Habari za Punde

ZAECA yamnasa trafiki kwa rushwa

Na Hafsa Golo
MALAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imemtia mbaroni askari wa usalama barabarani, Koplo Ramadhan Sheha akishawishi na kupokea rushwa ya shilingi 10,000 kutoka kwa mpanda pikipiki.

Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mussa Haji, alisema askari huyo alimatwa na maofisa wa ZAECA akipokea rushwa hiyo ili asimfikishe katika vyombo vya sheria mpanda pikipiki huyo.

Tukio hilo lilitokea Mwanakwerekwe Agosti 19 mwaka huu saa 7:00 mchana.

Alisema mpanda pikipiki ambae ni raia mwema anaepinga rushwa, alitoa ushirikiano kwa taasisi hiyo kuweza kufanikisha kukamatwa kwake.

Alisema tayari jalada la kesi linalomuhusu askari huyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.

Kuhusu mtu alietoa fedha hizo, hatashtakiwa kwa sababu ni raia mwema ambae hakuwa na dhamira ya kutoa rushwa na kwamba anaonekana kuchukia dhambi hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema taarifa hizo zipo, lakini hazijafikishwa rasmi na kumtaka mwandishi wa habari hizi awafuate ZAECA.


Aidha alisema vitendo vya rushwa kwa askari wa usalama barabarani vimekuwa vikishamiri katika maeneo ya Unguja na Pemba, hivyo wananchi wawe tayari kumfichua askari yeyote atakae kiuka utaratibu wa majukumu yake ya kazi.


Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kukomesha vitendo hivyo kwa sababu Zanzibar bila rushwa inawezekana.

1 comment:

  1. sawa wananchi watoe mashirikiano lakini hao wahusika mtawapa adhabu gani ili wakome?, au atasomewa shtaka halafu siku mbili aje atutie adabu tena barabarani? (ataendelea na kazi yake kama kawaida halafu alipize kisasi kwa huyo raia mwema).

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.