Habari za Punde

Hotuba ya Balozi Seif uzinduzi wa mpango wa mikopo kwa wastaafu


HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, BALOZI SEIF ALI IDDI ALIYOITOA KATIKA UZINDUZI WA MPANGO WA MIKOPO KWA WASTAAFU KUPITIA BENKI YA POSTA TAREHE 19 JULAI, 2014

 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta,


Mkurugenzi Mwendeshaji, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Zanzibar,

 

Ndugu Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Benki ya Posta,

 

Ndugu Wanahabari,

 

Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

 

Assalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kufika hapa siku hii ya leo tukiwa wazima, hatuna budi kumshukuru Mola wetu kwa ukarimu wake.
Napenda kutoa  shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa kunipa heshima ya kunialika kuwa mgeni rasmi katika hafla hii ya uzinduzi wa mpango wa kutoa mikopo kwa waastafu. Ahsanteni sana, na naahidi kuienzi heshima hii kubwa mliyonipa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
 Aidha, naomba  kuushukuru Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar pamoja na Benki ya Posta kwa kubuni mpango  maalum wa kutoa mikopo kwa wastaafu ili waweze kuishi maisha yenye matumaini.  Uzoefu wa maisha yetu ya kila siku unaonyesha kuwa wastaafu hupata taabu ya kukopeshwa kwa kuwa wanajulikana mapato yao yamepungua, na pale wanapobahatika kukopeshwa hufuatwa siku ile ile wanayolipwa pensheni zao za kila mwezi.  Wakati mwengine matangazo ya radio ya kuitwa wastaafu kwenda kuchukuwa pensheni zao Wizara ya Fedha huleta huzuni kwa wastaafu wadaiwa.
Ndugu Wastaafu,


Mpango huu wa utoaji mikopo kwa wastaafu ambao umeshaanza kutekelezwa una lengo la kuleta faraja na kuwasaidia wastaafu katika kukidhi mahitaji yao ya mbali mbali ya kimaisha. Mikopo inayotolewa huwasaidia wastaafu kulipia gharama za matibabu, ada za shule za watoto au wajukuu zao au kuendesha biashara ndogo ndogo zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya kila siku.
Azma ya Serikali yenu ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga mazingira mazuri kwa wastaafu wake ili kustaafu kusiogopwe na kuonekana ni mwanzo wa kuanza kwa kipindi cha maisha ya shida, yasiyokuwa na matumaini. Tunataka wafanyakazi wetu wanapopata barua za kustaafu wasianze kuhuzunika kama ilivyozoeleka.


Ndugu Wastaafu,
Napenda kutoa wito kwa wale wastaafu wenye sifa za kuomba mikopo hii wajitokeze kwa wingi.  Hii ni fursa muhimu kwenu kujiendeleza kimaisha.  Ni imani yangu kuwa pindipo tutaitumia mikopo hii vizuri tutaishi maisha mazuri pia.  Kuitumia mikopo vizuri maana yake ni kuitumia mikopo kwa shughuli tulizoziombea mikopo hiyo, na siyo vyenginevyo. 
Kwa wastaafu watakaopenda kukopa, ushauri wangu wa bure  mtu akope kwa mujibu wa uwezo wake.  Na akumbuke kuwa mkopo ni lazima kulipwa kwa kupitia pencheni zenu pamoja na asilimia ya riba ambayo Benki imejipangia.  Wadaiwa wote watalazimika kurejesha mikopo hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miaka mitatu kulingana na umri wa mwombaji. Aidha, ni vyema tukajipanga vizuri kabla ya kukopa kwani mkopo sio sadaka.
Mwisho, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwaomba wastaafu watakaochukuwa mikopo kwa kufanya biashara kuhakikisha kuwa biashara wanazotaka kuzifanya wanazielewa vizuri ili kuepukana na hasara.
Kwa mara nyengine tena nawapongeza wale wote waliobuni mpango huu wa kutoa mikopo kwa wastaafu.  Hakika mpango huu ni mkombozi kwa mstaafu na pia utasaidia Taifa letu kupambana na umasikini wa kipato.  Ni matarajio yangu kuona wastaafu wanajitokeza kwa wingi kuchukua mikopo ili kuweza kujiendeleza kimaisha kwa kuwekeza mikopo hiyo kwenye miradi yenye faida nzuri.
Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kuwa Mpango wa Mikopo kwa Wastaafu umezinduliwa rasmi na nyote mnakaribishwa na mtapokelewa kwa mikono miwili.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.