Na Khamis Amani
WAZIRI wa zamani katika Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mansoor Yussuf Himid, ameachiwa kwa dhamana na
Mahakama Kuu ya Zanzibar .
Mansoor
ambae alikuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembe Samaki kabla ya kufukuzwa na
CCM, alikaa kizuizini kwa muda wa siku
14 kutokana na kukabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kupatikana na silaha katika mahakama ya mkoa
Vuga.
Jaji wa Mahakama Kuu, Abraham Mwampashi,
alimpatia dhamana mshitakiwa huyo baada ya kunyimwa na mahakama ya mkoa Vuga,
chini ya hakimu Khamis Ramadhan Abdalla alipofikishwa kwa mara ya kwanza.
Masharti yaliyotolewa na mahakama kuu ni
kuwa na wadhamini wawili wenye kuaminika na kukubalika vizuri ambao kila mmoja
atasaini bondi ya shilingi milioni tano.
Kabla ya kutoa maamuzi hayo, Jaji
Mwampashi alitupilia mbali hoja za upande wa mashtaka kwamba shitaka
linalomkabili halina dhamana kwa kusema kwa mujibu wa sheria, hakuna shitaka
lolote lisilokuwa na dhamana na wala mtu kukutwa na silaha sio hatari.
Mansoor
aliwasilisha ombi la kupatiwa dhamana chini ya kifungu cha 150 (4) cha sheria
za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7 ya 2204 sheria za Zanzibar .
Masharti mengine ni fedha taslimu
shilingi milioni tatu, kuwasilisha mahakamani hati ya kusafiria pamoja na
kumtaka kutoondoka nchini bila ya idhini ya mahakama.
Alisema kauli hizo (mashtaka yasio na
dhamana) zitahitajika kuangaliwa ni wapi zinatumika kwani mahakama za mwanzo
hadi mkoa ndizo zisizopaswa kutoa dhamana kwa makosa yaliyoainishwa katika
kifungu cha 150 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria
za Zanzibar .
Alisema Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka
ya kutoa dhamana kwa makosa yaliyoainishwa katika kifungu hicho kwa mujibu wa kifungu
kidogo cha nne (4) cha sheria hiyo.
Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka, Raya Issa Mselem, aliiomba mahakama kukizingatia
kifungu kidogo cha kwanza, kutokana na kwamba tayari kuna watu kadhaa
wanashikiwa kwa sheria jambo ambalo Jaji Mwampashi hakukubaliana nalo.
Kutokana na kauli hiyo, Jaji Mwampashi
alisikitika kuona watu hawaitumii sheria hiyo ambapo sio kila mtu anaweza kunyimwa
dhamana bali kuna wengine wanahitajika kupatiwa kutokana na vigezo mbali mbali,
na kuomba watu wakitumie kifungu hicho ili waweze kupata haki zao za kikatiba.
Akipingana na hoja za upande wa wapingaji
dhamana, (DPP) kuhusu hatari ya muombaji huyo ya kukutwa na silaha, Jaji
Mwampashi alisema kukutwa na silaha si hatari bali hatari ipo katika matumizi ya
silaha.
Alisema, upande wa wapingaji umeshindwa
kuonesha hatari ya muombaji ya kumiliki silaha ambayo alikamatwa nayo nyumbani
kwake baada ya upekuzi na wala hawakuonesha madhara aliyoyafanya ya kuitumia
silaha hiyo kinyume cha sheria.
Pamoja na mambo mengine Jaji Mwampashi
alisema, muombaji ni mtu anaejulikana na kufahamika ambae ni mdau mkubwa wa
serikali katika harakati za maendeleo za ulipaji wa kodi kutokana na biashara
zake anazozifanya.
Alisema, kukaa kwake kizuizini ni
kuikosesha serikali mapato pamoja na kuitia hasara kutokana kuwepo kwake
rumande kutakuwa ni mzigo kwa serikali wa kumtunza pamoja na gharama za usafiri
wa kwenda na kurudi mahakamani na ilhali ni mtu mwenye shuguli zake ambazo
zinatoa ajira kwa vijana.
Hivyo Jaji Mwampashi, alilazimika
kumpatia muombaji huyo masharti hayo ya dhamana ambayo aliweza kuyatekeleza
baada ya mahakama ya mkoa kutakiwa kuyasimamia.
Wakati huo huo, mahakama ya mkoa Vuga
mara baada ya kumwachilia mshitakiwa huyo kwa masharti hayo ya dhamana,
mahakama hiyo iliyo chini ya hakimu Khamis Ramadhani Abdallah ameiahirisha kesi
hiyo hadi Agosti 28 mwaka huu kwa kutajwa kutokana na upelelezi wake bado
haujakamilika.
Mansoor aliwasili mahakamani hapo akiwa
chini ya ulinzi wa jeshi la polisi akitokea rumande ili kuendelea na kesi inayomkabili
ambayo kwa mara ya kwanza ilifikishwa mahakamani hapo tokea Agosti 5 mwaka huu
na kusomewa mashitaka ya kupatikana na sialaha, risasi na marisau kinyume cha
sheria mashitaka ambayo aliyakana.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliongozwa
na Wakili wa serikali Maulid Ame Mohammed na Khamis Juma Khamis na upande wa
utetezi ulisimamiwa na Wakili wa kujitegemea Gaspar Nyika na Omar Said
Shaabani.
Nje ya mahakama Mansoor alionekana
akitembea barabarani huku akilakiwa na mkewe pamoja na ndugu, jamaa na marafiki
kwa kumfariji na baadae aliondoka katika viunga vya mahakama majira ya saa 7:28
za mchana akiwa ndani ya gari aina ya PRADO yenye nambari za usajili Z 103 AE.
No comments:
Post a Comment