Habari za Punde

Bunge la katiba lakerwa taarifa za wajumbe kutolipwa posho

Na Benedict Liwenga, Maelezo, Dodoma

Ofisi ya Bunge Maalum la Katiba, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za wajumbe wa bunge hilo.

Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Jossey Mwakasiyuka, alitoa ufafanuzi huo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo, ambazo alisema zimelikera bunge la katiba.

Alisema ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa hizo kwani ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba wajumbe wa bunge maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato na kwamba ujumbe wa bunge maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa katiba kpya,” alisema.

Alisema si vyema kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya bunge maalum vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.

Akifafanua kuhusiana na malipo ya posho hizo, aliviambia vyombo vya habari kuwa, wajumbe wote wa bunge maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea wamelipwa posho zao zote kama wanavyostahili.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha kutoka hazina, na upatikanaji wa fedha kutoka benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika,” alisema.

Alivitahadharisha vyombo vya habari vinavyondika habari za Bunge Maalum kuzingatia maadili na kanuni za uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao vya bunge maalum ili taarifa kama hizo za upotoshaji zisijirudie tena.

“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini,” alisema.


Katika kanuni za bunge maalum, kanuni ya 77 inawataka waaandishi wa habari kuandika habari za bunge maalum kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ili kuondoa uandishi wenye kuleta chuki kati ya serikali na wananchi wake.

1 comment:

  1. Ukweli hasa hizi posho bora ziondoshwe hili bunge maalum lipate kwisha , zikisitishwa tu makubaliano yatapatikana . Na pesa hizo zote zitumike kwa mengine ya maana , likes , madeksi ya maskuli , magodoro ya hospitali , wasisubiri misaada tu

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.