Na Khamis Haji, OMKR
Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim
Seif Sharif Hamad, amesema migogoro inayowakumba wakulima na wafugaji na
kusababisha mauaji inasababishwa na serikali kukosa sera sahihi ya kilimo na ufugaji.
Aliyasema hayo katika mikutano
tafauti akiwa katika ziara ya siku nne mkoani Mwanza kwa ajili ya kuzindua
miradi ya maendeleo iliyo chini ya kata zinazoongozwa na CUF pamoja na
kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Akizungumza na wananchi baada
ya kuzindua daraja katika kata ya Igogo, alisema inasikitisha kuona kila siku
wakulima na wafugaji wakiuana kwa kugombea maeneo ya kilimo na kulishia mifugo
huku serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo.
Maalim Seif ambaye pia ni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema kusingekuwa na mauaji kati ya
wakulima na wafugaji iwapo serikali ingekuwa na sera thabiti inayoanisha maeneo
maalum kwa ajili ya ufugaji na wakulima.
Alisema Tanzania imejaliwa
maliasili nyingi kuliko nchi nyingi duniani na iwapo zingeweza kuzitumika
vizuri hakuna sababu nchi kuwa miongoni mwa nchi masikini.
Alisema mbali na maliasili
zilizopo chini ya ardhi kama vile madini, gesi na mafuta, Tanzania imejaaliwa
kuwa na hali ya hewa inayotafautina katika maeneo ambayo inaifanya nchi
kuzalisha mazao tafauti tafauti.
Hata hivyo, alisema kukosekana
kwa sera muafaka kunasababisha wananchi walio wengi kushindwa kunufaika na
neema hiyo na kutoa mfano, licha ya wananchi wa kanda ya Ziwa kuongoza kwa
kilimo cha Pamba, lakini hakuna hata kiwanda cha nguo.
Akihutubia katika mkutano wa
hadhara katika uwanja wa Furahisha Kirumba, alisema wananchi hawana budi
kujiandaa kufanya mageuzi ya uongozi wa nchi kwa kuwaweka madarakani viongozi
wenye uwezo na mtazamo mpya wa kuleta maendeleo ya wananchi.
Naye Mbunge wa Nyamagana
kupitia CHADEMA, Ezekiel Wenje, akihutubia katika mkutano huo alisema njia
muafaka ya kuleta mageuzi ya kiuongozi nchini ni vyama vya upinzani kuendeleza
ushirikiano na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote.
Alisema yeye binafsi yuko
tayari kufadhili safari ya viongozi wakuu wa CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi
wakajifungie nchini Sychelles ili waweze kupata mgombea mmoja ambaye
watamsimaisha kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani kupitia Ukawa.
Hata hivyo, akilifafanua hilo,
Maalim Seif alisema jambo hilo wala halihitaji kwenda kuamuliwa nje ya nchi, na
badala yake viongozi hao wanaweza kutoa maamuzi hayo hapa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment