Wananchi wakiwa wameubeba mwili wa Mwandishi Mkongwe Zanzibar Marehemu Juma Masoud, aliefariki jana hafla katika hospitalim Kuu ya Mnazi mmoja, Marehemu amefanyakazi Redio Zanzibar, Gazeti la Nuru na kumalizia ajira yake katika gazeti la Serekali la Zanzibar Leo,
Mhariri Mkuu (mstaafu) wa
Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, linalochapisha magazeti ya Zanzibar
Leo, Zanzibar Leo Jumapili na Zaspoti, Juma Massoud Ali, amefariki dunia akiwa
na umri wa miaka 61.
Alifariki alfajiri ya kuamkia
jana katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja
kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa sukari na shinikizo la damu.
Marehemu alizikwa jana kijijini
kwao Bambi wilaya ya Kati Unguja,ambapo mazishi yake yalihudhuria na maelfu ya
wananchi, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wafanyakazi wenzake wa zamani.
Marehemu alianza kufanya kazi
katika vyombo vya habari kuanzia mwaka 1975 katika chumba cha habari cha kituo cha redio Zanzibar (sasa ZBC redio) akiwa kama mwandishi
wa habari.
Mwaka 1976, alijiunga na Chuo
cha Uandishi wa Habari (TSJ) mpaka mwaka 1979 na kutunukiwa Diploma ya uandishi
wa habari.
Baada ya kurudi kituo chake cha
kazi, kuanzia mwaka 1994-1998 alifanya kazi magazeti ya Uhuru na Mzalendo
akitokea gazeti la Nuru aliloanza nalo mwaka 1992.
Baada ya kumaliza mkataba na
magazeti ya Uhuru na Mzalendo alirejea kulitumikia gazeti la Nuru na alikuwa
miongoni mwa waandishi wa habari wa kwanza walioanzisha gazeti la kila siku la
serikali la Zanzibar Leo mwaka 2002, Mhariri Mwandamizi.
Aliendelea kupanda cheo na
baada ya kuanzishwa Shirika la Magazeti ya Serikali chini ya sheria namba 11 ya
mwaka 2008, aliteuliwa kuwa Mhariri Mkuu, cheo ambacho aliendelea kukishikilia
hadi alipostaafu Septemba 1, mwaka 2013.
Marehemu ameacha kizuka mmoja
na watoto saba.
Mungu ailaze roho ya marehemu
mahala pema peponi, Amiin.
Xxxxxxxxxxx
Wanasheria:Kamishna wa Polisi
Z’bar anavunja Katiba
Wanadi amepora mamlaka ya DDP
Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Wanasheria Zanzibar
(ZLS) kimesema kitendo kinachofanywa na Kamishna wa Polisi Zanzibar cha
kuwakamata watuhumiwa, kuwasafirisha na kuwafungulia mashtaka nje ya Zanzibar,
kimepora mamlaka na madaraka ya kikatiba
aliyokabidhiwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar.
Aidha kitendo cha polisi
kukabidhi washtakiwa kwa mamlaka zilizo nje ya Zanzibar ni kumdharau na
kumkiuka Mkurugenzi wa Mashtaka.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana, Rais wa Chama hicho, Awadh Ali Said, alisema hali hiyo
imesababisha watuhumiwa kukosa haki zao jambo ambalo ni uvunjifu mkubwa wa haki
za binaadamu hasa ikizingatiwa kwamba
watuhumiwa hao wamekuwa wakiteswa kudhalilishwa kulikovuka viwango vya
ubinaadamu, madai ambayo hayakukanushwa na mamlaka husika.
Alisema chama hicho kinalaani
uvunjaji wa katiba ya Zanzibar na ukiukwaji mkubwa wa sheria za usimamizi na
uendeshaji wa makosa ya jinai Zanzibar na vitendo vya udhalilishaji
wanavyofanyiwa watuhumiwa.
Alisema masuala ya jinai,
sheria zake, usimamizi na uendeshaji
wake sio mambo ya Muungano na ndio maana Zanzibar na Tanzania Bara kila moja
ina sheria tofauti zinazosimamia utaratibu wa mwenendo wa makosa ya jinai.
Aidha alisema pande hizo mbili
zina sheria za ushahidi tofauti na ndio maana zina taasisi tofauti
zinazosimamia mambo ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai.
Alisema pamoja na Tanzania kuwa
na jeshi moja la polisi, jeshi hilo kwa upande wa Zanzibar linasimamia sheria
za Zanzibar na upande wa Tanzania Bara linasimamia sheria za huko.
“Na hata pale mtuhumiwa
anapotuhumiwa kuvunja sheria ambayo inahusu mambo ya kimuungano, bado sheria
zinazotumika kuendesha mashtaka hayo ni za Zanzibar kupitia taasisi za
Zanzibar- hili limefanyiwa maamuzi kadhaa na mahakama ya Rufaa Tanzania,”
alisema.
Alisema kwa upande wa Zanzibar,
sheria ziko wazi kwamba jukumu la polisi ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa wa
uhalifu kufanya upelelezi wa makosa ya jinai na baadae kuwasilisha ushahidi kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar ambaye kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ndie
pekee aliyepewa mamlaka ya kuendesha mashtaka katika mahakama za Zanzibar.
“Katiba ya Zanzibar haijatoa
mwanya wowote kwa Mzanzibari anayetuhumiwa na makosa ya jinai kukamatwa na
kusafirishwa nje ya Zanzibar na kumkabidhi kwa mamlaka nyenginezo ambazo hazikuidhinishwa
na Katiba ya Zanzibar,” alisema.
Chama hicho kimezitaka Mamlaka
zilizokabidhiwa jukumu ama la kiushauri au la kiutendaji chini ya katiba ya
Zanzibar hususan Mkurugenzi wa Mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Waziri
wa Katiba na Sheria, kuchukua hatua za dharura kuhakikisha watuhumiwa
waliosafirishwa nje ya Zanzibar wanarudishwa mara moja katika mahakama za
Zanzibar kwa mujibu wa sheria.
Pia kimeitaka Serikali ya
Zanzibat kuunda Tume Huru ya Uchunguzi itakayopewa jukumu la kuchunguza uhalali
wa kikatiba na kisheria wa maamuzi wa kuwakamata watuhumiwa na kuwasafirisha
nje ya Zanzibar na kuwakabidhi kwa mamlaka ambazo hazijaidhinishwa na katiba.
Aidha imeomba mamlaka
itakayoundwa ichunguzi malalamiko yote ya uvunjifu wa haki za binaadamu, mateso
na udhalilishaji waliyofanyiwa watuhumiwa kama walivyoyatoa mahakamani.
No comments:
Post a Comment