Habari za Punde

Mwakyembe awachimba mkwara madereva wa treni

Na Fatina Mathias, Dodoma.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atawafukuza kazi madereva wa treini watakaobainika kuiba mafuta au kutumia vibaya mali ya shirika la Reli Tanzania.

Alitoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na madereva wa shirika hilo katika semina iliyowakutanisha madereva wote kwa lengo ya kupeana mikakati ya kuliendesha shirika hilo kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uelewa na uaminifu madereva hao.

Alisema ni ukweli kwamba madereva wengi wanatuhumiwa kwa wizi wa mafuta pamoja na kutumia vibaya mali ya shirika hilo jambo ambalo linasababisha kuwepo uharibifu mkubwa wa mali ya serikali.

Alisema hakuna dereva atakaeonewa aibu atakapobainika anahusika na wizi au uharibifu wa mali ya shirika.


Alisema pamoja na serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika shirika hilo, bado kuna watumishi wanaoendelea na tabia zao za wizi wa mafuta, kutokuwa waaminifu katika kuendesha vichwa vya treini pamoja na mabehewa jambo ambalo linasababisha hasara kubwa.

Alisema pamoja na kuwepo wizi wa mafuta bado serikali imeweka utaratibu wa kuboresha maisha ya
madereva wa treni ambao watafikisha mizigo yao vizuri katika vituo vyao.

Hata hivyo, madereva hao wamelilalamikia shirika hilo kwa madai kuwa wafanyakazi wana masilahi duni kuliko hata madereva wa daladala.


Mmoja wa madereva hao, Adrof Mwabugale, alisema maisha ya madereva wa treni yamekuwa magumu zaidi kutokana na shirika kutowathamini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.