JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
|
Simu ya mdomo: 255 22 2460
735/2460 706-8
Nukushi: 255 22 2460 735/700 S.L.P.
3056
Unapojibu
tafadhali nakili:
Kumb.
Na.: TMA/1622 4
Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA OKTOBA - DISEMBA 2014
NCHINI
A: UTANGULIZI
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za masika
(Machi - Mei) 2014 na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa
kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2014(Vuli).
|
Dondoo
muhimu Mvua za Vuli Oktoba-Disemba, 2014



B: TATHMINI YA MVUA KIPINDI CHA MACHI – MEI, 2014
Katika msimu uliopita wa mvua za Masika Machi hadi
Mei, 2014. Maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya wastani
isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Mwanza, Singida na Dodoma ambayo yalipata
mvua za chini ya wastani. Matukio ya vimbunga hususan Kimbunga ‘Hellen’ kilichotokea
katika Rasi ya Msumbiji kusini magharibi mwa baharí ya Hindi kilisababisha
ongezeko la mvua katika eneo la Pwani ya kaskazini.
Maeneo
yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka:
Kanda ya Ziwa
Victoria: Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vya Bukoba na Musoma vilikuwa juu ya wastani. Kituo
cha Shinyanga kilipima mvua kiwango cha wastani wakati katika kituo cha Mwanza kiwango
cha mvua kilikuwa chini ya wastani.
Nyanda za juu
kaskazini mashariki: Vituo vya Arusha, Lyamungo na Kilimanjaro vilipima mvua
juu ya wastani ilihali vituo vya Moshi na Same kiwango cha mvua kilikuwa cha
wastani.
Pwani ya kaskazini
na visiwa vya Unguja na Pemba: Vituo vya Dar es Salaam, Morogoro na Pemba vilipima mvua za
juu ya wastani na vituo vya Zanzibar, Amani, Kizimbani pamoja na Tanga mvua zilikuwa
wastani.
Maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Nyanda
za juu kusini magharibi: Vituo vya Mbeya, Tukuyu, na Mahenge vilipima mvua
juu ya wastani na kituo cha Sumbawanga kiwango cha mvua kilikuwa cha wastani.
Kanda ya magharibi: Mvua juu ya wastani ilipimwa katika kituo cha Kigoma
ilihali vituo vya Kibondo na Tabora mvua zilikuwa ni za wastani.
Pwani ya kusini: Kituo cha Kilwa kilipima mvua juu ya wastani na vituo
vya Mtwara pamoja na Naliendele mvua
zilikuwa za wastani.
Kanda ya kati: Vituo vya Singida na Dodoma vilipima mvua
chini ya wastani na kituo cha Hombolo mvua za wastani.
Kanda
ya kusini: Kituo cha Songea kiwango cha mvua kilichopimwa kilikuwa juu ya wastani.
C: MIFUMO YA
HALI YA HEWA
Katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba,
2014 hali ya joto la bahari katika maeneo ya magharibi na kusini -magharibi mwa
bahari ya Hindi inatarajiwa kuwa juu ya wastani, upande wa mashariki mwa bahari
ya Hindi hali ya joto la wastani inatarajiwa.
Hali hii inatarajiwa kusababisha
upepo wenye unyevunyevu kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika eneo la
Pwani ya Africa Mashariki. Aidha, hali
ya joto la chini ya wastani katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki
(Pwani ya Angola) inatarajiwa kusababisha ongezeko la hewa yenye unyevunyevu
kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya magharibi na kusini
Magharibi mwa nchi.
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la
Tropikali ya bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi ya
Oktoba hadi Disemba, 2014. Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua
katika baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua. Hali ya joto la juu
ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi linaashiria
kuwepo kwa matukio ya vimbunga katika msimu wa mvua za Vuli kuanzia
mwezi Novemba, 2014.
D: MWELEKEO WA MVUA OKTOBA - DISEMBA 2014:
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya
hewa inayotarajiwa, mvua za kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014 zinatarajiwa
kuwa kama ifuatavyo:
(i)
Mvua za Vuli (kwa maeneo yanayopata misimu
miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (Vuli)
ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya
kaskazini, kanda ya Ziwa Viktoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Katika msimu huu mvua zinatarajiwa kuwa za
wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar
es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, pamoja na visiwa vya
Unguja na Pemba), nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha na Manyara) pamoja na mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na kaskazini
mwa mkoa wa Kigoma.
Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2014
katika ukanda wa Ziwa Viktoria na kusambaa katika maeneo mengine. Hata hivyo,
mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema katika maeneo ya ukanda wa pwani (Mkoa wa
Tanga na kisiwa cha Pemba) na katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini
Mashariki.
Kanda ya Ziwa
Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza katika
wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Septemba, 2014 katika mkoa wa Kagera na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Mvua hizo zinatarajiwa
kuwa za juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Mwanza
pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Maeneo mengi ya mkoa wa Shinyanga
yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Ukanda wa Pwani ya
Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na
Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi
Septemba, 2014 katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam pamoja na visiwa
vya Unguja na Pemba na kusambaa maeneo ya mkoa
wa Morogoro. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
katika maeneo mengi.
Nyanda za juu
Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza
wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa juu ya
wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na kaskazini mwa
mkoa wa Manyara. Hata hivyo, kusini mwa mkoa wa Manyara, mvua zinatarajiwa kuwa
za wastani hadi juu ya wastani.
(ii) Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni
mahususi kwa maeneo ya Magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini-magharibi, kusini
mwa nchi na pwani ya kusini. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014
maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi
(Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya
mwezi Novemba, 2014. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika
maeneo ya mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na kusini mwa mkoa wa Kigoma. Hata
hivyo, maeneo mengi ya mkoa wa Tabora yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi
juu ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa
ya Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya
mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini
Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya
pili ya mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
katika maeneo mengi. Maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Mbeya, mvua zinatarajiwa
kuwa juu ya wastani.
Maeneo ya kusini na
pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya
pili ya mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
isipokuwa maeneo mengi ya mkoa wa Ruvuma, yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani
hadi chini ya wastani katika baadhi ya maeneo.
Kielelezo: 1 – Ramani ikionesha Mvua – kushoto: Wastani wa mvua Mwezi Oktoba hadi Disemba;
Kulia: Mwelekeo wa Mvua katika msimu huu wa Oktoba hadi Disemba 2104.
Izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio mengi ya mvua
kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia
inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi
chini ya wastani.
Matukio ya Vimbunga
katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi yanatarajiwa kuchangia
katika mwenendo wa mvua nchini. Maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuathiriwa
zaidi na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati, Nyanda za juu Kusini Magharibi,
Magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani.
E: ATHARI
NA USHAURI
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua
za wastani hadi juu ya wastani isipokua baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi
yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Matarajio ya mvua
hizo pamoja na ushauri kwa baadhi ya sekta za kiuchumi na kijamii zimeainishwa
kama ifuatavyo;
Kilimo na Usalama wa
Chakula
Katika
maeneo mengi ya nchi hali ya unyevunyevu
wa udongo inatarajiwa kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo. Hata hivyo,
kwa maeneo machache ya kusini mwa nchi (hususan Mkoa wa Ruvuma) vipindi vya
upungufu wa mvua vinatarajiwa mwanzoni mwa msimu na hivyo kuathiri kiwango cha
unyevunyevu wa udongo. Hali ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi inayoambatana
na vipindi vya mvua kubwa inaweza kusababisha
ongezeko la magugu, matumizi makubwa ya pembejeo, hivyo kuongeza gharama za
uzalishaji. Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na pembejeo mapema pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa
kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.
Malisho na maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori
Hali ya malisho na upatikanaji wa maji
kwa ajili ya mifugo na wanyama pori inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi
nchini. Hata hivyo, wafugaji
wanashauriwa kuzalisha malisho na kuyahifadhi kwa matumizi wakati wa kiangazi. Aidha,
wafugaji wanashauriwa kufuata maelekezo ya wataalam wa ugani katika maeneo yao hususan
matumizi ya maji na malisho na
kukabiliana na magonjwa ya mlipuko
yanayoweza kujitokeza. Kutokana na hali ya mvua inayotarajiwa, matukio ya migogoro
inayosababishwa na mifugo, wanyamapori
na shughuli za binadamu na kilimo hayatarajiwi kujitokeza kwa kiasi kikubwa.
Maliasili
na Utalii
Mamlaka za usimamizi wa shughuli za
utalii na hifadhi za wanyamapori zina shauriwa kuchukua hatua stahiki katika kuzuia
uharibifu wa miundombinu kama barabara
na madaraja ndani ya hifadhi dhidi ya adhari za mvua kubwa na za juu ya wastani
katika maeneo husika. Aidha, wawindaji,
wapiga picha za kitalii na makampuni ya kitalii yanashauriwa kuchukua tahadhari
ya uwepo wa mafuriko kutokana na mvua zinazotarajiwa.
Maji na Nishati
Mtiririko wa maji katika mito na vina vya
maji katika mabwawa vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi
kutokana na mvua za msimu wa Vuli.
Pamoja na matarajio ya kuwepo kwa mvua za juu ya wastani inashauriwa kuwa maji
yatumike kwa uangalifu na kuzingatia taratibu za uvunaji, uhifadhi na matumizi
endelevu ya rasilimali maji.
Mamlaka za Miji
Inashauriwa
kuchukua hatua za kuhakikisha
kuwa mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi katika kiwango cha kutosha kuhimili mvua
zinazotarajiwa ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu
wa miundombinu, upotevu wa maisha na mali katika maeneo husika.
Sekta ya Afya
Ushauri unatolewa kwa jamii na sekta husika
kuchukua hatua stahiki katika kuzuia
milipuko ya magonjwa yanayosababishwa
na kutuama kwa maji na utiririshaji wa maji taka usiodhibitiwa katika
maeneo yao.
Menejimenti ya Maafa
Mamlaka za maafa na wadau wengine
wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji
wa maji safi na salama, na usambazaji wa madawa, maji na chakula ikiwa ni hatua
za kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na vipindi
vya mvua kubwa na mvua za juu ya wastani
zinazotarajiwa.
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia,
kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika
kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Aidha,
jamii nayo inashauriwa kufuatilia na kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa na
mirejeo yake kupitia vyombo vya habari.
Angalizo: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi
mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia
mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo
utazingatiwa katika uchambuzi wa
utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu
wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na wa mwezi kama
zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia mwenendo wa
mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU
No comments:
Post a Comment