Na Fatma Kassim, Maelezo
HOSPITALI ya Kivunge iliyopo Mkoa wa
Kaskazini Unguja inakabiliwa na tatizo la usafiri wa wajawazito na wagonjwa
wengine wanaohitaji huduma hiyo.
Wanaoathiriwa zaidi na tatizo hilo ni wale wanaopewa
rufaa ya kwenda Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu zaidi.
Daktari Dhamana wa Hospitali ya Kivunge,
Dk. Shau Ali Hamdan alisema hospitali
hiyo ina gari moja tu la kubebea wagonjwa ambalo hata hivyo linatumiwa kwa
shughuli nyengine za kiofisi.
“Ni usmbufu mkubwa kwani linapotakiwa
kubeba wagonjwa linakuwa katika shughuli zingine za ofisi na linapotakiwa kwa
shughuli za ofisi linakuwa katika shughuli ya kubeba wagonjwa,” alisema na
kulitaja gari hilo
kuwa ni Ambulance.
Alisema pamoja na uwepo wa gari hilo , Dk Hamdan alisema wanakabiliwa na tatizo la mafuta
ya kuendeshea gari hilo
na inapotokezea mgonjwa kupatiwa rufaa, inamlazimu kuchangia shilingi 30, 000 kwa ajili ya mafuta.
Alisema Wizara ya Afya imepanga kuwapatia
lita 400 za mafuta kila mwezi lakini
hupatiwa chini ya kiwango hicho jambo linalokwamisha utekelezaji wa majukumu yao .
Gari hiyo imetolewa kwa msaada wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB) mwaka 2009 kwa ajili ya kuwahudumia wajawazito
wanaopatiwa rufaa kupelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Dk. Hamdan alisema hospitali ya Kivunge inategemewa na wakaazi wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja wakiwemo wale wanaotoka mbali kama
kisiwa cha Tumbatu, Kijijini Matemwe na sehemu nyengine.
Uwezo wa hospitali hiyo inapokea wastani
wa wagonjwa 150 kwa siku, na wajawazito
wanaohudumiwa kila mwezi wastani wa 250 na wanaopewa rufaa ni 22 kwa mwezi.
“Kuna baadhi ya wajawazito wanakuja moja kwa moja kujifungua
hapa, lakini, wengine wanakuwa weshacheleweshwa, wengine wanakuja kwa kupatiwa rufaa na mara nyingi akifika hali ishakuwa mbaya, inabidi
sisi tumpatie rufaa kwa kumuwahishia Mnazimmoja na hapo inabidi mgonjwa achangie mafuta”,
alifahamisha Dk. Shau.
Wajawazito na wagonjwa wengine wanapopta
rufaa kupelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja
wanapokosa usafiri hospitalini huwa wanatumia gari za kukodi ambazo
hulazimika kulipia zaidi ya 30,000.
Dk. Hamdan alisema kutokana na hali hiyo,
lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi litakuwa gumu kufikiwa iwapo
mamlaka husika haitojipanga ipasavyo katika kuzipa kipaumbele huduma za mama
wakati wa ujauzito wake, anapojifungua na baada ya kujifungua.
Wastani wa vifo vya wajawazito
vinavyotokea kwa kila mwaka ni vinne katika hospitali hiyo.
Mkakati wa Kupunguza Umasikini Zanzibar
(MKUZA), umelenga kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 473 mwaka 2007 hadi
vifo 170 kwa kila vizazi hai 100,000
ifikapo mwaka 2015.
Malengo ya Millenia namba tano ni kupunguza vifo vya uzazi kutoka 473 mwaka 2007 hadi 170 kwa kila
vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2015.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk.
Mohammed Saleh Jidawi, alisema, nia ya Wizara hiyo ni kutekeleza mikakati ya
kuimarisha huduma za wajawazito katika hospitali pamoja na vituo vya afya huku
wajawazito wakitakiwa kutochangia huduma
wakati wa kujifungua.
No comments:
Post a Comment