Habari za Punde

Profesa Lipumba , Maalim Seif wachaguliwa tena Mwenyekiti na Katibu Mkuu CUF, Juma Duni Makamo mwenyekiti


Viongozi wakuu wa CUF wakionyesha mshikamano baada ya kuchaguliwa kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Wa pili kulia ni msimamizi wa uchaguzi huo Awadh Ali Said (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR)
 
Mkutano Mkuu wa CUF Taifa umemchagua tena Katibu Mkuu wa Chama hicho kuendelea na wadhifa huo kwa kupata kura 675, sawa na asilimia 99.5 ya kura zilizopigwa.
 
Mkutano huo pia umemchagua Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa kupata kura 659 sawa na asilimia 95.5 na kumshinda mpinzani wake Chifu Lutalosa Yemba aliyepata kura 30 sawa na asilimia 4 nukta 3.
 
Aidha mkutano huo umemchagua Mhe. Juma Duni Haji kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kupata kura 662 sawa na asilimia 99.25.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumpa tena ridhaa ya kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
 
Wakati wa Kampeni.
 
Mapema akizungumza katika kampeni za kuomba kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif amesema siri ya mafanikio yake kisiasa ni kutokana na kujiamini kwake kuwa kiongozi, kuwa mkweli na kuwa na dhamira njema kwa wananchi.
 
Akijibu hoja za wajumbe wa mkutano huo Maalim Seif amewataka viongozi wa chama hicho kutotangaza kuhudhuria kwa viongozi wa kitaifa kwenye mikutano ya hadhara hadi pale wenyewe watakapothibitisha kuhudhuria, ili kuepusha wananchi kutoamini utendaji wa viongozi hao.
 
Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Juma Duni Haji amesema iwapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atashirikiana na viongozi wengine wa kitaifa pamoja na wananchi kuhakikisha kuwa chama kinapata maendeleo zaidi.
 
Chifu Yemba amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kutetea demokrasia ya kweli ndani ya chama na taifa kwa ujumla.
 
Chifu Yemba ambaye ni mwanasayansi kitaaluma, pia ni Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Shinyanga Mjini.
 
Prof. Lipumba amesema akichaguliwa atahakikisha anatembelea nchi nzima kuimarisha chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
 
Aidha amesema atafanya juhudi za ziada kuona kuwa Tanzania inakuwa na Muungano wa kuheshimiana baina ya pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).
 
Amesema wanawake watapewa nafasi ndani ya kamati tendaji ya chama kuondosha dhana ya mfumo dume  unaodaiwa kuwepo katika ngazi za juu za uongozi.
 
Mgombea mwengine wa nasafi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa M’bezi Adam Bakar, amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kubakia wagombea wawili wa nafasi ya Mwenyekiti.
 
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa kuongoza uchaguzi huo uliosimamiwa na mwanasheria Awadh Ali Said.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.