Abu Ammaar
Baadhi ya makosa yanayotokea wakati wa kutoa Zakaatul Fitr
1 Kuitoa
wakati wa Sala ya Idd, siku ya Idd yenyewe.
Zakaatul Firtr hupaswa kutolewa mapema ili
iwafikie walengwa waliokusudiwa. Ikitolewa wakati wa Sala hukosa ile dhamira
iliyokusudiwa ya kuwalisha maskini na wenye kuhitaji na kuwafika kwa wakati.
Ni
Sunna ikatolewa siku moja au mbili kabla ya siku ya Idd. Baadhi ya Maulamaa
wamejuzisha kutolewa hata kabla ya hapo ikiwa itakuwa na manufaa zaidi na
kuweza kuwafika wahusika kwa wakati.
2 Kuisafirisha
kuipeleka sehemu nyengine bila ya dharura
Hasa
ndugu zetu hupenda kupeleka Zakaatul fitr nchi walizotoka au huenda Misikitini
na kuweka katika masanduku yaliyoandikwa Zakaatul Fitr wakidhani tayari
wameshatekeleza wajibu.
Asli ya Zakaatul Fitr ni kutumika sehemu inayotolewa
kama kuna wanaostahiki na wanahitaji. Kama hakuna hapo inajuzu kuisafirisha
kuipeleka sehemu nyingine na huwajibika kwa mwenye kuitoa kwa njia hii
kuhakikisha kwamba aliowapa ni watu thika wanaoaminika na ni kweli wataifikisha
kwa wahusika kabla ya siku ya Idd.
Vyenginevyo
bado mtoaji atakuwa na dhimma kwa Zakaah hii ikiwa haikuwafika walengwa katika muda
unaotakiwa
3 Kutoitoa kabisa
Baadhi
ya ndugu zetu katika dini wanadhani kutoa Zakaatul Fitr si wajibu au si lazima
hiyo wakiitoa sawa na kama hawakuitoa pia ni sawa.
Zakaatul
Fitr ni wajibu kwa kila Muislamu aliyeshuhudia mfungo wa Ramadhaan. Kama
haikutolewa hiyo ni dhambi kubwa na mas’uuliyah (jukumu) kwa mhusika na
atakwenda kuulizwa na Mola wake.
Hutolewa na mwenye kuisimamia familia na huwatolea wote wanaomtegemea katika
familia yake.
4 Kuchanganya kati ya Zakaatul Fitr na
Zakaatul Maal
Baadhi ya ndugu zetu hawaoni tofauti kati ya Zakaah
ya mali na Zakaatul Fitr hivyo hujiweka katika kundi la kwamba hawana sifa ya
kuitoa.
Zakaatul Fitr
ni maalum kwa ajili ya mwezi wa Ramadhaan tu na haina uhusiano kabisa na
Zakaatul Maal isipokuwa ni jina tu ndilo hushirikiana.
Na wanaowajibika kuitoa wana hukumu tofauti na
Zakaah ya mali. Hivyo lazima itolewe bila ya kuihusisha na Zakaah ya mali..
5 Kuitoa na kuwapa pesa wanaostahiki badala ya
chakula
Asli
ya Zakaatul Fitr ni hutolewa chakula kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume Swalla
Allaahu ‘Alayhi Wasallam si pesa. Na kama itatolewa pesa basi walio na dhamana
itawabidi wanunue chakula na kuwapa wanaostahiki kwa siku hii ye Idd ili nao
wawe miongoni mwa walio katika furaha katika siku hii muhimu.
Baadhi
ya Maulamaa wamejuzisha kutolewa pesa ikiwa tu kama itakuwa na manufaa zaidi
kwa wanaohitajia kuliko chakula.
6 Kuwapa Zakaatul Fitr wasiokuwa Waislamu
Moja
ya malengo ya kutolewa Zakaatul Fitr ni kuwalisha maskini na wenye kuhitaji
miongoni mwa Waislamu siku ya Idd. Hivyo Zakaatul Fitr ni maalum kwa masikini
na wanaohitaji miongoni mwa Waislamu tofauti
na sadaka ambayo wanaweza kupewa wasiokuwa Waislamu .
7 Zakaatul Fitr kutumika katika miradi mengine
Baadhi
ya ndugu zetu hutoa Zakaatul Fitr kwa ajili ya kuchangia Msikiti au ujenzi wa
Madrasah, kujenga kisima na kadhalika.
Zakaatul
Fitr haiwezi kutumika katika malengo yasiyokusudiwa hata kama yatakuwa ni ya
kheri kwani dini yetu ina taratibu zake kwa kila kinachotolewa kwa mujibu wa
munasaba wake. Zakaah hii ni kwa ajili ya wanaohitajia
miongoni mwa Waislamu na si vyenginevya na kiwango chake ni kidogo mno ambapo
kila mmoja wetu ana uwezo wa kukitoa.
Na Allaah ndie ajuaye
No comments:
Post a Comment