Na Said Ameir,Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, amempelekea salamu za pongezi Rais wa India,
Shri Pranab Mukherjee kwa kutimiza miaka 68 ya uhuru wa nchi hiyo.
“Inanipa
furaha kutumia fursa hii adhimu kukutumia wewe binafsi Rais na kupitia kwako
kwa wananchi wa India salamu za pongezi kutoka kwangu na kutoka kwa wananchi wa
Zanzibar kwa kusherehekea miaka 68 ya uhuru wa
nchi yenu ,” salamu hizo zimeeleza.
Katika salamu hizo Dk. Shein amebainisha
kuwa wananchi wa Zanzibar wanajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri na wa
kihistoria uliopo kati yao na wananchi wa India na kwamba azma yao ni kuona
uhusiano na ushirikiano huo unazidi kuimarika siku hadi siku.
Aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar wanafarijika kuona India imepiga hatua kubwa
kimaendeleo katika kipindi cha miaka 68 ya uhuru wake na kwamba maendeleo hayo yamekuwa yakiwanufaisha
wananchi katika mataifa mengine.
“Kwa hiyo ninachukua fursa hii kuwasalimu
ndugu zetu wa India katika siku hii muhimu na adhimu na kuwatakia maendeleo
zaidi siku zijazo huku tukitarajia kuongeza kasi ya ushirikiano kati ya nchi
zetu na watu wake,” alisema.
Wakati huo huo Dk. Shein, amemtumia salamu za
pongezi Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kwa kuadhimisha miaka 68 ya uhuru
wa India .
Katika salamu zake hizo Dk. Shein alisema
yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wanayo
furaha kuungana na Narendra na ndugu zao wananchi wa India katika kusherehekea siku ya
uhuru wa nchi hiyo.
Alitumia fursa hiyo kumtakia afya njema
na maisha marefu Waziri Mkuu huyo.
No comments:
Post a Comment