Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba waathirika
wa mafuriko ya kiasi cha miaka minne iliyopita mjini Kilosa.
Alitoa agizo hilo wakati akizungumza
na wananchi wa Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada
ya kutembelea wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Alirejea mkoani Morogoro
kuendelea na ziara yake ya siku saba baada ya kuikatisha Jumamosi, kwenda
kwenye Chuo cha Uongozi wa Kijeshi, Monduli, mkoani Arusha, ambako alitoa kamisheni kwa maofisa wapya wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa
maneno na kwa mabango na waathirika hao
kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa
wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea
kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa miaka minne iliyopita, Rais Kikwete alisema:
“Ni jambo la kusikitisha kuwa
bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja
kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kujenga nyumba za
kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la
kwanza,”alisema.
Baada ya kuambiwa kuwa
vimepimwa viwanja 800 katika halmashauri hiyo, aliamuru kuwa kiasi cha viwanja
400 vitengwe kwa ajili ya waathirika hao wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja,
yaani kuanzia Jumatatu hadi a Ijumaa, nataka taratibu zote ziwe zimekamilika na
kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazingumzia habari ya ujenzi
baadaye,” alisema.
Mapema asubuhi, ameweka jiwe la
msingi la ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika eneo la Msolwa, wilaya ya
Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda Matakatifu ya
Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo lilianza
shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini
Hydropower Project unajengwa kwenye
milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na
2.3 kwa ajili ya mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo skuli maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St.
Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao unagharimu shilingi
bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli,
utawezesha skuli ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za
vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na
utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza
tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao
utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia
mradi wa umeme vijiji (REA) na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa
ajili ya ujenzi wa mradi.
No comments:
Post a Comment