Na Ramadhani Ali, Melezo
Mkurugenzi wa Idara ya hospitali
za Mnazimmoja,Dk. Jamala Adam Taib, amesema kazi kubwa inayofanywa na idara
hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2010 ni kuimarisha hospitali ya
Mnazimmoja ifikie kiwango cha hospitali ya rufaa.
Alisema hatua zinazochukuliwa
na idara ni kuimarisha miundombinu,
kusomesha wataalamu wa fani tofauti za afya, kuimarisha uchunguzi wa maradhi na
kuhakikisha dawa zinapatikana.
Alimueleza Waziri mpya wa Afya,
Rashid Seif Suleiman, alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kuangalia
utendaji wa kazi na changamoto zinazoikabili.
Alisemamajukumu yote
waliyopangiwa katika kuimarisha hospitali
kuu ya Mnazimmoja yamefikia hatua nzuri na hivi sasa wananchi wamejenga
matumaini makubwa kutokana na huduma zake.
Alisema idara ya hospitali za
Mnazimmoja ina wafanyakazi 800 wakiwemo
madaktari bingwa 14 na serikali
inaendelea kusomesha wataalamu wa fani mbali mbali ambapo wanafunzi 200 wa fani ya udaktari wapo vyuoni.
Pamoja na mafanikio makubwa
yaliyofikiwa na hospitali kuu ya Mnazimmoja, alisema bado inakabiliwa na
ufinyu wa bajeti na mageuzi.
Msaidizi Mganga Mkuu wa hospitali
kuu ya Mnazimmoja, Dk. Muhidini Abdalla Mohamed. amemueleza Waziri wa Afya ambae
alifuatana na Naibu wake, Mahmoud Thabit Kombo, kwamba kliniki ya meno ya hospitali hiyo ina vifaa vya kisasa kutoka shirika la MCW la Marekani
na kuifanya kuwa kliniki bora zaidi
kuliko hospitali nyengine za Zanzibar.
Aliwahakikishia wananchi kwamba
huduma za matatizo yote ya meno
zinapatikana kwenye kliniki hiyo na kuwataka wananchi kutokuwa na wasi wasi na
waendelee kuitumia.
Katika kitengo cha maradhi ya
kisukari, Daktari Msaidizi wa maradhi hayo,Miskia Ali Mohammed alimueleza
Waziri kwamba maradhi hayo yanaongezeka
kwa kasi na kumekuwa na upungufu mkubwa wa dawa.
Alisema tatizo jengine linalokikabili
kitengo hicho ni upungufu wa chakula cha wagonjwa wa kisukari wanaolazwa
ambacho kinatakiwa kiliwe sambamba na matatibabu wanayopatiwa ili dawa wanazotumia zifanye kazi kwa ufanisi.
Waziri wa Afya kwa upande wake
aliwataka viongozi wa idara hiyo
kuimarisha umoja na mshikamano na watendaji
wao ili kufanikisha malengo yaliyoweka
ya kuwahudumia wananchi na kuwapa huduma nzuri.
No comments:
Post a Comment