Na Fatina Mathias, Dodoma
Rais Jakaya Kikwete, ameshangazwa na ufaulu wa chini
katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani
Dodoma na kuwataka viongozi kukaa chini na kujiuliza sababu ya kushuka kwa
ufaulu huo.
Agizo hilo alilitoa kwa nyakati
tofauti akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoa wa Dodoma.
Alisema kiwango cha ufaulu nchini kimekuwa
kikiongezeka lakini wilaya hizo zimeendelea kuwa chini kielimu.
"Mwaka jana katika wilaya ya Kondoa ufaulu katika
darasa la saba ulikuwa asilimia 23 na kwa kidato cha nne ulikuwa asilimia 46
ambapo katika wilaya ya Chemba kiwango cha ufaulu ni asilimia 19 wakati
lengo lililopo ni kuinua ufaulu hadi
kufikia asilimia 60 ili mwakani wafike kwenye asilimia 80,"alisema.
Kuhusu migogoro ya mipaka,aliahidi kukutana na Waziri Mkuu na viongozi wengine
wenye dhamana ili waweze kulipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa katika ziara
yake alipokea vilio vya migogoro hiyo.
Alisema wakati akipita katika
kijiji cha Haneti, wananchi walisimamisha msafara wake na kueleza kilio chao
cha mgogoro wa mipaka.
Aidha aliiagiza halmashauri ya
wilaya ya Chemba m kuhakikisha inatenga ardhi kwa ajili ya Shirika la Nyumba
(NHC) ili liweze kujenga nyumba bora kwa ajili ya watumishi.
Alisema wakiwapa ardhi NHC watawajengea nyumba bora na hivyo itaondoa visingizio vya
watumishi kwenda kukaa wilaya
nyingine ya Kondoa.
Alisema katika maeneo ambayo
NHC wamejenga makazi wamefanya vizuri kwa kuwa yatasaidia pia kuifanya wilaya
kuonekana na kupangika vizuri.
Aidha alisema hali hiyo
itawafanya wafanyakazi wasipate adha ya kupanga nyumba ambazo mazingira yake hayaridhishi.
Aidha alisema eneo la ujenzi wa
hospitali limepatikana na NHC wamekabidhiwa ili waweze kujenga na atawasaidia
kulisemea
suala hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa
Kusini, Juma Nkamia, alisifu afanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya CCM na kumpongeza Rais
na serikali yake kwa kufanikisha hilo.
No comments:
Post a Comment