Habari za Punde

DK Shein Ataka Mazingira ya Skuli ya Mpya ya Sekondari Mkanyageni Yaimarishwe Kukamilisha Ujenzi Wake.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                         11 Julai, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha Skuli mpya ya Mkanyageni inakuwa na mazingira mazuri yanayoizunguka pamoja na eneo la kutosha ili kukamilisha mradi mzima wa ujenzi wa skuli hiyo inayotarajiwa kuwa ya Wilaya.
 Agizo hilo amelitoa jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa skuli hiyo huko Mkanyageni Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu kisiwani Pemba iliyoanza Jumanne iliyopita.
 Katika maelezo yake kwa Mhe. Rais, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Abdalla Mzee alisema kuwa baadhi ya huduma katika skuli hiyo ikiwemo kiwanja cha michezo zitakosekana kutokana na uhaba wa eneo la skuli.
Alifafanua kuwa ingawa eneo hilil ni shamba la Ser
ikali lakini wameshindwa kupewa kwa sababu baadhi ya wananchi wamelichukua na kudai ni lao na baadhi tayari wamejenga nyumba za makaazi.
 Kwa hiyo Mhe. Rais aliagiza utaratibu ufanyike kuwasiliana na wananchi waliopo katika eneo hilo ili kufahamu kama wapo kisheria au vinginevyo na kusisitiza kuwa taratibu za umilikaji wa ardhi lazima zizingatiwe na kufuatwa.
 Dk. Shein ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban alisisitiza kuwa skuli hiyo ambayo ni kati ya miradi mikubwa ya aina yake ya ujenzi wa skuli za sekondari Zanzibar ikiwemo ya Kibuteni kisiwani Unguja ujenzi wake lazima ukamilishwe kama ilivyopangwa ili kuipa haiba na hadhi iliyokusudiwa.
 Skuli za sekondari Mkanyageni na Kibuteni zinajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Mendeleo ya Uarabuni(BADEA).

 Sambamba na agizo hilo Mhe. Rais aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwasilisha serikalini taarifa rasmi ya hali halisi ya utekelezaji wa ujenzi wa skuli ya Mkanyageni ambayo kwa mujibu wa maelezo ya Ndg. Abdalla Mzee baadhi ya majengo hayakuweza kujengwa kutokana na uhaba wa fedha.
Mapema katika taarifa yake kuhusu ujenzi wa skuli hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema kuwa baadhi ya majengo katika skuli hayataweza kujengwa kutokana na uhaba wa fedha.
Katika maelezo yake hayo alisema kati ya nyumba 16 za walimu, zimejengwa 8 tu huku dakhalia kwa wanafunzi wa kiume haikujengwa kutokana na sababu hizo hizo.
Halikadhalika uhaba wa fedha umesababisha pia msikiti kutojengwa ingawa zipo dalili za kupata wafadhili wa kujenga msikiti huo.
Kwa hivyo alieleza lengo la skuli hiyo kuwa ya dakhalia kwa wanafunzi wote halitatekelezeka badala yake wanafunzi wa kike tu ndio watakaoishi dakhalia na kwa wanafunzi wa kiume watachaguliwa wale wanaoishi karibu na skuli tu hivyo kutotimiza lengo lililokusudiwa.
Hata hivyo alieleza kuwa majengo yalioyoachwa yanaweza kujengwa katika awamu ya pili kama Serikali itakuwa na fedha.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa wizara yake inakabiliwa na changamoto kubwa katika kukamilisha ramani ya ujenzi wa skuli hiyo upande wa barabara ambazo hazikuwemo katika bajeti ya ujenzi.
Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa skuli hiyo ambao ulianza mwezi Agosti, 2012 na kutarajiwa kumalizika Julai 2013 Ndg. Abdalla Mzee alisema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 78 na inatarajiwa ujenzi utakamilika mwezi wa Disemba mwaka huu.
Alifafanua kuwa kuchelewa kukamilika kwa wakati kulitokana na kucheleweshwa malipo ya mkandarasi kutokana na fedha kuchelewa kutolewa kutoka kwa mfadhili.
Akiwa kisiwani Pemba, Dk. Shein alizindua ununuzi wa karafuu kwa msimu wa 2014/2015 na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ufugaji samaki katika vijiji vya Pujini na Mwambe mkoa Kusini wan Pemba na ujenzi wa barabara za Wete-Gando,Gando-Ukunjwi na Wete –Konde. Mbali ya kukagua miradi hiyo alipata fursa ya kufutarisha wananchi kisiwani humo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.