Na Rehema Mohamed, Pemba
USHIRIKA wa ufugaji
samaki cha Chambani unakabiliwa na tatizo la soko la kuuzia samaki wao, ambapo
kwa sasa wana zaidi ya kilo 2,000 za samaki.
Kilo moja ya samaki
inauzwa kati ya shilingi 7,500 na 8,000, lakini kwa sababu ya ukosefu wa soko
la uhakika wanalazimika kuuza kilo moja kwa shilingi 2,000 hadi shilingi 2,500.
Akizungumza na mwandishi
wa habari hizi kijijini kwao Chambani, Katibu wa Ushirika huo, Nassor Suleiman
Nassor, alisema wakati mwengine hata bei ya shilingi 2,000 kwa kilo moja,
huikosa na baadhi ya samaki huwagawa kwa wanachama.
Alisema pamoja na
kuanzisha ushirika huo kwa lengo la kujikwamua na hali ngumu ya maisha, bado
wanakumbana na hali gumu kutoka na ukosefu wa soko.
Alisema ushirika wao
wenye wanachama zaidi ya 20, umeanzisha mradi wa ufugaji samaki ambao kwa kiasi
kikubwa umepata mafanikio lakini tatizo kubwa ni soko.
Samaki wanaofugwa ni
mwatiko, mizira na chaa na wanatarajia kuongeza samaki wa aina nyengine ambao
wanakubaliana na hali yoyote ya hewa katika kipindi cha kiangazi.
Mwenyekiti wa ushirika, Said
Omar Haji, alisema wamekuwa wakivuna samaki mara mbili ambapo, wastani wa kilo
4,000, kila mwaka hupatikana.
Mwenyekiti huyo alisema
mafunzo ya ufugaji samaki aliyapata China na aliporudi aliwafundisha wenzake
mbinu za ufugaji wa kisasa wa samaki.
No comments:
Post a Comment