Habari za Punde

Michuano ya Kombe la ZEWADA Kaskazini B Unguja.

Na Othman Khamis Ame OMPR.
Timu ya Soka ya African Coast ya kijiji cha Upenja Wilaya ya Kaskazini “ B” imeanza  vishindo vyake vizito katika mashindao ya Kombe la Zaweda baada ya kuitandika timu ya Kitope United kwa Magoli 3 -1 katika pambano la fungua dimba la mashindano hayo yanayotarajiwa kushirikisha Timu 12 za Soka.

Pambano hilo lililofanyika katika uwanja wa Santiago Benabao Kitope lilishuhudiwa na mamia ya wapenzi wa soka wa Jimbo la Kitope na Vitongoji vyake ambapo mgeni rasmi wa ufunguzi huo alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo akiambatana na Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Ibrahim Makungu { Bhaa } pamoja na Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi.

Kitope United ndio iliyoanza kuliona lango la African Coast ndani ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo kwa goli safi na la kuvutia lililofungwa na mchezaji makeke wa Timu hiyo Mateo Jackob.

Dadika sita baadaye ndani ya kipindi hicho cha kwanza Mchezaji Idrissa Makame wa African Coast akaisawazishia Goli timu yake na kuwafanya mafahali hao wawili wanakwenda mapumziko wakiwa nguvu sasa ya goli moja kwa moja.

Turufu ya African Coast ikaanza kung’ara ndani ya kipindi cha pili pale mchezaji wake mahiri Kitwana Hassan alipopachika kimiani Goli la Pili baada ya gonga safi iliyopigwa na wachezaji hao.

Amour Haji akahitimisha karamu ya magoli yaliyotinga kimiani mwa Kitope United na kuifanya Timu hiyo ya walima mpunga kutoa kifua mbele kwa magoli matatu kwa Moja dhidi ya wenyenyeji hao wa mashindano hayo Kitope United.


Akipiga mwaju wa Penalti kuashiria uzinduzi rasmi wa mashindano hayo Mgeni rasmi Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo alitoa ofa kwa timu tatu za mwanzo za mashindano hayo na zile zilizoshinda kombe la Muungano ndani ya Jimbo la Kiembe Samaki kushindana ligi  ya pamoja kati ya majimbo hayo mawili.

Mahmoud Thabit Kombo aliyataka mashindano hayo yawe ya amani na upendo ili lengo lililokusudiwa la kuwashirikisha vijana katika sekta ya michezo na kuondokana na vitendo viovu lifikiwe vyema.

Akitoa Taarifa fupi msimamizi wa mashindano hayo Rashid Tamimu alisema lengo la kuanzishwa ligi hiyo ni kuwafanya vijana wapende michezo chini ya usimamizi wa Jumuiya isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji wa taaluma ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana { ZAWEDA }.

Hata hivyo Tamimu alisema bado zipo changa moto ndogo ndogo zinazokwamisha malengo sahihi ya kamati ya mashindano hayo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa posho kwa ajili wa waamuzi wa mashindano hayo.

Msimamizi huyo wa Zaweda Cup alielezea zawadi maalum zitakazotolewa kwa washindi wa ligi hiyo akizitaja kuwa ni fedha taslim shilingi Laki 500,000/-, Seti ya Jezi, Kikombe, Mipira pamoja na Seti ya Tv na Dikoda yake itakayotolewa na Mke wa Mbunge wa Jimbo hilo Mama Asha Suleiman Iddi.

Mshindi wa Pili atazawadiwa shilingi Laki 300,000/- taslim, Jezi, Kikombe pamoja na Mipira wakati mshindi wa tatu atajinyakulia shilingi Laki 200,000/- jezi na mpira na timu zote shiriki zitapata zawadi ya mipira.

Mashindano hayo yanashirikisha timu 12 za mchezo wa soka za Jimbo la Kitope zikiwemo pia mbili za kualikwa nje ya Jimbo hilo.

Timu hizo ni  Kitope United wenyeji wa mashindano hayo, African Coast ya Upenja,African Boys ya Kazole, Matetema ya Kazole, New Star ya Kiwengwa, Kichungwani, Lindi Boys, Mbuyuni, Kombora,Zaweda wasimamizi wa ligi hiyo pamoja na timu mbili zilizoalikwa ambazo ni Mahonda Kids na Kilimani City.

Mapema mchana mashindano hayo yalianza kwa ligi ya mchezo wa Pete  yatakayoshirikisha timu sita za mchezo wa huo utakaokuwa ukianza mwanzo kabla ya kuanza kwa mchezo wa soka.

Timu zilizofungua dimba la mashindano hayo kwa mchezo huo wa Pete { Netball } ni Kitope “A “ wenyeji wa ligi hiyo walopambana na Mabanati wa Kizimbani katika pambano kali na la kusisimua.

Katika mchezo huo mabanati hao wa Kitope A waliweza kuwashinda wapinzani wao Kizimbani kwa kuwachakaza  pete 33 kwa 15.

Hadi wanakwenda mapumziko ya nusu ya pili ya mchezo huo Kitope A Ilikuwa ikiongoza kwa Pete 23 dhidi ya Kizimbani waliopata pete 7 tuu.

Ligi hiyo ya wanawake inashirikisha timu sita ambazo ni Asha Queen,Kitope a, Kitope B, Fujoni, Upenja pamoja na Timu mbili alikwa za Mahonda na Kizimbani.

Hayo ni mashindano ya awamu ya tatu yanayoandaliwa na Jumuiya isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji wa taaluma ya mapambano dhidi ya ubaya wa dawa za kulevya kwa vijana { ZAWEDA }.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.