TAARIFA
YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201
KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Sisi Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi
za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili
kubwa.
Tukiamini kuandaa Katiba Mpya kwa
maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi wote, tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu
Kitaifa. Aidha tunaamini kwamba katika
kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo na fikra inayotolewa
na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya kidemokrasia kwa kupiga kura
na kukubaliana na matokeo ya wengi.
Kama ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya
kuanza shughuli za Bunge Maalum, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu
na mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na
ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi
Mungu amsaidie.
Tumeshangazwa na kusikitishwa sana
kuona kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hili kwa
wananchi, unachafuliwa taswira yake.
Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli zake kuingiliwa na
kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge, Makundi, Taasisi na Vyombo
mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za BungeMaalum la Katiba
unapotoshwa. Wananchi wanaaminishwa yasiyo
na ukweli.
Upotoshwaji
huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na bado
linaendelezwa kama ifuatavyo:
1. Kwamba Bunge Maalum
la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu walioondoka wameliondolea
uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo Bungeni basi uhalalai wake utakuwepo -
utapatikana;
2. Inadaiwa kwamba
Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo;
3. Inadaiwa pia,
kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si Rasimu
iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyowasilishwa rasmi Bungeni
na kuanza kujadiliwa na wajumbe;
4. Inadaiwana
watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201, wanapewa rushwa. Isitoshe Vyombo vya
habari vimeandika tuhuma kama hizi.
5. Inadaiwa pia
kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache, ukilinganisha na hao
walioko nje ya Bunge hilo;
6. Bunge hili,kwatuhuma
hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
Kabla ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji
huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201
katika Bunge Maalum la Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato
wa kutayarisha Katiba Mpya ulivyo kisheria.
Tunapenda kuwafahamishaWatanzania
wenzetu kwamba mchakato huu una hatua tatukwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Mpaka hivi sasa nihatua moja
imekamilika. Hatua ya pili ndiyo inayoendelea,na
hatua ya tatu bado haijaanza.
Hatua ya kwanza ni ile ya uandaaji wa
Rasimu. Sheriaya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, chini ya kifungu cha tano cha sheria hiyo. Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na
kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya
wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba.
Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi cha takriban miaka miwili na hatimaye
Rasimu ya Katiba ilikamilika.
Hatua ya pili ilikuwa ni kuipeleka
Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli
maalum ya kuandika Katiba inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao
wataamua waikubali au waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho. Hawa ni Watanzania wote wenye uwezo wa kupiga
kura kwa kutoa maoni yao. Hoja ya Mamlaka
ya Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania ili
kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili.
Tunachoweza kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza
Katiba inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi waipigie kura ya maoni. Hatua hii ya pili bado inaendelea.
Hatua ya tatu ni pale Bunge Maalum la
Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa
wananchi ili waikubali kama wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi
matarajio yao.
Hatua hii ni ya mwishowananchi
wakiikubali tunapata Katiba Mpya wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.
Kilichotokea ni kwamba, wajumbe
wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua kuukiuka utaratibu uliowekwa kisheria. Badala yake wamepeleka Rasimu ya Katiba kwa
wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba inayopendekezwa bado
haujakamilika.
Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini,
ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu
katika jamii, tumesikitishwa sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi
na makundi, taasisi na vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge
hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato
huu. Tuna wajibu wakusahihisha upotofu
huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali
halisi inayojiri hapa Bungeni.
Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe. Hali ni shwari. Mchakato unaendelea kwa amani na utulivu.
Katika kusahihisha upotofu
unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo mbali mbali katika jamii, tunaomba
kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-
TUHUMA KWAMBA BUNGE
MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI
Jambo
hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni ambao
wamewekwa na kutambuliwa kisheria. Hawa
ni kama wafuatao:
1. Wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Wajumbewa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
3. Wajumbe 201
walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na Taasisi, Mashirika na
makundi mbali mbali nchini,
Uhalali waBunge unakuwapo wakati
wajumbe kutoka makundi hayo matatu wapo Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee. Iwapo kwa mfano wajumbe wa 201 wakiamua
kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja muhimu ya Bunge
haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo.
Hata hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la
Katiba zimeweka idadi ya akidi ambayo ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge
Maalum. Akidi hii ikifikiwa Bunge huendelea
na shughuli zake. Akidi hii hufikiwa
kila wakati BungeMaalum linapokutana. Hii
inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha shughuli zake kwa misingi
ya sheria na taratibu zilizojiwekea.
Bunge lina uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
TUHUMA KWAMBA KANUNI
ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA
Suala hilo halijawahi kutokea. Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa
nawajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria Namba
83. Vile vile uendeshaji wote wa
shughuli za Bunge zinafanywa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum. Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge Maalum
kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni
Namba 87.
WARAKA
MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME
Hili nalo si kweli. Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi
kama Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa
ujumla tunasema hii si kweli.Ni upotoshaji wa makusudi. Tunaijadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ibara kwa ibara. Ibara nyingi
zimeachwa kama zilivyo. Kuna ibara ambazo
zimeboreshwa au kurekebishwa, kuna ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya
ambazo zimewekwa ili kuweka mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au
haikuyaona.
WAWAKILISHI WA
TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA
RUSHWA
Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini na
Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge hili tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa
na baadhi ya watu, na kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia
kwenye mijadala, midahalo na makongamano mbali mbali.
Baadhi yetu sisi Viongozi waKiroho tumeapishwa viapo vya uadilifu katika
uongozi wetu wa kiroho na tuko mstari wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka
dhambi ya tamaa ya fedha, na kusema uongo.
Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini au nafasi zetu za kipekee
katika uongozi wa kiroho. Taarifa hizi
zinatangazwa kwa makusudi na watu mbali mbali
kupita vyombo vya habari kwa malengo ya kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi
wa kiroho mbele ya umma. Tunaomba tabia
hii ikomeshwe.
TUHUMA KWAMBA BUNGE
KUWA NA WAJUMBE WACHACHE
Hili nalo si kweli. Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi
inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.
HOJA
YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM
Hii ni hoja inayozungumzwa katika
mijadala mbali mbali katika jamii.
Msingi wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa
kupeleka taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa
mwelekeo. Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa
maananikwa kuwa hakuna sababu za msingi na za kisheria za
kufanya hivyo.
HITIMISHO
Kumekuwa na taarifa mbali mbali zenye
malengo ya ama kuingilia shughuli za Bunge hili au kutudhalilisha sisi wajumbe
ambao si Wabunge au Wawakilishi. Wajumbe201,
ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali umekuwa na uzito wa
pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo zimejaa malengo ya kisiasa zaidi
kuliko ukamilishaji wa shughuli za Bunge Maalum.
Kuna taarifa nyingine zimesambazwa
zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo
zina wajumbe wake katika Bunge Maalum.
Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo hapa
Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli na ili
kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na Kimataifa. Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi
wajumbe ambao kwa hiari yetu tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo
tulitumwa tuje tuyakamilishe.
Kama tulivyosema hapo awali ni wajibu
wetu kama Viongozi wa Dini na Wajumbe wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi
katika shughuli za Bunge Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu
ukweli na wawaheshimu watanzania kwa kuwaeleza ukweli.
Ahsanteni sana.
……………………. …………………………
SHEIKH HAMID
MASOUD JONGO ASKOFU AMOS JOSEPH MUHAGACHI
BAKWATA KIKRISTO
TAREHE 3
SEPTEMBA, 2014
No comments:
Post a Comment