Habari za Punde

Balozi Seif Akabidhi Cheki kwa Ajili ya Umeme Kisima cha Maji Kirombero

Mbunge wa Jimbo la Kitop[e ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwapongeza wananchi wa Kijiji cha kirombero kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi yanayotarajiwa kupatikana muda si mrefu kijijini hapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu akitoa ufafanuzi kwa wananachi wa Kijiji cha Kilombero Wilaya ya Kaskazini “ B “ juu ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kisima cha maji safi na salama cha kijiji hicho.Ufafanuzi huo aliutoa wakati wa hafla fupi ya Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Sei Ali Iddi kukabidhi  hundi  ya shilingi milioni 14,000,000/- kwa ajili ya uwekwaji wa huduma za umeme katika Kisima hicho.
Balozi Seif akimkabidhi Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Nd. Hassan Ali Hassan Hundi ya shilingi Milioni 14,000,000,/- kwa ajili ya uwekwaji wa huduma za umeme kwenye kisima cha maji cha kijiji cha Kilombero.
Aliyepo kati kati yao ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B “ Nd. Khamis Jabir Makame.(Picha na Hassan Issa wa OMPR)


Na.Othman Khamis Ame
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Nd. Hassan Ali Hassan alisema shirika lake linakusudia kutumia rasilmali ilizonazo katika kuhakikisha huduma za umeme zinapatikana kwenye kisima cha maji cha Kijiji cha Kilombero ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma za maji safi Wananchi wa Kijiji hicho.

Alisema kazi hiyo itakayoanza wakati wowote kuanzia sasa inatarajiwa kukamilika sambamba na ulazwaji wa mabomba ya maji utakaofanya na wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kutoka kwenye kisima hicho hadi maeneo ya wakaazi wa Kijiji hicho.

Nd. Hassan Ali Hassan alitoa kauli hiyo mara baada ya kupokea hundi ya shilingi Milioni 14,000,000/- zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kupitia mfuko wa Jimbo ili kuanza kazi za kukipatia umeme kisima hicho kilichopo ndani ya shamba la ASP mashariki mwa Kijiji cha Kilombero.

Alisema licha ya gharama halisi zinazohitajika katika mradi huo wa umeme zinayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi Milioni 60,000,000/-  ikijumuisha nguzo, waya pamoja na transfoma lakini shirika litajitahidi katika kuona mradi huo unafanikiwa ili umeme upatikane katika kisima hicho.

“ Shirika litakuwa tayari kutumia rasilmali zake kidogo ilizonazo ili kuona mradi huu wa kuwafikishia huduma za umeme wananachi  wa Kilombero kwenye kisima chao unakamilika “. Alifafanua Nd. Hassan.

Meneja Mkuu huyo wa Shirika la Umeme Zanzibar alimpongeza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif kwa jitihada zake anazoendelea kuchukuwa za kukabiliana na kero  zinazowasumbua  wananchi wake hasa zile za huduma za umeme na maji safi na salama.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema kisima hicho tayari kimeshakamilika kwa muda mrefu sasa, lakini kilichobakia ni kusambazwa kwa mabomba kazi itakayochukuwa muda kidogo.


Dr. Garu alisema kisima hicho chenye uwezo mkubwa wa kusambaza huduma ya maji kwa  idadi kubwa ya wananchi kitahitajika  kuwekewa mabomba makubwa yenye upana wa  inchi nne ili kwenda sambamba na kasi ya maji yake.

Alisema hicho ni kisima cha pili kuchimbwa katika eneo hilo la kijiji cha kilombero badala ya kile cha awali ambacho hakikuwa na uwezo kamili wa kutoa huduma itakayotosheleza mahitaji  ya wananchi  hao.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho cha Kilombero Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza wanakiji hao kwa ustahamilivu wao mkubwa wa kukosa huduma za maji safi na salama kwa muda mrefu.

Balozi Seif alisema nia ya uongozi wa jimbo hilo ilikuwa ni kuona wananchi hao wanafaidika na maji kutoka katika kisima hicho ndani ya kipindi hichi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini upungufu wa vifaa vya kukamilishia miundo mbinu ya mradi huo ndio uliochangia tatizo hilo.

Alifahamisha kwamba eneo la kilombero limekuwa likikabiliwa na tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa huduma za maji safi kiasi kwamba wananchi wake hasa akina mama wanatumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo badala ya nguvu zao kuzielekeza katika harakati zao za kimaisha.

Zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na Mbunge  wa jimbo la Kitope Balozi Seif zimetumika kugharamia ujenzi wa kibanda cha kisima hicho kilichochimbwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.