Na Farida Msengwa,Morogoro
WACHUNGAJI wa jamii ya kisukuma wamepigwa
marufuku kutembea mitaani na fimbo
kutokana na baadhi yao
kuzitumia vibaya kwa michezo ambayo wakati mwingine husababisha mauaji.
Onyo hilo limetolewa na Ofisa tarafa wa
Ngoheranga,Conrad Mzwalandili, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa
vijiji vya Ngoheranga na Ihowanja wilayani Ulanga na kusema kwamba wamefikia
hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu athari ya fimbo
pamoja na ngoma.
Alisema imebainika baadhi ya vijana huchapana
hadi kusababisha mauaji na tayari zaidi ya fimbo sabini zimekamatwa, huku
akiwataka wananchi wa eneo hilo kutembea kwa kujiamini katika Tanzania huru,
badala ya kutumia fimbo ambazo zimegeuka silaha.
Alisema wamepiga marufuku ngoma aina ya
sagulaga, ambayo imekuwa ikiwadhalilisha mabinti wakiwemo wanafunzi,ambao
vijana hata zaidi ya 100 humkimbiza binti bila kujali ni mwanafunzi ama
vinginevyo na kumfanyia matendo yasiyo faa.
Awali wananchi wa kijiji cha Ihowanja,
Luminicu Ngonyani, Anastasius Ngaliwa na Frank Kufakwenda katika mkutano wa
hadhara, waliilalamikia serikali ya kijiji chao kugawa maeneo ya ardhi kiholela kwa wageni kutoka
nje, huku fedha zinazopatikana wakiwa hawajui matumizi yake.
Hata hivyo , Mwenyekiti wa kijiji cha
Ihowanja, Yonas Ngonyani, alisema wanaolalamikia kwa kufanya matumizi mabaya
ya fedha za kijiji wengi ni kutoka vyama vya upinzani ambao wamekuwa
wakiwashawishi wananchi kushiriki kazi za kujitolea kwa maendeleo yao .
No comments:
Post a Comment