Na Mwantanga Ame,Dodoma
KAMATI za Bunge Maalum la
Katiba, zimepinga ukomo wa kushika nafasi za ubunge, kama ilivyopendekezwa
katika rasimu ya katiba na kutaka mfumo wa sasa uendelee.
Mwenyekiti wa Kamati namba 2,
Shamsi Vuai Nahodha, aliwasilisha maoni ya wengi jana katika sura za tisa na
10, alisema ameamua kufanya mabadiliko ya sura hiyo, kwa kuondoa ukomo wa
kutumikia nafasi hiyo kwa vipindi vitatu kama ilivyopendekezwa na rasimu na
badala yake liwachwe liendelee kama ilivyo sasa.
Alisema Tanzania inafuata mfumo
wa kidemokrasia na haitakuwa busara uhuru huo ukabanwa pale watu wachache watakapoona
kwao ni sawa kumuondoa mbunge huyo.
Alisema mabadiliko mengine
ambayo kamati hiyo ilipinga ni ushikaji
wa nafasi pale Mbunge aliyechaguliwa atakapoondolewa ama kufariki kwa nafasi
yake kushikwa na mtu alieshika nafasi ya pili.
Alisema hatua hiyo inaweza
kuzua visa vya makusudi, kwa mtu ambaye alishika nafasi ya pili ambaye anaweza kufanya
jambo lolote litakalochangia kuondolewa
kwa mbunge aliechaguliwa.
Maeneo mengine ambayo aliyataja
kufanyiwa marekebisho ni kuwepo mahakama
ya juu, ambayo itafanya shuhuli zake vyema kwa vile hivi sasa kazi kubwa
imekuwa ikifanywa na mahakama ya rufaa.
Nae mjumbe wa kamati namba 10,
Dk. Kafumu, alisema wajumbe walio wengi wanapendekeza ibara hiyo ifutwe na
badala yake wananchi waachwe kutuimia demokrasia yao.
Kuhusu elimu ya mgombea kuwa elimu
ya kidato cha nne, alisema haipaswi
kuwekwa ibara hiyo kwa kuwa hakuna nchi inayofuata kigenzi hicho na inaweza
kuwanyima wananchi haki ya kumchagua mtu wamtakae.
Mjumbe Mahmoud Mussa Abdalla,
akitoa maoni ya kamati yao namba 9, alisema
suala la haki ya kupiga kura ya kumwajibisha Mbunge, wajumbe wa kamati
hiyo walipendekeza ibara 129 ifutwe na
kuandikwa upya, kwa kuzingatia nafasi ya mbunge ni ya muda maalum.
Alisema ibara mpya itaelekeza
kwamba bunge litakuwa na mamlaka ya kutunga sheria itayoweza kuwawajibisha wabunge
ambao wataonekana kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Nae mjumbe Pindi Hadhara Chana,
akitoa amaoni ya kamatu namba moja, alisema Makamu wa Pili wa Rais kama ataonekana
kukiuka katiba, kamati yake imependekeza suala hilo lipelekwe bungeni na kama
bunge litaridhia, maamuzi yatapelekwa Baraza la Wawakilishi, ambalo nalo
likishindwa kumuwajibisha basi suala hilo litafikishwa mahakama ya katiba.
Hata hivyo, wajumbe wengine
walipinga suala la uondoshwaji wa nafasi za wanawake kwa kupendekeza nafasi
hizo sasa ziwe zinafanyika kwa wilaya.
No comments:
Post a Comment