Na Khamis Amani
KESI inayowakabili Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Hamdani Oamar Makame na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI)
Salum Msangi, waliofunguliwa mashtaka na ndugu wa watu wanane kwa kuwashikilia
kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani, limepigwa kalenda hadi Agosti 19 mwaka huu.
Kesi hiyo inasikiliwa na Jaji wa mahakama
kuu Zanzibar, Mkusa Issack Sepetu.
Naibu Mrajisi wa mahakama kuu, Yessaya
Kayange, aliiahirisha kesi hiyo jana baada ya Jaji anaeisikiliza kutofika mahakamani
na sasa itafikishwa tena mahakamani Agosti 19 kwa ajili ya kutajwa.
Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo na
familia ya watu hao kupitia Wakili wa kujitegemea Abdallah Juma na Rajab
Abdalla kutoka Kampuni ya AJM & Solicitor Chamber ili kuielezea mahakama
mahali walipo ndugu zao.
Hatua hiyo imekuja baada ya jamaa hao wa
karibu wa watu hao kuwatafuta kwa muda mrefu bila ya matumaini ya kuwaona licha
ya jeshi la polisi kukiri kuwashikilia.
Watu hao walikamatwa katika maeneo
tafauti ya mji wa Zanzibar
na jamaa hao hawawajui mahali walipo licha ya juhudi za kuwasaka maeneo tafauti
ikiwemo na vituo vya polisi kushindikana.
Kutokana na hali hiyo, jamaa hao walilazimika
kuwafikisha mahakamani maofisa hao wakuu wa polisi ili kuelezea mahali walipo.
Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilianza
kusikilizwa Julai 21 lakini upande wa polisi ulikiri kwamba unawashikilia na
wameshafikishwa mahamani Kisutu.
Hata hivyo, siku nyengine iliyopangiwa
kusikilizwa Julai 24, Jaji Mkusa aliifuta kwa kuwa hati ya kiapo haikuwa na
saini ya Mrajisi.
Hata hivyo, upande wa walalamikaji
hawakuridhika na uamuzi wa mahakama kuu na kuamua kuirejesha tena kesi hiyo
mahakamani Agositi 11.
Watu hao waliodaiwa kukamatwa ni Nassor
Ahmad Abdallah, Mohammed Is-haq Yussuf, Said Kassim Ali, Hassan Bakari
Suleiman, Rashid Ali Nyange, Antar Humoud, Khamis Salum Amour pamoja na Salum
Ali Salum.
No comments:
Post a Comment