Na Fatuma Kitima, Dar es Salaam
JUKWAA la Katiba Tanzania
(JUKITA), limesema tatizo la mahudhurio katika Bunge Maalum la Katiba,
limesababisha baadhi ya kamati za Bunge kuchelewa kuanza kazi au kushindwa
kuendelea na kazi.
Hali hiyo imesababisha kamati
hizo kuishia kuendesha semina zisizotarajiwa ili kuhalalisha matumizi ya fedha
za wavuja jasho wa Tanzania.
Waraka wa JUKITA uliosainiwa na
Kaimu Mwenyekiti, Hebron Mwakagenda, imesema taarifa hizo zimepatikana kufuatia
ufuatiliaji uliofanywa kuanzia Agosti 11 hadi 23 mwaka huu.
Aidha Jukwaa hilo limesema Bunge la Katiba limetaja kuwa juma la wajumbe
441 walihudhuria vikao vya bunge, lakini uchunguzi umebaini wajumbe hao ni wale
wote ambao waliwahi kufika na kusaini kitabu cha mahudhurio na wengi wao
takribani wajumbe 100 waligundulika hawapo bungeni, wakiwemo mawaziri wa
serikali zote mbili.
Taarifa hiyo imesema pamoja na
ofisi ya Katibu wa Bunge Maalum kuonesha imebana mianya kwa wajumbe ambao
husaini na kutofanya kazi, lakini fedha zimeendelea kuvuja kwa kutumia mianya
mengine ikiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri ambao hutoa taarifa za
kutohudhuria bungeni kwa Waziri Mkuu
kutokana na shughuli nyingine za
kiserikali.
Alisema hali hiyo inasababisha
viongozi hao kulipwa posho mara mbili; kutoka bunge la katiba na kule
wanakokwenda kutekeleza majukumu mengine.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
tayari shilingi bilioni 6.3 zimeshatumika mpaka kufikia Agosti 23 mwaka huu.
Kuhusu rais kutokuwa na uwezo
wa kusitisha bunge la katiba, taarifa ilisema wasaidizi wake wanajaribu kutumia
jina la Rais
kwa manufaa yao.
Imesema pamoja na kwamba rais
hakuwa na mamlaka ta kuanzisha mchakato wa kuandika katiba kisheria mwaka 2010,
lakini aliuanzisha kupitia upenyo wa kisiasa kwa kuwa yeye ni
kiongozi mkuu wa
nchi.
Hivyo, imesema JUKATA inaamini
Rais hawezi kuacha mambo yaharibike na kukaa kimya kwa sababu tu kisheria hana
mamkalaka.
Kuhusu kupatikana theluthi
mbili (2/3) hasa kutoka Zanzibar ili kupitisha katiba mpya, Jukwaa hilo
limesema hoja sio idadi ya kura au wajumbe, bali ni maridhiano ya kitaifa na
kwamba kama haiwezekani kupata kupatikana hakuna sababu ya kufuja fedha
za
walipa kodi maskini ambazo zingefanya mambo mengine.
Jukwaa hilo pia limesema
kitendo kinachofanywa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta na
Makamu wake, Samia Suluhu Hassan cha kupokea maoni mapya, ni kunyume na sheria
ya mabadiliko ya katiba kifungu 9(1) ambacho kinaeleza kazi za tume ambazo ni
kukusanya, kuchambua, kuandika na kuwasilisha kwenye bunge maalum la katiba na
kwamba kazi ya bunge ni kupitisha katiba.
No comments:
Post a Comment