Habari za Punde

'Hakuna malipo mengine kwa Hajj Mabruur isipokuwa pepo'


Abu ‘Ammaar

Tunapoazimia kwenda kufanya ibada ya Hajj, hatuna budi kujipanga katika mpangilio ambao tutahakikisha tutanufaika katika safari yetu hii muhimu katika kila Nyanja ya maisha yetu.

Ni fursa ambayo hutokea mara moja katika maisha hivyo si jambo la kulichukulia kiwepesi wepesi.

Ibaada ya Hajj ni miongoni mwa ibada muhimu kwa Muislamu ambazo Allaah Subhaanahu Wata’ala anazipenda na kuziridhia.

Na moja katika jambo la kulizingatia ni kujiandaa katika kuipata ile aina ya Hajj ambayo Mtume wetu Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam ameipa jina la Hajj Mabruur. Tusiende kuhiji tu bali tuazimie kwenda kuhiji hajj hii ya Mabruur.

فعن أبي هريرة – رضي الله عنه- قال: سئل النبي صلى الله عليه وسلم: أي الأعمال أفضل؟ قال: (إيمان بالله ورسوله)، قيل :ثم ماذا؟ قال: (جهاد في سبيل الله)، قيل : ثم ماذا؟ قال: (حج مبرور) "متفق عليه".

Kutoka kwa Abu Hurayrah , Allaah amuwie radhi amesema: Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam aliwahi kuulizwa: ‘Amali gani iliyokuwa bora? Akasema: Kumuamini Allaah na Mtume wake’ Pakasemwa:‘kisha kitu gani?’ Akasema: ‘Kupigana jihad kwa ajili ya Allah’ Pakasemwa: ‘ Kisha kitu gani?’ Akasema : ‘ Hajj Mabruur’ Bukhaari na Muslim.

Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam amemuhakikishia kila anaekwenda kuhiji kwamba ikiwa atafanya Hajj ili inayoitwa Mabruur basi malipo yake ni pepo kama alivyosema katika hadithi

والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة) "متفق عليه"

Hakuna malipo mengine kwa Hajj Mabruur isipokuwa pepo. Bukhaari na Muslim

Na hata Ummul Muuminiyna, Mama wa waumini, Aaishah, Allaah amuwie radhi, aliwahi kumuuliza Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi Wasallam

: يا رسول الله،ألا نغزو ونجاهد معكم، فقال عليه الصلاة والسلام: (لكُنّ أحسن الجهاد وأجمله الحج، حج مبرور)، قالت: فلا أدع الحج بعد إذ سمعت هذا من رسول الله صلى الله عليه وسلم) "رواه البخاري".

Ewe Mjumbe wa Allaah! Kwanini hatuwezi kupigana na kushirikiana nanyi kwenye Jihaad? Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam akasema: ‘Lakini Jihaad iliyokuwa bora na nzuri kwenu ni Hajj; Hajj Mabruur’. Bukhaari

Neno Mabruur linatokana na asli ya neno Birr katika lugha ya kiarabu na lina maana pana kwani linajumuisha tabia iliyotukuka, kutekeleza wajibu na kuhakikisha kila mwenye haki basi anapata haki yake.

Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam anasema ‘Birr ni tabia njema’ Pia aliwahi kuulizwa Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam kwamba kitu gani mtu afanye ili Hajj yake iwe Mabruur? Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam akasema :

 (إطعام الطعام وإفشاء السلام) "رواه أحمد".
 ‘kulisha watu chakula na  Kudhihirisha (kupeana) salam (baina yenu)’

Ili tuweze kuifikia Hajj Mabruur, ni wajibu kwa kila mwenye kujaaliwa kwenda safari ya Hajj kuhakikisha kila tendo atakalolifanya wakati wa kutekeleza ibada hii liko sahihi. Hivyo ni lazima ajielimishe vizuri taaluma ya Hajj, fardhi zake, wajibu wake, sunnah zake, makatazo yake kama vile ambavyo ametufundisha Mtume wetu Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam. Pia ahakikishe kwa kila jambo analolifanya anamfuata Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika kulitekeleza.

فعن جابر –رضي الله عنه- قال: رأيت النبي صلى الله عليه وسلم يرمي على راحلته ويقول: (لتأخذوا مناسككم فإني لا أدري لعلي لا أحج بعد حجتي هذه) "رواه مسلم".

Kutoka kwa Jaabir, Allaah amuwie radhi, amesema: Nilimuona Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam akirusha (mawe) akiwa katika kipando chake (msimu wa Hajj) na akasema: ‘Chukueni kutoka kwangu matendo ya Hajj, kwani sina hakika kama nitahiji (tena) baada ya Hajj yangu hii’ Muslim

Ili Hajj ifikie darja ya kuitwa Mabruur lazima ifanyike kwa Ikhlaas ya darja ya juu kabisa. Kwasababu kuwepo Ikhlaas ni moja ya masharti muhimu ya kukubaliwa ibada ya mja. Ikhlaas ni ile hali ya kufanya ibaada si kwa jambo lengine lolote isipokuwa kutaka radhi za Allaah Subhaanahu Wata’ala pekee. Ndiyo maana Mtume Swala Allaahu ‘Alayhi wasallam anatukumbusha wakati tukifanya Ibada hii muhimu kuomba dua’a

( اللهم حجة لا رياء فيها ولا سمعة رواه ابن ماجة

“Ewe Mola (tunakuomba utuwafikishe kwa) Hajj isiyokuwa na Riyaa (kujionesha) wala  majivuno (ya kutajwa na watu) “. Ibnu Maajah.

Masahaba ambao walimfahamu vyema kigezo cha kuigwa katika matendo mema kwa Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam kwani Anas bin Maalik, Allaah amuwie radhi ,

إذا أحرم لم يتكلم في شيء من أمر الدنيا حتى يتحلل من إحرامه

Akishahirimia (kwa ajili ya Hajj) hakuwa akizungumza jambo lolote katika mambo ya kidunia mpaka anapomaliza Ibada yake.

Tumuombe Allaah Subhaanahu Wata’ala atujaalie na awajaalie Wageni wa Arrahmaan Hajj mabruur na Dhambi zilizosamehewa, Sa’ay yenye kushukuriwa.

Tumuombe Allaah Subhaanahu Wata’ala awafanyei wepesi kwa wote waliotia nia ya kwenda kuhiji na awawafikishe katika Hajj kwa kuwatakabalia Ibaada zao na maombi yao

  Aamiyn Aamiyn.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.