Na Fatma Kitima, Dar es Salaam
WAKATI msuguano kuhusu uraia pacha
ukiendelea katika bunge maalum la katika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, amesema suala hilo ni muhimu lakini serikali haina mamlaka
ya kulazimisha.
Hata hivyo, alisema suala hilo limewekwa ndani ya rasimu
ya katiba mpya kukujadiliwa.
Lakini kutokana na umhimu huo ,Serikali
ya Muungano na Zanzibar
zitaendelea kutoa ushirikiano na kulishughulikia kwa umakini zaidi ili kuondoa
changamoto zilizopo.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika
hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza katika mkutano wa
siku mbili, uliowakutanisha wanadiaspora wanaoishi ndani na nje ya nchi wenye lengo
la kujadili na kubadilishana mawazo pamoja na kuangalia changamoto
zinazowakabili huko ughaibuni.
Aidha alitoa wito kwa Watanzania
wanaoishi nje ya nchi,kutumia fursa
walizonazo kuwekeza na kuwashawishi wawekezaji wa kigeni kuja Tanzania ili
kukuza uchumi wa taifa.
Aliwakumbusha kuthamini nchi yao na kuzisaidia familia zao kwa kuzitembelea mara kwa
mara badala ya kuishia mijini wakati wanapofika nchini Tanzania na kutojua
mazingira na utamaduni wa kwao hali inayodhihirisha kwamba wamezitenga familia
zao.
Alisisitiza kutoa msaada wa kuwaendeleza
ndugu zao kielimu ili kujikwamua na umaskini na baadae familia ziwe mabalozi wa
kueneza elimu na chachu ya maendeleo kiuchumi.
“Natoa wito kwa wanadiaspora wote mtumie
fursa hii na uelewa wenu kuwashawishi watu na makampuni yenye uwezo na nguvu ya
kuwekeza hapa nchini kwani hakuna nchi yeyote inayokua kiuchumi bila uwekezaji
wa ndani au nje nchi,” alisema.
Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo,
walitoa ahadi kwa serikali kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha na kuangalia
maeneo ya uwekezaji ndani ya nchi kwa kuwashawishi wawekezaji kuwekeza nchini
ili kupanua uchumi na kupunguza
umaskini.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa mawasiliano
Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema katiba haimruhusu Rais kulivunja au
kuliahirisha bunge la katiba.
Alisema
wapinzani lazima waende kusoma tena sheria ya mabadiliko ya katiba kwa undani
na watajiridhisha kuwa Rais hana ubavu wowote kisheria kuahirisha wala
kulivunja bunge la katiba linaloendelea sasa.
Aliwataka pia wapinzani kama wana hoja
yoyote kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi, ili kusaidia upatikanaji wa
katiba mpya lakini wasitarajie kusimamishwa kwa mchakato kwani ni kinyume cha
sheria.
Kuhusu maandamano, alsiema hayatakuwa na
msaada wowote kupata katiba mpya zaidi ya kuleta vurugu.
No comments:
Post a Comment