Na Kija Elias, Moshi
TAASISI ya Kuzuia na Kumbana na
Rushwa (TAKUKURU), imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 38.96, kupitia operesheni
mbali mbali na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, iliyotekelezwa na
serikali katika kipindi cha mwezi Julai,2013
hadi Juni 2014.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hosea,aliyasema
hayo jana alipokuwa akitoa maelezo ya kazi za taasisi yake kwa kipindi hicho
kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa siku tatu wa wakuu wa TAKUKURU,
unaofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema taasisi hiyo imeweza
kuokoa kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 33.59, ikilinganishwa
na fedha zilizookolewa mwaka 2013.
Alisema katika uchunguzi wa
taasisi hiyo, imefanikiwa kufungua kesi mpya 327, pamoja na kesi kubwa tatu
zinazowahusu viongozi wa serikali, ambao wamebainika kujihusisha na vitendo vya
rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Alisema kazi
hiyo ni juhudi ambazo zimefanywa na taasisi hiyo, ambayo hivi sasa
imepiga hatua kubwa ya kiutendaji ikilinganishwa na taasisi kama hiyo kwa nchi nyingi
za Afrika.
Akielezea mpango wa elimu kwa umma unaolenga kudhibiti
rushwa, alisema hadi sasa taasisi hiyo imeweka mkazo kwenye ufunguzi wa klabu za
wapinga rushwa katika skuli za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu.
Aliongeza kuwa hadi sasa
taasisi hiyo ina jumla ya klabu 2,371 katika skuli za msingi kote nchini, zenye jumla ya
wanachama 172,706, ambapo kwa upande wa
skuli za sekondari zipo jumla ya klabu 4,016
zenye wanachama 270,422 na klabu 85 katika vyuo na taasisi za elimu ya juu
zenye wanachama 9,643.
Awali akifungua mkutano huo, Mkuu
wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliitaka TAKUKURU kuongeza juhudi za kuwabana
watumishi wa umma, wanaolalamikiwa kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.
Alisema muundo wa taasisi hiyo
unatakiwa kufikisha huduma zake kuanzia ngazi za wilaya,ili kuwasaidia wananchi
kuwatatulia matatizo ya rushwa, ambayo yanafanywa na baadhi ya wachache.
Alisema rushwa imekuwa tishio katika baadhi ya maeneo
na kuitaka taasisi hiyo, kuhakikisha inaanza kuwabana viongozi wa kisiasa
wanaohusika kutoa rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu
mwakani.
Mkutano huo wa siku tatu, umewakutanisha
Wakurugenzi wa idara mbali mbali za taasisi hiyo, maofisa wa TAKUKURU ngazi ya
mkoa na wilaya zote nchini, wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama
mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment