Na Joseph Ngilisho,Arusha
Mtoto Lowasa Ingine (15), mkazi
wa kijiji cha Sepeto, wilayani Monduli,amelazwa hospitali ya Seliana, iliopo mjini
Arusha, baada ya kujeruhiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kwenye mikono yake
miwili.
Akizungumza kwa shida katika
hospitali hiyo, alisema siku ya tukio Septemba 7 mwaka huu, majira ya saa 8:00
mchana alikuwa kwenye eneo la jeshi ambalo lilitumika kufanyia mazoezi ya kivita
Septemba 5 mwaka huu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya jeshi hilo.
Alisema wakati akiwa eneo hilo
kwa ajili ya kuchunga ng’ombe yeye na wenzake waliokota kitu kinachofanana na
chuma.
“Nilipookota nilikuwa na
wenzangu, wakati nikikiangalia na huku nikijaribu kufungua,ghafla nikasikia
kishindo na kikaanguka chini na kupoteza fahamu,”alisema.
Alisema baada ya kushituka
alijikuta yupo hospitalini na tayari kiganja chake cha mkono wa kulia na mkono
wa kushoto kimekatwa vidole vinne na kubakiwa na kidole kimoja.
Kaka wa mtoto huyo,, Miage Ingine,
alisema mdogo wake alikwenda eneo la jeshi kuchunga ng’ombe akiwa na wenzake
watatu, akiwa huko ng’ombe alikanyaga kitu ambacho kiliripuka na kumkata mdogo
wake mikono na ng’ombe kukatika miguu.
“Baada ya tukio hilo tulipata
taarifa kutoka kwa majirani zetu na tukaenda kuwachukua ambapo tuliwapeleka
hospitali ya wilaya Monduli ambako walihudumiwa na wenzake kwa kuwa hawakuumia
sana waliruhusiwa ila mdogo wangu aliyekatwa vidole na kiganja tuliamuriwa tuje
Selian,”alisema.
Alisema baada ya tukio hilo
walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kijiji chao, ambaye aliahidi kupeleka taarifa
jeshini.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali
hiyo, Dk. Geofrey Kichira, alithibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa amepoteza kiganja
na vidole tisa.
“Mtoto huyu tumempokea na
tunaendelea kumpatia huduma na hali yake inaendelea vizuri tofauti na
alipofika,”alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa JWTZ, Kanali Erick Komba,
akizungumza kwa njia ya simu, alisema jeshi halina taarifa na tukio hilo na
wanalifuatilia.
No comments:
Post a Comment