Na Mwantanga Ame,Pemba
MFUKO wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, ni
fursa mpya inayolenga kuyasaidia makundi
ya wananchi wa kipato cha chini,Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi,
amesema.
Aliyasema hayo jana wakati akizindua
utoaji wa mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, kwa wananchi wa
Pemba, katika uwanja wa skuli ya Micheweni wilaya ya kaskazini Pemba .
Alisema serikali imeamua kuanzisha mfuko
huo kwa dhamira ya kuwasaidia wananchi kuwa na mbinu mbadala za kupambana na umaskini,
hivyo wananchi wazitumie fursa zilizopo.
“Ujasiriamali ni ajira, msifikiri ajira
ni kwenda jeshini, uhamiaji, KMKM, au vikosi vyengine, kuna watu wana ajira
zinaweza kuwaingizia 100,000 kwa siku watu wametajirika kwa kuuza soji za punda
tu, sasa msidharau hili,” alisema.
Alisema kuna benki 10 zinatotoa huduma za
kifedha huku mifuko ya kutoa mikopo ikiwa miwili na SACCOS kubwa sita, jambo
ambalo linaloonesha bado kuna mahitaji ya
wananchi kusaidiwa.
Aidha alisema serikali imeamua kuimarisha
mfuko huo, ambao utakuwa hauna masharti magumu ili kuwawezesha wananchi
kujituma na kujisaidia, kwani ni moja ya mfumo unaofuatwa na baadhi ya mataifa
duniani.
Kwa mfano alisema India, Bagladesh,
Bolivia, Indonesia na Uingereza, zimekuwa na mifuko ya aina hiyo ambayo inawasaidia wananchi wake kupata uwezo wa
kubadili maisha yao .
Alisema kila kijana kuanzia sasa atakuwa na
uwezo kupata fursa hiyo, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa kuhakikisha
anakopa na kulipa madeni yao, kwani mikopo hiyo itakuwa ikitolewa kwa kila
shehia za Zanzibar .
Alisema mfuko huo utakuwa unamilikiwa na
wananchi wenyewe kwenye mauneo yao, jambo ambalo litaweza kuwaletea mafanikio
makubwa katika siku chache zijazo.
Aliwakabidhi wananchi hao hundi ya
shilingi milioni 25, kwa vikundi 13, kwa niaba ya wajasiriamali wa Pemba, ambapo kwa awamu ya kwanza fedha
zilizoidhinishwa ni shilingi 75,650,000 kwa wilaya nne za Pemba .
Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Jamii,
Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Mohammed, aliwataka wananchi waliopewa
mikopo hiyo kuitumia vizuri na kuhakikisha inatimiza malengo yao .
Alisema jumla ya maombi 1,215 yenye
thamani ya shilingi milioni 77.8 yamepokelewa kutoka wilaya 10 za Zanzibar, na
mfuko umekamilisha kupitia maombi 433
wanawake wakiwa 225 na wanaume 167.
Mapema Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Asha
Ali Abdalla, alisema hadi sasa mfuko huo una kiasi cha shilingi 972,140,000
ambazo ni sawa na asilimia 95.
No comments:
Post a Comment