa ni kawaida panapokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuona sherehe za harusi zimetanda karibu kila pembe ya Zanzibar.
 
Watu hufurahi na kula mapochopocho na kucheza ngoma kwa furaha. Lakini kumbe badala ya kusherehekea jambo zuri huwa wanashiriki kufurahia jambo ambalo sio zuri na halina kheri kwa wanandoa na jamii kwa jumla.
 
Hapana ubishi hata kidogo juu ya uzuri wa watu kufunga ndoa ili kuanza maisha mapya kwa lengo la kukidhi kihalali mahitaji ya maumbile na kutaka kuwa na familia zao kama walivyofanya wazee wao miaka ya nyuma.
 
LiIilo muhimu hapa na linalohitaji kuangaliwa kwa makini ni nani hao watu wawili wanaofunga pingu za maisha.
 
Kinachosikitisha hapa ni kuona baadhi ya ndoa hizi zinawajumuisha wale ambao hutakosea kama utawaita watoto kwani baadhi yao huwa bado ni wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
 
Hivi karibuni yamesikika tena malalamiko juu ya hizi ndoa za utotoni kuendelea na kusababisha baadhi ya watoto wa kike kulazimika kukatisha masomo na kuagana na kusaka elimu ambayo ni nyenzo muhimu kwa maisha yao baadaye.
 
Kwa mfano katika shule ya kisiwa cha Kojani, Kaskazini Pemba, zimesikika habari za wanafunzi watatu wa kike kukatishwa masomo na wazee wao wiki chache zilizopita ili kupewa waume.
Hii ni taarifa ya kusikitisha na ambayo haistahili kupuuzwa na jamii.
 
Walimu wa shule hiyo wamewatupia lawama wazee kwa kuchukua hatua hiyo ya kuwakatisha mabinti zao masomo na kuwapa waume.
 
Lakini ukichunguza utaona sio hao wazazi pekee wanaostahili kubebeshwa lawama kwani sababu kubwa ya hawa wazee kuchukua hatua hiyo ni ukosefu wa elimu ya kutosha.
 
Viongozi wa serikali, vyama vya siasa, dini na taasisi za kiraia nao wanapaswa kulaumiwa kwa kutotekeleza wajibu wao ipasavyo wa kutoa elimu ya kutosha kwa wazee ambao hawaelewi athari na hatari za kuchukua hatua hii.
 
Tatizo lililopo Zanzibar ni kwamba viongozi wengi wamejikita katika siasa na masuala ya uchaguzi na kusahau wajibu wao wa kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ya maisha, kama ya ubaya wa hizi ndoa za utotoni.
 
Viongozi wengi wa dini nao wamejikita katika kuzungumzia zaidi jambo gani litamsaidia muumini kwenda peponi na lipi litamtia motoni baada ya kumaliza hii safari yetu ya mpito hapa duniani.
 
Kinachosikitisha zaidi ni kusikia baadhi ya hao wanaoitwa masheikh kufika hadi kuwataka vijana kuoa wake wanne kwa siku moja – wa kwanza baada ya Sala ya Adhuhuri (saa 7 mchana), baada ya Sala ya Alasiri (saa 10), baada ya Sala ya Magharibi (saa 1 usiku) na baada ya Sala ya Isha (saa 3 usiku).
 
Sababu wanayotoa ni kwa kuwa dini ya Kiislamu imehalalisha mwanamume kuoa wake wanne. Kama huu sio wazimu ni kitu gani?
 
Kwa fikra zangu, hotuba za viongozi wa dini kama hawa, hazifai kutangazwa katika vyombo vya habari na ikiwezekana kuwafungia watu wa aina hii kutoa mihadhara.
 
Ni vizuri kwa viongozi wa sekta mbalimbali kubadilika na kutoa umuhimu kwa suala hili kwa kutoa elimu ya kutosha juu ya ubaya wa ndoa za utotoni kwa hao wanaofunga pingu za maisha, jamii na taifa kwa jumla.
 
Ni lazima pafanyike juhudi kubwa za utoaji wa elimu hii, hasa katika maeneo ya vijijini na zaidi katika sehemu ambazo watu wake hawana uelewa mzuri wa suala hili.
 
Huu mtindo unaoonekana sasa wa lawama… lawama… lawama… hausaidii. Kinachotakiwa ni kuchukua hatua za kuirekebisha hali hii na sio kila mmoja kumnyooshea kidole cha lawama mwenzake.
 
Viongozi wa dini wanasikilizwa sana na kuheshimiwa na jamii. Kwahivyo ni muhimu kutumia nafasi hii kuelimisha waumini juu ya hatari na ubaya wa hizi ndoa za utotoni, ikiwa pamoja na kuwakatisha watoto masomo.
 
Hili linaweza kuwa na mafanikio makubwa kama viongozi wa dini watatumia muda katika mihadhara yao misikitini, kama ya Sala ya Ijumaa na Misa ya Jumapili kanisani, kuzungumzia suala hili.
 
Hata pale watakapotakiwa kuwafungisha ndoa watoto wadogo wakatae na kuwaeleza wanaotaka kuoana na wazee wao juu ya umuhimu wa kuvuta subira.
 
Tatizo lililopo ni kuwa hawa wazazi, pamoja na hao wanaotaka kuoana, hawaelewi madhara ya baadaye ya kufunga ndoa ikiwa mmoja wa maharusi au wote wawili ni wenye umri mdogo au mmoja wao analazimika kukatisha masomo.
 
Wanasiasa wetu, hasa wabunge na wawakilishi, wanapaswa pia kulipa umuhimu suala hili kama vile wanavyopiga kampeni ya kupata kura katika majimbo ya uchaguzi waliosimama kama wagombea.
 
Tunapozungumzia maendeleo ya watu wetu sio kuwa na barabara, shule na vituo vya afya tu, bali ni pamoja na kuwapa elimu wapiga kura wetu ya kujua jambo gani ni zuri na lipi baya.
 
Wawakilishi na wabunge wanao wajibu pale wanaposikia habari za msichana mwanafunzi kuposwa na kufanyika mipango ya harusi kuingia kati na kusaidia kuisimamisha ndoa hiyo ili binti aweze kuendelea na masomo bila ya usumbufu.
 
Walimu wanaweza kusaidia sana kwa kutoa taarifa mapema na sio kusubiri hadi ndoa zimefungwa na bwana na bibi kutangazwa kama mke na mume ndio baadaye kusikika wakilalamika.
 
Uzoefu wa miaka mingi umeonyesha kuwa watu wetu, hasa wa vijijini ni wasikivu wanapopewa ushauri mzuri na kuuelewa.
 
Kinachohitajika hapa ni kufanyika kampeni iliyoandaliwa vizuri na iwe kwa kutumia hekima na busara na sio kwa kutumia amri na vitisho.
 
Tunapoifanya kampeni hii tukumbuke wasia uliojaa hekima na busara wa wazee wetu unaosema “hiari inashinda utumwa.”
 
Vyombo vya habari vya Visiwani vya serikali na binafsi na hasa hizi redio za jamii zilizochipuka hivi karibuni, ambavyo vinaonekana kutumia muda mwingi kushughulikia hotuba za kisiasa za viongozi na mambo ya muziki, navyo vinalazimika kubadilika.
 
Suala hili la ndoa za utotoni linapaswa kupewa umuhimu kwa kutoa elimu na kufanya mijadala itakayosaidia kuwapa wazee uelewa mzuri juu ya hizi ndoa za utotoni.
 
Nchi nyingi na hata baadhi ya maeneo ya nchi yetu ziliwahi kukabiliwa na tatizo hili. Ni vizuri kufanya utafiti wa kina wa kuelewa mbinu gani zilitumika hata jamii ya nchi hizo ikabadilika.
 
Kwa kuelewa uzoefu uliopatikana katika sehemu mbalimbali, vyombo vyetu vya habari vinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuifanya jamii, kama ya watu wa Kisiwa cha Kojani kubadilika.
Kuwanyooshea kidole cha lawama bila ya kutoa elimu, hakusaidii watu wenye elimu ndogo kama wazazi wa Kojani na watoto wao.
 
Kwa upande mwingine, zipo sheria zinazolenga kuzuia ndoa za utotoni. Ni vyema kuhakisha sheria hizo hazibaki katika makaratasi, bali zinatumika kama zinavyoelekeza.
 
Ni kwa jamii tu kushirikiana na kupeana elimu ya kutosha ndiyo tutaweza kuzuia hizi ndoa za utotoni na kuwapa watoto wa kike haki yao ya kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya siku za mbele.
 
Hili ni tatizo letu sote na sio la watu maalumu. Tushirikiane na tushauriane ili tupate ufumbuzi wa uhakika utakaosaidia leo na baadaye familia ambazo zinaendeleza mwenendo huu bila ya kuelewa athari na hatari zake.
 
Kwa pamoja tunaweza kufanikiwa kukomesha ndoto za utotoni, lakini kila mmoja akikaa pembeni na kulaumu ndoa hizi zitaendelea na kuwa na athari kubwa kwa jamii na taifa.
 
Chanzo - Tanzania Daima

3 comments:

  1. Muandishi habari nyengine usituekee ndoa za utotoni ndio zipi? Masheikh wasiwambie watu waoe wake wanne kwanini na dini inaruhusu kama unauwezo wa kuwahudumia kuwafanyia justice, umebugi step muandishi mabaya yote yanayotendeka Zanzibar ulimwenguni unatuekea ndoa za utotoni hebu tufafanulie ndoa za utotoni ndio zipi ??

    ReplyDelete
  2. Hata tuwe wanne tutabanana hapo hapo.Muandishi umeishiwa kwa hivyo nyamaza..

    ReplyDelete
  3. Kwa suala hili ndugu muandishi umekwenda mchomo.Mara kadhaa huwa unaandika ukiambatanisha na historia lakini leo umeisahau historia ya kidini pale muongozaji mkuu wa dini ya Kiislam alipomuowa mwnamke hata hajawa balegh na ulipomjia ukubwa binti huyo akawa naye .Jee alikosea na jee wasema haifai kumfata nyayo zake .Kumbuka bwana mtume (saw)kahusia kuwa binti anapopata ukubwa asiwekwe ikiwezekana apewe mwenziwe.Jee wewe hukubaliani na mahusio hayo.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.