Habari za Punde

DPP: Kutoa majibu ya uongo kwa Kamati za BLW ni kosa la jinai




Na Himid Choko, BLW
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ndugu Ibrahim Mzee Ibrahim  amesema ni kosa la jinai kwa Afisa yeyote wa Umma kutoa majibu ya uongo kwa kamati za Baraza la Wawakilishi.

Amesema Kifungu  cha 22 cha sheria ya Baraza la wawakilishi  Nambari 4 ya mwaka  2007 inayohusu Kinga, uwezo na  Fursa  kinakataza mtu kuidanganya kamati ya Baraza la Wawakilishi  na atakaethibitika kwa makusudi kutenda kosa hilo   ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai.

Ndugu Ibrahim amesema hayo leo wakati akitoa mada inayohusu Wajibu na utekelezaji wa Kazi za makatibu Kamati  huko hoteli  ya Coconut  Tree Village, Marumbi Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema Kamati za  Baraza la Wawakilishi zinauhalali wa Kikatiba na sheria hivyo  si vyema kwa maafisa wa umma kutoa majibu au ushahidi wa uwongo  kwa  kamati hizo.

“ Ni haki ya Wajumbe wa kamati kupata taarifa wazitakazo kutoka kwa maaafisa wa umma (kifungu cha 9 Cha Sheria ) . Maafisa wa Umma hawatakiwi kukataa kutoa ushahidi , hawatakiwi kukataa kuwasilisha nyaraka kwenye kamati , hawatakiwi kukataa kuwasilisha taarifa kwenye Sekretarieti  ya Baraza isipokuwa kama Rais ataelekeza vinginevyo kwa maslahi ya Umma”. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Mashtaka.

Mkurugenzi huyo wa Mashtaka pia ametanabahishwa kwamba ni kosa la jinai kumtisha, na kumuadhibu  mtu aliyetoa ushahidi  kwenye kamati .

Amesema, pia ni kosa kuidharau kamati kwa kukataa wito wa kutoa ushahidi  au kutokuwa na nidhamu na kuzuwia shughuli za kamati hizo.


Amesema Kamati  za Baraza la wawakilishi zinauwezo wa kumuita mtu yeyote kuhudhuria kwenye kamati  na kutoa ushahidi ama nyaraka aliyonayo ikihitajika  katika kazi zake  na kwamba mtu huyo atakuwa na fursa na kinga kama zile anazokuwanazo shahidi anapotoa ushahidi mahakamani.

Hata hivyo amesema mtu anaweza kukataa  kujibu maswali anayoulizwa au kuwasilisha nyaraka  zinazohusu mambo binafsi ya mtu huyo ambayo hayataathiri uchunguzi unaofanywa na Kamati.

Wakati huo huo Mkurugenzi huyo wa mashtaka amesema ni kosa kwa mjumbe au Afisa wa Baraza kutoa au kupokea rushwa  au kufanya vitendi visivyofaa kulingana na hadhi na itifaki zao.

Wakitoa uzowefu wao katika kazi za kamati za baraza ,  Wenyeviti wa kamati za Baraza la Wawakilishi  wamesema  hadhi  ya Baraza inashuka kutokana  na   tatizo kubwa  la utoro na Ucherewaji   pamoja na kukosa uwajibikaji mzuri  kwa baadhi ya   wajumbe  suala ambalo mara nyengine huathiri akidi katika vikao vya Baraza  na kamati zake.

Mwenyekiti  wa Kamati ya Fedha ,  Biashara na Kilimo Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin na Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa  Mheshimiwa Hamza Hassan Juma  wameuomba uongozi wa  Ofisi ya Baraza la Wawakilishi  kufikiria utaratibu wa malipo ya Wajumbe ili kudhibiti  mahudhurio na utoro  katika vikao vya Baraza na kamati zake.

Mapema akifungua mafunzo hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Kificho amewataka Makatibu wa  Kamati kutoa huduma kwa usawa na  kuwa wastahamilivu wakielewa kwamba wanawahudumia  wajumbe  wenye  uzowefu, elimu na  misimamo tofauti .

Amewataka Makatibu hao  kuweka kumbu kumbu za  Mikutano yao vizuri na  kuwashauri vyema wenyeviti wao ili  kuhakikisha kwamba kanuni za baraza la wawakilishi zinafuatwa  ili shughuli za kamati hizo kufanyika kama zilivyokusudiwa.

Kamati za kudumu za Baraza la wawakilishi hivi sasa zinaendelea na kazi zake za kawaida tokea tarehe 10/07/2014 hadi  tarehe 23/07/ 2014 hapa Unguja  na Mkutano ujao wa  Baraza  unategemewa kufanyika Oktoba 22  mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.