Habari za Punde

Kesi ya ugaidi haijavunja Katiba ya Zanzibar

 
na Mwinyi Sadallah
 
Zanzibar. Mahakama Kuu ya Zanzibar imesema mashtaka ya ugaidi yanaweza kufunguliwa katika mahakama yoyote baina ya pande mbili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama ilivyotokea kwa Wazanzibari 14 waliokamatwa Zanzibar na kufunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara.
Akitoa uamuzi katika kesi ya maombi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa Polisi Zanzibar na washtakiwa hao 14 wanaopinga kukamatwa Zanzibar na kufunguliwa mashtaka Tanzania Bara, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu alisema hakuna sheria wala Katiba iliyovunjwa.
Jaji Sepetu alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama Kuu imejiridhisha kuwa Sheria ya Ugaidi Namba 2 ya mwaka 2002, iliyotumika kuwafungulia mashtaka inatoa uwezo wa kukamata na kufungua mashtaka katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jaji Sepetu alisema ombi la Wazanzibari hao la kuitaka Mahakakama Kuu ya Zanzibar itoe amri kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaachia huru watuhumiwa hao ni sawa na kuingilia uhuru wa mahakama nyingine iliyopo katika upande mmoja wa Muungano ambayo inatakiwa ifanye kazi bila ya kuingiliwa na upande mwingine.
 
Jaji Sepetu alisema ombi lililofunguliwa na walalamikaji halina nguvu za kisheria kwa vile limefunguliwa nje ya wakati huku watuhumiwa wakiwa wamefikishwa mahakamani siku tisa kabla Wazanzibari hao kuwasilisha maombi yao Mahakama Kuu ya Zanzibar ya kupinga kushtakiwa Tanzania Bara.
Jaji huyo alisema Mkurugenzi wa Mashtaka wa Tanzania (DPP) aliwafikisha watuhumiwa mahakamani mnamo Julai 17 wakati maombi ya Wazanzibari hao ya kupinga kukamatwa na kufunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara yalifunguliwa Julai 28, mwaka huu.

“Kama waombaji wanapinga uamuzi huu, wanaweza kufungua maombi yao katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga wateja wao kushtakiwa upande wa pili wa Muungano,” alisema Jaji Sepetu.

Vilevile, alisema Mahakama Kuu ya Zanzibar haina mamlaka wala uwezo wa kuchukua hatua ya kuingilia uhuru wa mahakama nyingine hasa kwa kuzingatia watuhumiwa hao hawapo tena mikononi mwa Polisi, wapo ndani kwa amri ya Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu na kushikiliwa katika Gereza la Segerea.

Hata hivyo, Jaji Sepetu alilitaka Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na taratibu ili kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima hususan suala la ukamataji na kuepuka kukaa na watuhumiwa nje ya wakati kwa mujibu wa sheria bila ya kuwafikisha mahakamani.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo, Wakili Abdallah Juma alisema wateja wake walikamatwa na kufunguliwa mashtaka kinyume na Kifungu cha 56 a(1)(3) kinachotoa mamlaka pekee kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar kufungua na kushughulikia mashtaka yoyote ya jinai dhidi ya mtu yeyote mbele ya mahakama yoyote isipokuwa ya kijeshi.

Alisema kitendo cha kuwakamata na kutowafikisha katika Mahakama za Zanzibar ndani ya saa 24, kilivunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Kifungu cha 14(1) na 16(1) vinavyotoa uhuru wa kila mtu kuwa na haki ya hifadhi ya maisha yake na kutonyimwa uhuru wake wa kwenda popote, haki ya kuishi katika sehemu yoyote ya Zanzibar.

Wazanzibari hao 14 walifunguliwa mashtaka ya kula njama za ugaidi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na Kifungu cha 21 cha Sheria ya Ugaidi cha Sheria Namba 2 ya mwaka 2002.

Chanzo: Mwananchi
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.